Tangu kompyuta za aina ya PC zianze kutumika hasa kuanzia mwaka 1982 mpaka leo hii, kifaa maarufu kinachotumika kuchukulia mafaili ya kompyuta ni disketi. Kifaa hicho kimekuwa maarufu sana kiasi kwamba watumiaji wengi wa kompyuta hawawezi kabisa kukamilisha kazi zao bila ya kuwa na disketi. Kitu kisichojuilikana na wengi ni kuwa, disketi ni kifaa ambacho kinaweza kuharibika kwa urahisi sana kama hakikutunzwa ipasavyo. Kwenye makala hii inshaallah tutaziangalia njia kadhaa zinazoweza kuiharibu disketi yako.

Njia hizo ni za "uhakika" lakini ni za wazi mno – chambilecho waingereza, ni "nobrainer" – yaani hazihitaji kuwa na akili nyingi kujua kuwa disketi itaharibika ikikutwa na masaibu yaliyotajwa hapo juu. Na wala tusingekuwa na haja ya kupoteza muda kuzungumzia njia hizo. Badala yake, njia tutakazozizungumzia ni zile ambazo ni za uhakika lakini hazieleweki sana.
Itasaidia maelezo yetu kwanza tukifahamu kuwa disketi inatunza data kwa kutumia smaku (electromagnetism). Disketi zimefanywa kwa kutumia maadini kama chuma (iron) na cobalt ambayo yana sifa ya kuweza kirahisi kabisa kufanywa kuwa smaku. Kompyuta ikiandika data kwenye disketi kwa kutumia head iliyo kwenye floppy disk drive (inayofanyakazi karibu sawa na head ya cassette recorder inayorekodi kwenye kaseti za kawaida za radio), data hizo huhifadhiwa kama vipande vidogo vidogo sana vya smaku vyenye mpangilio maalum. Maadini yanayotumika kwenye disketi yana sifa kuwa, yakishafanywa kuwa smaku, si rahisi kupoteza nguvu hiyo ya smaku iliyonayo. Ndio maana disketi zikaweza kuhifadhi data kwa muda mrefu.
Kwa vile disketi inatunza data kama vipande vidogo vodogo vya smaku vyenye mpangilio maalum, mpangilio huo ukiharibika basi data hizo zitashindikana kusomeka. Njia ya uhakika ya kuuharibu mpangilio huo ni kwa kuipitisha disketi kwenye kitu chochote kile chenye nguvu za smaku za kutosha kuchafua mpangilio huo.
Vitu vya kawaida vinavyotoa nguvu za smaku ni pamoja na mota (motor) za aina zote. Karibu kila mashine ya umeme yenye kitu kinachozunguka inatoa nguvu za smaku za kutosha kuiharibu disketi. Kwa hivyo ukiiweka disketi, kwa mfano, juu ya feni linalozunguka, disketi hiyo inaweza kuharibika. Air-conditioner, nayo inatoa nguvu za smaku za kutosha za kuiharibu disketi.
Vile vile, ukiiweka disketi yako karibu na jenereta (generator) la umeme linalofanyakazi, inaweza kuharibika. Kama jenereta (au mota) ni kubwa sana, ukiingia tu kwenye chumba chenye mashine hiyo wakati inafanyakazi, kama una disketi inaweza kuharibika. Hii ni kwa sababu, kila mashine ikiwa na nguvu zaidi ndivyo inavyotoa nguvu za smaku kubwa zaidi.
Spika (speaker) zote zinatumia smaku. Kila spika ikiwa na nguvu zaidi basi ujue kuwa ina smaku yenye nguvu zaidi. Ukiiweka disketi yako yenye data, juu ya spika kuna uwezekano mkubwa wa kuharibika. Kwa hivyo usiweke disketi, kwa mfano, mbele ya radio, au juu ya radio.
Simu zenye "mechanical ringer" , yaani zile zinazolia kama kengele mtu anapokupigia simu, kengele yake inafanyakazi kwa kutumia nguvu za smaku. Ukiiweka disketi yenye data karibu sana na simu ya namna hiyo disketi yako inaweza kuharibika. Simu zenye "electronic ringer" hazina tatizo hilo lakini kwenye simu karibu za aina zote ule mkono wa kusemea na kusikilizia (handset) ndani yake mnawekwa smaku, kwa hivyo ukijisahau ukauweka mkono huo juu ya disketi yenye data, disketi hiyo inaweza kuharibika.
Monita yako (na televisheni) inatoa nguvu kubwa sana za smaku kila unapoiwasha, na inatoa nguvu kidogo za smaku wakati ikifanyakazi. Disketi yenye data itakayowekwa chini ya umbali wa futi moja kutoka kwenye monita (au TV) inaweza kuharibika. Kwa hivyo usikiweke kisanduku unachohifadhia disketi karibu na monita au televisheni.
Ukitembelea kinu cha umeme (power station), kama pale Ubungo, na ukawa umechukua disketi yenye data na ukawa futi chache kutoka kwenye nyaya zinazochukua umeme wenye nguvu kubwa sana, disketi yako inaweza kuharibika. Hii ni kwa sababu nyaya za umeme za namna hiyo zinatoa nguvu kubwa sana za smaku za kutosha kuiathiri disketi yako.
Ukisafiri kwa ndege usipite na disketi (au hata kompyuta ya kubeba mkononi, yaani laptop), kwenye ile sehemu yenye "metal detector". Kwenye viwanja vingi vya ndege sehemu hiyo ni mahali unapoambiwa upite penye nguzo mbili – moja kulia na moja kushoto – ili kuweza kungundulika kama umechukua kitu chenye chuma. Kwenye baadhi ya viwanja vya ndege, kama kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam (DIA) na cha Kilimanjaro (KIA), hawana metal detectors za namna hiyo, badala yake wanakupapasa mwilini kwa kutumia "portable metal detector" ambayo hutoa sauti kama imekugundua una kitu cha chuma.
Metal detectors zinafanyakazi kwa kutumia nguvu za smaku, kwa hivyo zinaweza kirahisi sana kuiharibu disketi yenye data na hata hard disk drive iliyo kwenye laptop. Ni vyema kupitisha mkoba wenye disketi na laptop kwenye ile sehemu yenye X-ray. Kuna wanasayansi wawili walifanya utafiti maalum mwaka 1993 kuhusiana na athari ya X-ray kwa data zilizo kwenye disketi na wakachapisha ripoti yao waliyoipa kichwa, "Airport X-rays and floppy disks: no cause for concern," ("X-ray za viwanja vya ndege na disketi: hakuna cha kuogopa,"), kwenye jarida lenye jina, Computer Methods and Programs in Biomedicine. Tafsiri ya sehemu ya dibaji ya ripoti hiyo inasema hivi:
Njia zisizohusiana na vyanzo vya smaku, ambazo zinaweza kuiharibu disketi yako ni pamoja na kuiacha disketi yako kwenye jua kwa muda mrefu. Kwa hivyo kama ni kati ya wale wenzangu mimi wanaokwenda kwa miguu muda mrefu kwenye jua la Dar es Salaam, ukiwa umebeba disketi, kwa mfano kwenye mfuko wa shati, inaweza kuharibika.
Uharibifu unaweza kutokezea pia kama umeiweka disketi kwenye chanzo chochote kile cha joto – kwa mfano juu ya jiko, juu ya friji, juu ya taa, n.k.
Disketi za siku hizi zimezibwa vizuri na haziwezi kuingia mavumbi kirahisi. Ukijaribu kuifungua na kusababisha kuingia mavumbi, au kwa makosa ukiigusa sehemu inayohifadhi data na kuacha hata alama tu ya vidole (finger prints) , basi inaweza kuharibika.
Ukiipinda disketi yenye data inaweza kuharibika. Ukiandika juu yake kwa kutumia kalamu au penseli kwa kudindiza inaweza kuharibika. Ukitembea na disketi kwenye mfuko wa nyuma wa suruali ni njia ya uhakika ya kuweza kuiharibu kwani ni rahisi sana kuikalia na kuipinda. Hata ukiitia kwenye mkoba pamoja na vitu vyengine vigumu kuna uwezekano wa kuipinda na kuiharibu. Kwa kifupi unatakiwa uitunze vizuri sana disketi yako ili isiweze kuharibika
Kwa kumalizia, tungependa kusema kuwa, unaweza kuchukua tahadhari zote lakini data zilizo kwenye disketi yako ni jambo la uhakika kuwa hazitaweza kudumu milele. Hii ni kwa sababu, hii dunia (earth) nayo ina nguvu za smaku za asili. Ijapokuwa nguvu hizo sio kubwa, lakini taratibu zinaweza kudhoofisha nguvu za smaku zilizo kwenye disketi. Chambilecho waswahili, "Bandu bandu, huisha gogo!". Vipande vidogo vidogo vya smaku tulivyovitaja hapo juu vinavyokuwa ndani ya disketi, navyo pia huathiriana vyenyewe kwa vyenyewe. Baada ya miaka kadhaa disketi inaweza kupoteza nguvu zake na hivyo kupoteza data.
Kama una data muhimu, ni jambo la busara kuhifadhi nakala za data hizo kwenye disketi angalau mbili tafauti – ili kama moja ikiharibika uweze kuitumia nyengine. Lakini zaidi ni kuwa, kila baada ya miezi kadhaa, inapendekezwa uchukue disketi mpya na uzitunze data zako kwenye disketi hiyo mpya. Unaweza kutumia disketi hizo hizo za zamani kama utazi-format upya na kutunza tena ndani yake nakala za data zako. Ni muhimu kuzi-format upya ili uweze kuwa na kumbukumbu zote zikiwa na smaku ya kutosha.
Kwenye disketi, hakuwekwi data tu, bali kuna na kumbukumbu nyengine zinazosaidia kuifanya disketi iandikike na isomeke. Kumbukumbu hizo huandikwa mara moja tu unapoi-format disketi yako. Baada ya muda, kwa sababu tulizozitaja hapo juu kumbukumbu hizo hufutika na kuifanya disketi isisomeke. Ndio maana ikapendekezwa kui-format upya. Ushauri huo pia unapendekezwa unapotumia disketi ya zamani, japokuwa haijapata kutumika. Unapoanza kuitumia disketi yoyote ile, hata kama imesemwa kuwa ishakuwa-formatted basi na wewe i-format upya kabla ya kuitumia, ili kuzipa uhai kumbukumbu zote.
Baada ya maelezo hayo, bila shaka sasa utakuwa
umezifahamu njia zote za UHAKIKA zinazoweza kuiharibu disketi yako yenye
data, zaidi ya kuisukumizia jiwe, au kuikaanga kwenye karai!
|
|