Ngurumo No. 1558 Jumamosi, Mei 9, 1964
KORTI ya kijeshi lililokuwa likiendelea
kusikiliza kesi ya askari walioshitakiwa kufanya maasi nchini Tanganyika
linatoa maoni yake juu ya yote korti hiyo iliyokusanya wakati wa kusikiliza
ushahidi, siku ya Jumatatu tarehe 11 saa tatu na nusu asubuhi.
Habari hii ilitangazwa na Sir Ralph Windham, Mwanasheria Mkuu wa serikali ambaye ni Rais wa Korti hiyo jana baada ya Bwana Hebert Chitepo, Mkurugenzi wa Mashitaka alipomaliza kulihutubia korti hilo kwa saa zipatazo tatu na dakika chache: Alieleza mashitaka ya serikali juu ya washitakiwa na kujibu utetezi wa Bwana Roden, Wakili wa washitakiwa.
Katika hotuba yake, Bwana Chitepo alieleza wazi kabisa, kwamba washitakiwa wanashitakiwa kushiriki kitendo ambacho kingeleta utumiaji nguvu, ama kitisho cha kutumia nguvu.
Bwana Chitepo akaeleza kuwa maasi ni kitendo cha namna fulani kifanywacho kwa njia fulani kinachotumia nguvu. Ikiwa mtu anahakikishwa kuwa kashiriki katika vitendo hivyo, basi kashiriki katika kufanya maasi. "Na ushahidi umethibitisha kuwa maasi kwa namna hiyo yametokea. Mtu yeyote ambaye alishiriki, ama amefanya kitendo hicho, ameshiriki katika maasi.
Bwana Chitepo akasema kuwa Bwana Roden katika hotuba yake aliwataja Alic na Hingo na watu wengine watatu kuwa hawakuhusika kabisa na vitendo vya nguvu, lakini maadamu watu hao wameshiriki katika kitendo kilichotishia utumiaji wa nguvu, hiyo yatosha watu hao kuhukumiwa.
Akieleza mpango wa maasi ulivyochukuliwa, Bwana Chitepo alisema kuwa kweli yaonekana kila kitu kilifanyika kwa mpango. Akautaja mpango huo kama wenye hatua tatu. Kwanza ilikuwa kuwatia nguvuni watu waliokuwa katika zamu ya kulinda, pale Kwota Gadi.
Kweli, akasema, maafisa kama Makaranga walitiwa ndani.
Baada ya hapo, kuwaita maofisa ambao hawakuwapo kwa alam. Hiyo ilifanywa. Kisha ndiyo aitwe Bwana Kambona. Na hivyo ndivyo hasa ilivyotokea. Kama alivyosema shahidi Tobias.
Wapendavyo
Bwana Chitepo akaendelea kueleza kuwa baada ya pale ilikuwa askari hawana budi kuchukua silaha. Maana jambo hilo ni la kutotaka kuwatii wakubwa wao na ili wapate kufanya wapendavyo wao ..’.
Kusema kuwa maofisa Wazungu hatuwataki, tutie wengine tuwapendao. Bila shaka wasingeweza kufanya hivyo. Kisha kama madai ni ya fedha, ilikuwa wahakikishe kuwa Jamhuri haitumii jeshi lake lolote jingine, askari hao walitoka kambini kwao na kuja mpaka mjini na kuziingilia njia za uchukuzi. Wakaenda kwenye kiwanja cha ndege kuzuia pengine jeshi lolote jingine lisije likasaidia serikali. Maafisa wa polisi walifukuzwa ofisini mwao.
"Kwa mambo ya aina hii, kila mtu ambaye alishiriki katika vitendo kama hivi, akasema Bwana Chitepo, ni mhalifu, anastahili adhabu iliyomo katika sheria. Bwana Chitepo akasema kuwa sheria yenyewe ni pana sana inaanzia tangu mtu kutumia nguvu mpaka chini kabisa kama kosa la kukataa kutii.
Msemaji
Bwana Chitepo akamtaja Baltazar. Baltazar, alisema, yeye hapa kortini anajifanya kama msemaji wa wenziwe kadhaa. Na hapa hapa, washitakiwa saba hivi wamekubaliana naye". Akasema Baltazar ameungana kuwa yeye mmoja katika wale ambao walikubali kufanya kitu tofauti walichokuwa wanafanya kuendelea kutoa madai yao. Chacha, akaendelea kusema Bwana Chitepo, kila mtu aliyepelekwa Gadirum alimwona kwenye mlango wa Gadirum. Akataja mashahidi kadhaa ambao katika ushahidi wao walimtaja Chacha.
Kuhusu Mwanaloya ambaye Roden alikubali kuwa yeye hakufanya lolote ila kampeleka Hospitali na kumrudisha Kanal Nyirenda nyumbani. Bwana Chitepo akasema kuwa baada ya pale, Kanal Nyirenda katika ushahidi wake alisema kuwa funguo za motokaa yake zilichukuliwa. Ushahidi kwamba Mwanaloya alishiriki katika matendo yale, hauna wasiwasi.
Kifupi chao
Kuhusu Hingo na Alic Bwana Chitepo akasema atasema juu yao kwa kifupi tu. Alic, akasema, alisema alipochajiwa na Kamanding Ofisa kuwa alichukuliwa akamchukue Bwana Kambona kwa kumtishia. Baadaye akasemwa na Kanal Nyirenda kuwa Alic ndiye aliyetishwa. Akaeleza kuwa tangu alipochukuliwa, kwenda State House, kwenye uchaguzi wa maofisa, mpaka kwenye Education Centre, haionyeshi hata kidogo kuwa alichukuliwa kwa kutishwa. Lakini ilikuwa katika mpango wa kuendeleza Plan yao.
Hingo akasema Bwana Chitepo, kwa sababu zisizojulikana, katika maofisa wote walioitika mwito wa king’ora yeye alichaguliwa kuwasemea askari.
Mwafrika No. 851 Jumatatu Oktoba 29, 1962
KWA mfululizo kesi za uvutaji bangi zimesikilizwa katika korti ya Mwanza mbele ya Hakimu Bwana Hill. Ajabu ni kwamba katika kesi hizo nyingi ziliwahusu wafungwa walioko jela.
Akimhoji mshitakiwa mmoja, Hakimu alisema kuwa ‘mwezi uliokwisha nimekwisha kuhukumu kesi nyingi za wavuta bangi’.
Mwandishi wetu aliyeko Mwanza anasema kuwa uvutaji wa bangi unaelekea umeenea sana katika Mwanza. Hivi majuzi tu mwanamke mmoja alivuta bangi na baadae akampiga mtu mmoja.
Mwanamke huyo alikamatwa na kupelekwa kwa
Liwali. Huko akatozwa faini.
Uhuru Na. 4,971 Jumanne, Mei 15, 1979
Na Mwadini Hassan
MAREHEMU Hussein Tindwa aliyekuwa mchezaji wa Klabu ya kandanda nchini Simba, alizikwa jana kwenye kiunga cha makaburi ya Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa, mjini Dar es Salaam.
Marehemu alifariki Jumamosi iliyopita alipokuwa akiichezea timu yake ilipopambana na Raccah Rovers ya Nigeria katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya mashindano ya kutafuta klabu bingwa ya Afrika, kwenye uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam.
Ripoti ya madaktari walioufanyia uchunguzi mwili wa marehemu imesema kwamba Hussein Tindwa alifariki kutokana na maradhi ya moyo.
Maelfu ya wapenzi wa kandanda waliohudhuria mazishi hayo akiwemo Waziri wa Utamaduni wa Taifa na Vijana Chadiel Mgonja, mwakilishi wa Balozi wa Nigeria nchini Tanzania, Kamisaa wa pambano kati ya Simba na Raccah Rovers Tambwe Mgandelu kutoka Zaire na viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo, walionekana kujawa na huzuni wakati maiti ya marehemu ilipokuwa mazishini.
Wachezaji wote wa Simba walifika kwenye mazishi hayo na walilia waziwazi wakati maiti ya marehemu ikiteremshwa kaburini, wakiwa na majonzi makubwa ya kumpoteza rafiki na mchezaji mwenzao.
Vile vile makelele ya vilio vya akina mama wengi yalisikika katika kila upande wa eneo hilo la mazishi na hali yote ya sehemu hiyo ilikuwa ya majonzi makuu.
Akizungumza kwenye wakati huo mgumu, Mwenyekiti wa Simba Luka Luhui alisema kwamba kifo hicho kimeleta pengo na mshtuko mkubwa kwa miongoni mwa wachezaji wa Simba na ana matumaini kwamba Wizara itaweka kumbukumbu ya mwanamichezo huyo ambaye amefariki akilitetea taifa katika michezo.
Akijibu hotuba hiyo, Waziri wa Utamaduni wa Taifa na Vijana, Chediel Mgonja alisema kwamba hayati Tindwa amekuwa shahidi na mfano wa kudumu katika utekelezaji wa siasa ya Taifa kuhusu michezo.
Aliahidi kwamba Wizara yake kwa kushirikiana na vyombo vya michezo na wananchi watafikiria njia ya kuhakikisha kumbukumbu ya kudumu ya marehemu Tindwa.
Wengine waliotoa hotuba za rambirambi kwenye mazishi hayo ni Mwenyekiti wa FAT, Said El Maamry, Mwakilishi wa Balozi wa Nigeria, kiongozi wa Raccah Rovers, Umoja wa Vijana wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Yanga Kristofa Mahimbo.
Klabu ya Simba imetangaza maombolezo ya siku tatu kuanzia jana.
Michango mbalimbali imetolewa kusaidia familia ya marehemu. Baraza la Michezo la Taifa limetoa shilingi 2,000/-, FAT shilingi 1,500/-, Wafanyakazi wa Wizara ya Utamaduni na Vijana shilingi 685/30, Klabu ya Chui Shilingi 300/-, Coastal Union ya Tanga, Yanga na Chama cha Kandanda mkoani Dar es Salaam shilingi 500/- kila moja na wafanyakazi wa bandari (Block B) shilingi 131/30.
Salam za rambirambi ziliendelea kumiminika katika Klabu ya Simba kutoka kwa klabu za michezo na watu mbalimbali nchini Tanzania.
Mwafrika, No. 443, Jumatano Machi 22, 1961
CONGRESS na AMNUT wametupwa nje na Bwana Koloni. Hawatakuwamo katika mkutano wa siasa utakaoanza Jumatatu ijayo. Kelele zimejaa mitaani kwamba TANU inapendelewa na watawala wa Kikoloni na ya kwamba Bwana Nyerere amekwisha kupatana na Macleod mambo fulani.
AMNUT wamesema, "Tumetupwa nje ili tusiingie katika lile jumba la Karimjee Hall, ndani ya mkutano na kuchafua mambo ambayo wakubwa wamekwishapatana".
Congress wakasikitika, "Tumekataliwa maana TANU haitaki vyama vya upinzani. Wanataka watawale wao peke yao tu".
Hapo hapo jana, Congress ilieleza masikitiko yake kwa vile Yusi Ligi yao ilikatazwa kuandikishwa serikalini.
Katibu Mkuu wa Congress Michael Sanga akasema, "Tumeambiwa kuwa eti Yusi Ligi yetu itachafua amani ya nchi. Mimi sikubaliani na sababu hiyo. TANU inaona kwamba Yusi Ligi wao wamefanya visa mitaani, sasa wanaogopa kuwapa nafasi Yusi Ligi wetu tukawaonyesha kuwa tunataka amani, bila machafuko".
Hakuna Uhuru
Congress na AMNUT walipoulizwa kwanini hawakukaribishwa kwenye mkutano wa siasa, walijibu kuwa "wameonelewa, wala njia iliyotumiwa siyo ya demokrasia".
Bwana Abdul Wahyd Karim, Katibu Mkuu wa AMNUT alisema "Kukataliwa kwetu kuingia katika mkutano kunatufanya tuwe na hakika kuwa uhuru sio mwaka huu wala mwaka ujao. Kungekuwa na uhuru mwaka huu, nasi tungealikwa ili tukatoe maoni yetu.
Wapeleke maoni
"Tumeambiwa kuwa tupeleke maoni yetu kwenye mkutano huo. Sisi tunaona kuwa huko ni kutudharau, wala hatutapeleka maoni yetu yakawafaidie watu ambao hawatujali".
Bwana Karim alisema kwamba AMNUT ilimwonya Macleod, asifanye habari na chama kimoja cha siasa, yaani TANU peke yake. Haki ni kusikiliza maoni ya kila upande.
Congress leo watafanya mkutano wa waandishi wa magazeti hapo watakapoeleza malalamiko yao kwa serikali, kwa vile hawakualikwa mkutanoni.
Ngurumo Na. 1059, Jumatano, Septemba 19, 1962
T.B.C ilitoa vipindi vitatu kwa Congress kutangaza ili kuwajulisha watu ambao hawataweza kufikiwa na kila kiongozi, siasa maalum ya Congress. TANU ilipewa vipindi sita na Bwana Nyerere atangaze siasa yake ili ambao hawataweza kumuona wapate kusikia kwa kutokana na redio. Alisema Bw. D. K. Masanja katika taarifa aliyoipa Ngurumo.
Bwana Nyerere bila shaka hakufurahishwa na shauri hilo, la kuwa pamoja na Bwana Mtemvu katika T.B.C. kwa kuwa amezoea kila jambo kufanya bila kupingwa! Amekataa kama yeye hatatangaza au hatatumia T.B.C. katika uchaguzi huu kwa kueneza siasa yake, hapo hapo T.B.C. baada ya kuona Nyerere kakataa nao wamemzuia Mtemvu kutumia T.B.C. kwa kuwa Nyerere kakataa. Iwapo Mtemvu angekataa kutumia T.B.C., T.B.C. ingemzuia Nyerere pia? Chama changu na wanachama wangu tunafahamu wazi kama Baba wa Taifa kaogopa kutangaza siasa yake pamoja na Mtemvu katika nyumba moja, pia ameona kama akimwachia atapike siasa yake pekee si ajabu baba wa taifa akakosa hata zile kura za wanachama wake, na hata moja asipate.
T.B.C. haikufanya haki
Hata hivyo T.B.C. haikufata haki kwa kuwa baada ya Bwana Nyerere kuogopa kutumia TBC pamoja na Mtemvu, amewasukuma watoto wake yaani Maregion na Ma Areas Commissioners kutangaza siasa yao katika T.B.C. kila siku, na hivi si haki, lazima ifahamike kama wale Ma Region Commissioners wanaotumia T.B.C. ni wanasiasa, na wanaelewa wazi kama wasipofanya vile huenda Mtemvu akashinda ndio wao watakuwa wamekwisha.
T.B.C. lazima ijihadhari na isijiingize katika mambo ya siasa, ikae tayari kupokea chama chochote cha siasa kinachotawala kuwa serikali yako. Na lazima iwakataze hao wanasiasa tokea leo kutumia T.B.C. katika Campaign na kama haitaki kuwakataza, Congress haitasita kufikiria njia itakayowakataza hao wanasiasa kutumia sauti ya Tanganyika.
|
|