SERIKALI ya Tanzania imewataka wananchi wake kuacha kununua maji ya chupa (Bottled or Mineral water) yasiyokuwa na nembo (alama) ya ubora inayotolewa na shirika la viwango Tanzania (TBS).
Kauli hiyo ya serikali ilitolewa na Naibu Waziri wa Viwanda, Mama Shamim Khan katika kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichomalizika mjini Dodoma hivi karibuni.
Katika taarifa hiyo, serikali ilikiri kuwa hivi sasa hapa nchini kuna makampuni yasiyosajiliwa ambayo yanajishughulisha na utengenezaji na uuzaji wa maji ya chupa.
Swala la kuwataka wananchi waache kununua maji ya chupa yasiyokuwa na nembo ya TBS ni sawa na serikali kutaka kukwepa wajibu wake katika swala zima la kuwaondolea wananchi kero na hatari ya kunywa maji yasiyokuwa safi wala salama.
Kauli yangu ya hapo juu ninaiegemeza kwa hoja tatu zifuatazo:
Kwanza, kwa vile serikali yenyewe imekiri kuwepo kwa makampuni yanayozalisha na kuuza maji ya chupa bila kusajiliwa, na kwa vile watu wanauza maji ya chupa ambapo si safi wala salama, dawa pekee ya haraka ya kuwanusuru Watanzania na hatari hiyo ni serikali kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara hao wasiokuwa waadilifu na wasiokuwa na huruma na binadamu wenziwao.
Pili, ufanisi wa utekelezaji wa mambo kadhaa kama hili la nembo ya TBS unategemea sana kiwango cha elimu ya walengwa. Nikizingatia ukweli huu wa kiwango cha elimu walichonacho wananchi wengi (walalahoi) wa Tanzania, nashindwa kuielewa serikali kama kauli yake ni ya kisayansi au ya kisiasa (ionekane kama inaondoa kero kumbe hakuna kitu).
Hata tukiwatazama hao wasomi, ni mara ngapi wasomi hao hutazama nembo ya TBS, hasa akiona chupa inavutia na kufungwa vizuri? Ni ukweli usiopingika kuwa utekelezaji wa jambo hilo ni mgumu. Jambo la kwanza la kufanya ni lile nililopendekeza katika hoja ya awali.
Tatu, nembo pekee siyo dawa. Mwishoni mwa mwaka jana (1998), baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sayansi wakishirikiana na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu kimoja cha nchini Marekani walifanya utafiti juu ya maji ya kunywa, yakiwemo yale ya chupa.
Katika utafiti huo, kama ulivyowasilshwa na wasomi hao mwaka jana katika semina iliyofanyika idara ya Kemia, imegungulika kuwa karibu maji yote (pamoja na yale yaliyokuwa na nembo ya TBS) yaliyofanyiwa utafiti yalikuwa na kiwango kikubwa cha madini ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Pia, baadhi ya maji yalikuwa na vijidudu (coliforms). Hivyo nembo ya TBS pekee siyo dawa.
Wafanyabiashara ambao si waaminifu hutengeneza bidhaa za ubora wa hali ya juu wakati wanatafuta nembo ya TBS. Wakishapata hawana habari tena na ubora wa bidhaa, bali ni kupunguza gharama!
Kinachotakiwa kufanywa ni TBS kukagua viwanda hivyo na pia kuchukua bidhaa na kuzipima. Lakini TBS ni shirika la umma. Linategemea fedha kutoka serikalini. Serikali nayo tunaisikia kila kukicha haina fedha. Tunajiuliza TBS inakagua viwanda na kupima vyakula (maji n.k.) vilivyomo katika maduka?
Ni katika hali hii ninasema kuwa nembo pekee siyo hoja. Serikali isikwepe wajibu wake. Vinginevyo Watanzania tutakwisha.
Hitma yasambaratisha Uislamu Magogoni
WAKATI Masheikh na Masheikh mjini hapa wakiendelea kufitiniana kwa vyombo vya dola, Uislamu na Waislamu wa Kijiji cha Magogoni, Tarafa ya Mvuha wanaelekea kubaya kufuatia kutokuwa na elimu sahihi juu ya dini yao imefahamika.
Akiongea na gazeti hili hivi karibuni Mama maarufu wa kijiji hicho Fatma Abdallah amesema kuwa hali ya Uislamu kijijini hapo ilikuwa mbaya kipindi cha nyuma na kufanya Msikiti wa zamani kuliko yote katika kata ya Ukutu kuwa ghala la kuhifadhia pamba badala ya nyumba ya kufanyia ibada.
Ameendelea kusema kuwa baadaye hali ilikuwa nzuri kidogo baada ya kufika wasomi wachache na kuondoa pamba iliyokuwemo ndani ya Msikiti na watu wakaanza kuswali kama zamani.
"Lakini sasa hivi hali imekuwa mbaya kutokana na Maustadh wa Msikiti wa Magogoni kupiga marufuku hitma na maulidi wakisema vitu hivyo ni haramu bila ya kuvitolea maelekezo zaidi ambapo vitu vyote hivyo tumevirithi kutoka kwa babu na bibi zetu", alisema Mama Fatuma Abdallah.
Kutokana na mtafaruku huo, Waislamu wa eneo hilo wakasusia kuswali Msikiti huo na kwenda kuswali katika Msikiti mdogo katika eneo la Kiganila ambapo huko nako mambo yakawa kama ya Msikiti wa Magogoni kupiga marufuku vitu hivyo.
Katika mparaganyiko huo ambapo baadhi ya Waislamu wamedai kuwa wangeelimishwa kwanza kuhusu mambo hayo kabla ya kupigwa marufuku, wamefanya kampeni kubwa ya kuwakataza watoto wao wasisome katika madrasa zilizopo katika Misikiti hiyo wala kuswali wao wenyewe hali iliyopelekea Msikiti huo kuwa gofu na baadaye kuanguka.
Hivi sasa baadhi ya Waislamu wa eneo hilo inadaiwa kuwa wamehamia katika Msikiti wa Kibumuloa umbali wa kilomita 10 kutoka Magogoni na wamemuandaa kijana wao aitwaye Omar Mguenga ili awaendeshee ibada zao pamoja na madrasa ya watoto wao.
Kufuatia tafrani hiyo, inadaiwa kuwa Makanisa nayo yamejipenyeza katikati na kufanikiwa kuwabatiza wazee mashuhuri wa Kiislamu wa Magogoni pamoja na vijana kadhaa hali ambayo imepelekea Waislamu wengine kuamua kutokuwa upande wa dini yoyote na kufanya mambo yao vile waonavyo wao.
Imamu wa Msikiti wa Kiganila Abdallah Selemani Mkundi alipoulizwa na gazeti hili kuhusu Waislamu kuukimbia Msikiti, Madrasa kufa na Msikiti kudondoka kutokana na yeye kupiga marufuku hitma pamoja na maulidi alisema ni afadhali aswali peke yake.
"Ni afadhali kuswali peke yangu kuliko kushirikiana na watu wenye kupenda Maulid pamoja na hitma vitu ambavyo ni haramu", alisema Abdallah Selemani Imam wa Msikiti wa Mkundi.
Magogoni ni kijiji kilichopo kilomita 16 kutoka Mvuha ni eneo lililofikiwa na Waislamu tangu karne ya 18 na ndio Msikiti wa kwanza katika eneo lote la Ukutu. Kufuatia hali hiyo Masheikh ‘wakubwa’ wa Mjini wameombwa kwenda kuokoa hali hiyo kijijini hapo.
Wakati huo huo, Waislamu wa kijiji cha Kolero mkoani Morogoro wanahitaji msaada wa mabati yasiyopungua 34 pamoja na mifuko 15 ya saruji kwa ajili ya kumalizia Msikiti wao waliouanza kuujenga kijijini hapo.
Taarifa iliyotolewa na Sheikh wa Kanda ya Mlimani katika Kata ya Kolero hivi karibuni, Sheikh Ally Mwinshehe Malenge imesema kuwa mpaka hivi sasa wamejitahidi kuujenga Msikiti huo na nguvu za Waislamu wa eneo hilo zimeonekana kuwa ni ndogo kufuatia hali ya ukame iliyokikumba kijiji hicho ambapo wamelazimika kuziandikia barua taasisi mbalimbali za Kiislamu na kuwaomba Waislamu popote pale walipo kusaidia ujenzi wa Msikiti huo.
Katika barua zilizotumwa ambazo gazeti hili ilipata nakala zake imebainisha kuwa mtu yeyote mwenye uwezo wa chochote katika hivyo avipakie katika magari yanayokwenda Mvuha na vikabidhiwe ofisi ya Tarafa Mvuha ambapo wao watakwenda kuvifuata hapo.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kijijini hapo, kuna wakazi wasiopungua 2,500 na kati yao asilimia isiyozidi 20 ni Waislamu, kwa muda mrefu eneo hilo limekuwa halina Msikiti.
Mnamo Januari, 1990 Sheikh Ally Mwinshehe kutoka kijiji cha Dutumi alifika kijijini Kolero kwa lengo la kuwalingania Waislamu wa huko. Baada ya kuelekeza nia yake hiyo kijijini hapo, alitokea bibi mmoja Fatuma Kiboko pamoja na mumewe Bw. Sadiki Athumani na kujitolea eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti.
Katika juhudi za Sheikh Mwinshehe akisaidiwa na Bw. Abdallah Omar Chivi pamoja na Mzee Omar Kiombwe katika mwaka huo wa 1990 walifanikiwa kuanzisha madrasa pamoja na kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti ambapo hali hiyo kwa kiasi fulani ilisaidia kusimamisha Uislamu.
katika kijiji hicho ambacho wakazi wake wengi walikuwa wakiabudu mizimu na miungu mingine waliojiundia wenyewe.
Akiongea na Waislamu wa eneo hilo hivi karibuni, Sheikh Hussein Hassan Kawambwa amesema hali ya Uislamu Kolero inazidi kuwa mbaya.
"Ndugu zangu Waislamu wa Kolero hali ya Uislamu hapa Kolero inazidi kuwa mbaya kila kukicha kwa sababu watu wamezama sana katika shiriki", alisema Sheikh Hussein.
"Kolero ni eneo maarufu sana katika Uluguru kwa mizimu, lakini hivi sasa baada ya kuingia katika Uislamu mambo hayo yanamuudhi Mwenyezi Mungu hivyo watu wayaache mara moja", aliongeza kusema Sheikh Hussein.
Naye Sheikh Ally Mwinshehe amesema Waislamu wa Kolero wajihadhari sana na pombe pamoja na nyama ya nguruwe ambapo vitu hivi vimekuwa vya kawaida kutumiwa na wakazi wengi wa Kolero wakiwemo baadhi ya Waislamu.
|
|