Na Alhaj Yusuf Kalala,
Washington DC, USA
KWANZA kabisa nawaomba radhi wasomaji wa makala zangu katika ANNUUR, kwa ukimya mrefu uliopita kati yetu, ambao sababu zake zilikuwa kando ya uwezo wangu wa kuzizuia. Katika kipindi hicho cha ukimya, nilifurahi sana kupata wasaa wa kuisoma makala ya ndugu yangu Mwapwani Mohamed ambayo aliandika ikifuatilia makala zangu zilizoandikwa kuhusu (i) Kuutafuta Ufalme wa Kisiasa na (ii) Silaha yetu ni kura ya pamoja.
Maoni ya ndugu yangu Mwapwani Mohamed ni mazuri sana na tena ni bora zaidi. Na makala yake kwa jumla ni yenye manufaa sana na pia ni yenye mwangaza mkubwa mno, hapa duniani na hali kadhalika kule akhera. Naitazama makala ya Mwapwani Mohamed kama ni nyongeza nzuri ya maoni niliyoyatoa katika makala zangu nilizozitaja hapo juu. Haya ndiyo yatakiwayo, ya kukosoana, kuelekezana na kushirikiana.
Lakini mimi naona kuwa ni vizuri kama watu mkiwa katika Baraza la Mjadala wowote ule na mnataka kuelewana kwa kubadilishana mawazo, la msingi linakuwa ni lile la kuzingatia somo linalojadiliwa. Ikiwa mmoja yumo katika somo moja na mwingine anajadili somo tofauti, mjadala unakuwa hauna budi kukorogeka na lugha kugongana. Na matokeo ya mjadala huo hayatakosa mushkeli ndani yake.
Ufalme wa Allah, anaouzungumzia ndugu yangu Mwapwani Mohamed, ndio ulio bora kuutafuta kuliko falme zote zingine ambazo mwanadamu anawajibika kuzitafuta. Kazi hii ni ya kudumu kwa kila mtu katika maisha yake yote, tangu kuzaliwa mpaka kuagana na dunia hii tuliyonayo, hilo ndio la muhimu kuliko jingine lolote lile liwalo. Hakuna wa kulipinga hilo.
Katika makala zangu, mimi sikuwa katika somo hilo la ndugu yangu Mwapwani Mohamed. Labda nitoe mfano mwepesi, ambao hata kijana mdogo sana atauelewa. Katika Uislamu, swala imehimiwa sana kwetu kuliko ibada nyingine zote. Tumeamrishwa kuswali mara tano kila siku. Kwa hiyo Waislamu tunahimizana na kukumbusha kuswali mara kwa mara. Lakini swala ina sharti zake na mpangilio wake. Pamoja na yote, mahali pa kuswali, tunaambiwa ni lazima pawe safi, nguo azivaazo mswali lazima ziwe safi na pia mwili wake na hata hivyo awe ametawadha.
Sasa mimi nazungumzia suala la kusafisha mahali pa kuswali, ndugu yangu Mwapwani Mohamed anazungumzia kuswali. Hakuna lililo baya kati ya hayo yote mawili. Ila tu mimi naona kuwa hayo ni masomo mawili ambayo yanaweza kuzungumziwa moja baada ya jingine au moja kabla ya jingine, lakini siyo yote kwa pamoja na kwa wakati mmoja. Mjadala utakorogeka, lugha zitagongana na wasikilizaji watachanganyikiwa.
Ufalme wa Kisiasa ninaouzungumzia mimi, ni ule wa kumkomboa Muislamu Mtanzania kutokana na bughudha mbalimbali tunazokumbana nazo zinazofanywa na serikali yetu wenyewe, tena kwa makusudi, jeuri, kejeli na dharau ambazo kwa jumla Waislamu tumekuwa tukizilalamikia miaka nenda, miaka rudi, tangu tupate uhuru wetu wenyewe.
Ufalme wa kisiasa ni ule utakaotuwezesha kushika hatamu za serikali yetu hii, tukaweza kuzuia kero za kuingiliwa Misikitini na askari wetu wenyewe, tukaweza kuzuia Misikiti yetu isinajisiwe na viatu vya askari hao au mijibwa yao, tukaweza kuzuia tusipigwe risasi na kuuawa bila ya sababu nzito, tukaweza kuzuia mitihani isifanyike wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan au wakati wa sherehe za Idd, tukaweza kuzuia nyama za nguruwe zisichomwe mbele ya Misikiti au kuuziwa watu hovyo na yote mengine ambayo sote tunayajua.
Ufalme wa kisiasa ndio utakaotuondolea fedheha ya kunyanyasika, kudharaulika na kupuuzwa. Ufalme wa kisiasa ndio utakao tuwezesha kuacha kuiomba serikali yetu yenyewe itupe haki sawa na raia wenzetu wengine. Hili ndilo somo ninalolizungumzia mimi. Amini, msiamini, ndugu zangu Waislamu, hakuna njia nyingine yoyote ya kuupata ufalme wa kisiasa nchini mwetu ila kwa kura ya pamoja na kuwa hakuna wakati mwingine mzuri kuliko katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2000. "Ngoja ngoja yaumiza matumbo". Tutangoja mpaka lini? Tumengoja miaka mingapi mpaka sasa?
Waislamu tumeagizwa kuifuata Qur’an na Sunnah. Hiyo ndio miangaza tuliyoachiwa na mpendwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) kwa fadhila zake Subhanahu Wataala. Miangaza hiyo ndio itakayotuwezesha, endapo tutaizingatia, kuupata ufalme wa Allah, anaouzungumzia ndugu yangu Mwapwani Mohamed na pia ufalme wa kisiasa, ninaouzungumzia mimi.
Sasa hebu tuangalie, kwa muhtasari tu nini alichokifanya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) alipokuwa katika hali ya unyonge kisiasa. Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) alipoanza kuitangaza Qur’an na Uislamu pale Makka alipambana na upinzani na dhahma kubwa sana, kama sote tujuavyo. Makafiri wa Makka na Arabuni kote wakati huo ndio waliokuwa wameshikilia ufalme wa kisiasa wa kibabe wa enzi hizo.
Tunajua kuwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) pamoja na wafuasi wake walinyanyaswa, walidharauliwa na kupuuzwa kiasi gani na kuwa waliteswa na kuuawa bila ya sababu yoyote. Iliwabidi wakati wa swala wajifiche na hata mua’zin anong’one. Ibada ikafanyika kwa hofu na si kwa utulivu unaohitajika, ili muradi ilimbidi Mtume (s.a.w.) awaamrishe baadhi ya wafuasi wake wakimbilie Abyssinia kuepukana na mateso na hatimaye yeye mwenyewe Mtume (s.a.w.) akaamrishwa na Mola wake (s.w.) kukimbilia Madina ambako Waislamu walikuwa tayari wana hatamu za ufalme wa kisiasa.
Katika kipindi chote hicho, ibada ilikuwa haiwezi kufanyika katika Kaaba. Humo mlikuwa mmerundikwa masanamu na kufuru kemkem zikiendeshwa ndani yake. Hayakwisha hayo mpaka Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) alipoupata ufalme wa kisiasa wa Makka kwa kuiteka.
Shida aliyoipta Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) na wafuasi wake wakati huo, ingawa hailingani na shida yetu Waislamu wa Tanzania, lakini zinafanana fanana. Na ndani yake kuna mafunzo kwetu. Haja yetu katika kipindi hiki ni kuupata ufalme wa kisiasa katika uwiano ulio sawa na idadi yetu ili tuweze kupata haki sawa na raia wengine wenzetu, ili tusidharauliwe, ili tusinyanyaswe, ili tusipuuzwe, ili tusiwe omba omba. "Silaha yetu ni kura ya pamoja".
Kwa mfano, tukitaka Waislamu waende kuswali Ijumaa, tunakaa katika serikali yetu na wenzetu tunaamua kuwa ofisi zote na shule zote siku za Ijumaa zitafungwa kuanzia saa sita adhuhuri mpaka saa nane mchana, ili kuwawezesha Waislamu kwenda kuswali Ijumaa. Sio tunakwenda kuiomba serikali itufikirie kutupa ruhusa hiyo. Hili zoezi la kuiomba serikali ndilo nisilolitaka. Kwa nini sisi tuiombe serikali? Hii serikali ni ya nani? Kama ni yetu kwa nini haitufanyii bila kuombwa? Kwa nini hatuiambii tu ikafanya? Na kama haifanyi tunavyoiambia kwa nini tusiing’oe kwa njia ya pamoja?
Nawahimiza tena ndugu zangu Waislamu, pamoja na ndugu yangu Mwapwani Mohamed kwa mara nyingine, tuutafute kwanza ufalme wa kisiasa kwa silaha ya kura ya pamoja na kama hatukufanya hivyo, matumaini yetu na jitihada zetu za kuutafuta ufalme wa Allah yatakuwa mashakani. Tutaundiwa MABAKWATA, tutaingiliwa Misikitini, tutalishwa miguruwe na nyamafu, tutapangiwa sheria za ndoa na mirathi kinyume cha maadili ya imani yetu, tutanyimwa ruhusa za kuswali, na sisi kazi yetu ni kulalamika huku hatusikilizwi tunapuuzwa na kuomba omba kwenye mabaraza ya Idd na huku hatupewi chochote zaidi ya kupigwa masindano ya ganzi.
Ndugu zangu Waislamu wa Tanzania popote pale tulipo, huu ndio wakati wa kuamka. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.) kuwa mwaka huuwa 1999, umetukuta katika mwezi mtukufu wa mfungo wa Ramadhani. Ni matarajio yetu kuwa funga zetu zimekubaliwa, kuwa swala zetu zimetakabaliwa, kuwa nia zetu zimetakasika na kuwa dua zetu zimesikika, insha Allah! Hakuna apasaye kuabudiwa na kuogopwa zaidi ya Allah na hakuna atoaye riziki na vyeo zaidi Yake (s.w.). Mwenye Enzi Mungu (s.w.) atuondolee uwoga na atuepushe na kutetemeka tetemekea vyeo vyetu na binadamu wenzetu, AMIN!
Mwaka huu wa 1999 miladia ni mwaka wetu wa kujiandaa kikamilifu tayari kwa pambano la uchaguzi mkuu wa 2000. Huu ni wakati wa kujizatiti tayari kushika hatamu za ufalme wa kisiasa. Tunahitajika kuuimarisha umoja wetu. Baraza Kuu na Taasisi zote za ufalme, Baraza la Misikiti, Baraza la Maimamu na vyombo vingine vyote vya Kiislamu nchini vishiriki katika kufanikisha zoezi hili.
Waislamu wanatakiwa waelimishwe juu ya faida ya kura ya pamoja. Umuhimu wa kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi wakati wa upigaji wa kura hizo na pia jinsi ya kupiga kura kwenyewe ili kura zao zisiharibike. Kama kuna chama kitakachoamuliwa kuungwa mkono basi itakuwa muhimu kijulikane na kutambulika mapema iwezekanavyo au sivyo watu wafahamishwe mapema na kujulishwa kuwa wasichague chama ila watu watakaokubalika bila kujali vyama vyao.
Tumekuwa tukiilalamikia serikali hii tuliyoikabidhi kwanza kwa TANU na hivi sasa kwa CCM kwa muda wa miaka 38 hivi sasa, lakini matokeo yake bado hayaridhishi hata chembe. Katika muda wote huo zimefanyika chaguzi zisizopungua 7 ambazo zote hizo hazikutuletea maendeleo wala faraja. Maana pangekuwapo faraja manung’uniko yetu yangemalizika au yangepungua, lakini badala yake ndio kwanza yameongezeka.
Hali hii tuliyonayo inaonyesha kuwa tumefanya makosa mara saba. Mara zote hizo tumepewa chungu za ahadi nzuri nzuri kila uchaguzi ukaribiapo. Ndimi za watoaji ahadi hizo huwa laini tena tamu sana lakini mara tu baada ya uchaguzi wale vinyonga wanageuka nyoka. Na sisi mpaka leo bado hatujasoma tu, sijui tutasoma mwaka gani. Maana hivi sasa baada ya hotuba za Idd, watu wamekwishaanza "tumeahidiwa vinono, bila shaka safari hii tutafaidi". Ama kweli mkaidi hafaidi ila siku ya Idd. Wanaotoa ahadi ni wale wale ingawa sura zao zimebadilika.
Hivi kweli Rais Mkapa siku zote hizi, tangu awe kada wa TANU na CCM mpaka awe Rais wa nchi na kukalia kiti cha Urais kwa miaka isiyopungua mitatu hivi sasa, alikuwa hajui shida za Waislamu nchini mwake ni zipi mpaka aambiwe katika Baraza la Idd mwaka huu. Kweli jamani kuna mtu atakayenitaka mimi niamini hivyo? Siyo yeye wakati wa kampeni mwaka 1995 aliyewatafuta wazee wa Kiislamu wamuorodheshee matatizo ya Waislamu ili atakapoingia madarakani ayashughulikie? Chambo hicho mimi sikimezi kamwe. Hivi kweli kuwa kadhia ya Mwembechai Rais Mkapa alikuwa haijui mpaka alipoambiwa katika Baraza la Idd? Hapo ndio zitolewe ahadi nasi twapiga vigele gele na vifijo. Mbona alitunyamazia mwaka mzima kuhusu hilo? Mimi ahadi za Rais Mkapa sina imani nazo na kura yangu asiitegemee hata kwa dawa. Ahadi zake si ahadi kitu hizo, hizo ni shindano za ganzi zinazotolewa kila uchaguzi mkuu unapowadia.
Waislamu wa Tanzania kaeni chonjo, saa ya ukweli imefikia na kazi ya kufanya kila mmoja wetu anaijua, tukijivunga tu, tutakumbana na miaka mingine mitano ya vilio na maombolezo. Mwenye kilanga haliliwi!
Katika muda huu mchache tulionao, kati ya hivi sasa na kufanyika kwa uchaguzi mkuu, kuna ulazima wa kuhamasisha umati wa Muhammad (s.a.w.) nchini kote Tanzania. Mfano nzuri wa kuigwa ni kama ule ulianzishwa na akina mama zetu, wa kongamano zilizokwisha endeshwa nchini pote. Tungependa kuziona kongamano za akina baba, za vijana na pia za wazee. Kongamano hizo zisiishie mijini peke yake, maeneo ya vijijini nayo yanahitajika kutiliwa mkazo.
Maimamu wa Misikiti yote wasibaki nyuma katika kueneza mikakati ya neno la utafutwaji wa ufalme wa kisiasa katika hotuba zao baada ya swala za Ijumaa na zile za Isha. Waumini nao wawape nguvu wahutubu kwa kusikiliza kwa utulivu na kuzipa umuhimu hutuba hizo katika kuzizingatia na kuzitekeleza. Kuanzia sasa hutuba zote za Ijumaa Misikiti yote nchini ziwe za kisiasa. Zenye kulenga kuuchukua ufalme. Tusikubali kudanganywa au kutishwa kwa kuambiwa kuwa tunachanganya dini na siasa. Lazima tujiulize ni dini gani hiyo ikatazwayo kuchanganywa na siasa? Katika Qur’an kuna siasa tele na fani mbalimbali zingine. Isitoshe ni wapi Mtume wetu (s.a.w.) pamoja na masahaba zake walikuwa wakipangia mikakati yao dhidi ya makafiri, na pia juu ya maendeleo ya maslahi yao kama sio Misikitini?
Silaha ya kura ya pamoja, imefanikiwa sana
kule visiwani pemba, katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka wa 1995. Ufanisi
wake hauna mashaka. Lililobaki kwetu ni kuiga tu.
|
|