Wanafunzi na hijabu
Salamu alaykumu, jamii Isilamia,
Wanafunzi Isilamu, hapa kwetu Tanzania,
Hili ni langu jukumu, maonyo kuwaletea,
Livaeni vazi lenu, la hijabu lipendeza.
Sheria ilililiwa, kwa serikali sikia,
Hijabu kuruhusiwa, kina mama Tanzania,
Ruhusa ilitolewa, Mwinyi kutangazia,
Livaeni vazi lenu, linakinga maasia.
Lakini nawashangaa, hasa ninyi wanafunzi,
Vazi mmelikataa, aloamuru Mwenyezi,
Lengo lenu natambua, kuonyesha yenu ngozi,
Livaeni vazi lenu, Mungu kawachagulia.
Mna matatizo gani, mnakataa hijabu,
Mnamuasi Manani, na kuzikosa thawabu,
Mwapendelea vimini, hijabu mwaona tabu,
Livaeni vazi lenu, linausitiri mwili.
Mnasingizia joto, hijabu mnazivua,
Mtayapata majuto, akhera nawaambia,
Muingizwe kwenye moto, huku mkijililia,
Livaeni vazi lenu, heshima kujipatia.
Joto mnalosema, si joto nawaambia,
Mtalikuta Qiyama, joto hili mara mia,
Uwanjani kusimama, huwezi hata kimbia,
Livaeni vazi lenu, ni zuri lawapendeza.
Wengine wanavyosema, eti wanaona haya,
Mitaani kuwasema, na kuzomewa vibaya,
Wanaogopa shutuma, sura zao kuwa mbaya,
Livaeni vazi lenu, uzuri ni palepale.
Kuna malengo mwataka, nusu uchi kujivika,
Wawaone kina kaka, ili waje kuwataka,
Sahani ikifunikwa, cha ndani kusitirika,
Livaeni vazi lenu, kubakwa siyo rahisi.
Wengine wakishavaa, wanapokwenda mashuleni,
Njiani wanavivua, vilemba vyao kichwani,
Dunia yawahadaa, wataonekana duni,
Livaeni vazi lenu, hijabu ina stara.
Ninaishusha kalamu, usia ukumbukeni,
Wazazi nanyi walimu, lazima kuwa makini,
Kwa shule za Isilamu, adhabu wapatieni,
Hijabu vazi makini, mbona hamtafakari.
Zabibu I. Ng’onda,
Mwadui.
Uwe mtu wa Unguja, Marekani ama Lamu,
Sisi sote ni wamoja, jambo hili ufahamu,
Wana wa baba mmoja, baba yetu ni Adamu,
Wanadamu mfahamu, sisi sote ni wamoja.
Rangi zetu sio hoja, zitugawanye sehemu,
Tukachukiana waja, tukawekeana sumu,
Tukaikosa faraja, katika yote misimu,
Wanadamu mfahamu, sisi sote ni wamoja.
Mithili uzi na koja, tushikane binadamu,
Tuimarishe umoja, tucheke tutabasamu,
Peponi tuwe pamoja, ikishapita hukumu,
Wanadamu mfahamu, sisi sote ni wamoja.
Hivi sasa ipo haja, hili linatulazimu,
Kuacha vyetu viroja, vilivyoshika hatamu,
Si raia sio “soja”, tusipangiane zamu,
Wanadamu mfahamu, sisi sote ni wamoja.
Uwe bado ni kikana, au mtu wa makamu,
Umesoma sana sana, elimu umehitimu,
Usije ukajiona, mja utajidhulumu,
Wanadamu mfahamu, sisi sote ni wamoja.
Tuache kubaguana, hilo jambo lisidumu,
Si usiku si mchana, nawaambia wanadamu,
Popote tukionana, tutoleane salamu,
Wanadamu mfahamu, sisi sote ni wamoja.
Ikiwa tutapendana, tukaacha uhasimu,
Atafurahi Rabana, mema akatukirimu,
Mambo yetu yatafana, ninaapa kwa Karimu,
Wanadamu mfahamu, sisi sote ni wamoja.
Nawaaga waungwana, chini naweka kalamu,
Si vizuri kutengana, kila kukicha “taimu”,
Twamuudhi Subhana, ambae ndiye hakimu,
Wanadamu mfahamu, sisi sote ni wamoja.
Hamis S. Mketto (Mwagabona)
c/o Bw. Abubakar Ahmed,
S.L.P. 2880,
Dar es Salaam
Kafungwa mwana tumbili, na nyanyagi nyanyagiri,
Wimbo huo mashuhuri, kuimbwa na wanawari,
Dini wanaibadili, Masheikh hivi vizuri?
Hivi Kombe la harusi, ni nini maana yake?
Zuberi Mohamed Mwinyi (Amir)
S.L.P. 61428,
Dar es Salaam.
Hakika wako ujumbe, wa swali kwa waungwana,
Wataka kujua kombe, la harusi yake ma’ana,
Si kombe bali uzembe, kwa hayo uliyoona,
Na kwamba haina maana, kuwa kombe la harusi.
Ikiwa hali ni hio, ya hayo uliyonena,
Hayo ni maandalio, kuwa karibu na zina,
Pabaya kwa mafikio, na kombe hapo hapana,
Imeshapotezwa maana, kuwa kombe la harusi.
Wapo hawajui dini, halafu wabishi sana,
Walipo wapo gizani, japokuwa ni mchana,
Wameweka harusini, kitu ambacho hakuna,
Wameshapoteza maana, kuwa kombe la harusi.
Kuna chakula “walima”, kwa Bwana harusi Sunna,
Hupikwa chakula chema, huliwa na wavulana,
Pia na akina mama, huko nyumbani kwa Bwana,
Na ndiyo khasa maana, kuwa kombe la harusi.
Bwana harusi akiwa, na rafikize vijana,
Chakula hicho huliwa, huku wametulizana,
Si kwa nyimbo kuimbwa, kelele hakuna tena,
Na ndiyo khasa maana, kuwa kombe la harusi.
Namalizia tamati, kwa yanayoonekana,
Katika huu wakati, kwamba kombe hili jina,
Kwa dini hatulipati, wala halikufanana,
Kwa hiyo haina ma’na, kuwa kombe la harusi.
Jumanne Shaibu Undi (Abu Khair),
Al-Madrasatu Fiisabiilillah,
S.L.P. 61588,
Kinondoni, Dar es Salaam.
|
|