MAKALA ya ndugu Rajab Rajab "Hitima yasambaratisha Uislamu Magogoni" yaliyochapishwa katika ANNUUR Nam. 189, toleo la Februari 19 - 25 yanasikitisha sana, kwa nini ikhtilafu zetu ziwe ndiyo sababu ya kutusambaratisha sisi na dini yetu?
Uislamu ni dini iliyojengea katika misingi ya umoja. Ndiyo maana tukaona hata ibada zake zimelenga zaidi katika kuleta umoja baina ya Waislamu. Kwa mfano, mtu anaweza kusali sala ya faradhi peke yake; lakini sala ya jamaa Msikitini ina daraja 27 juu ya sala ya mtu peke yake. Kuna saumu nyingi za sunna, lakini saumu yenye fadhila kubwa ni ile ya faradhi ya funga ya Ramadhani, ambayo Waislamu wote duniani huifanya pamoja. Tukija katika ibada ya Hijja tutaona kuwa kuna Umra, ambayo ni Hijja ndogo mtu anaweza kuitekeleza peke yake, wakati wo wote; lakini Hijja yenyewe ambayo ndiyo yenye malipo makubwa mbele ya Allah (s.w.) lazima itekelezwe na watu wote, kwa pamoja na kwamuda maalum. Tutaona lengo kubwa la ibada kufanywa hivyo ni kwa ajili ya kuwafanya Waislamu wawe na umoja.
Qur’an na Sunna zimesisitiza sana juu ya umoja na kutahadharisha juu ya utengano. Wahenga walisema: "Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu". Lakini inaonekana sisi Waislamu hatuna habari na hayo kabisa. Tuko tayari tutengane na tuwe dhaifu kwa ajili tu ya kuendekeza ikhtilafu zetu.
Ndugu Rajab, katika makala yake niliyotangulia kuyataja ameeleza jinsi Waislamu wa Magogoni, Morogoro walivyouhama Msikiti wa hapo kwa ajili ya kukatazwa na viongozi wa Msikiti huo wasisome Maulidi na hitima. Na Imam wa hapo akaridhika bora asali peke yake kuliko akasali na watu wanaopendelea hitima na maulidi.
Uongozi wa dini wataka hekima na elimu, hautaki jazba. Ni dhahiri kuwa watu wa kijiji hicho hawajui hata umuhimu wa sala, kwa sababu waliufunga Misikiti wao na kuugeuza kuwa ni ghala ya kuhifadhia pamba. Badala ya hao walimu waliokwenda katika kijiji hicho kuwafunza juu ya umuhimu wa sala na haja ya kusali sala zao jamaa pamoja na kuuimarisha Msikiti wao, Maustadhi hao, wao wameamua kuwakataza wasisome hitima na maulidi. Matokeo yake wameukimbia Msikiti. Iko wapi hekima na busara hapo? Lipi lililo baya zaidi kusoma hitima na maulidi au kuacha kusali?
Maswala ya hitima na maulidi ni mambo yenye ikhtilafu baina ya wanazuoni wetu. Baadhi ya wanazuoni wanasema haifai kusoma hitima na maulidi, lakini pia wapo wanazuoni wanaotetea mambo hayo. Wao wanaona yanafaa. Na wote wanatoa hoja na dalili nzito nzito kutoka katika Qur’an na Sunna ya Mtume (s.a.w.).
Mtume (s.a.w.) amesema mwanachuoni anapofanya ijtihadi juu ya kulitolea hukumu au fatwa jambo akisibu basi atapata malipo mara mbili na akikosea atapata malipo mara moja. Linalofaa kuzingatiwa hapo ni kuwa wanachuoni hata akikosea bado atapata malipo kwa ile ijtihadi yake. Hii ina maana kwamba Waislamu wanaweza kuhitalifiana katika rai, lakini bado wakawa ni wenye kuhesabiwa haki mbele ya Allah (s.w.). la muhimu ni kuwa rai iwe ina dalili zinazokubalika na sharia na pia mwenye kuitoa rai kama hiyo awe ana elimu inayomruhusu kufanya hivyo asiwe mbumbumbu.
Waislamu wanaweza kuhitalifiana kwa rai na wala wasitengane Ahli Sunna wala Wal Jamaa imekusanya madhehebu mane makuu, Hanafi, Hambali, Maliki na Shafii na wote wanahitalifiana katika rai lakini wameshikamana pamoja. Wote wanaitwa Sunni, kwa sababu wanakubaliana na sunna ya Mtume (s.a.w.). Na moja katika sunna za Mtume (s.a.w.) ni kukubali raia za pande zote mbili, japokuwa ni zenye kupingana, madamu zitakuwa na dalili ya sharia.
Ikhtilafu si jambo jipya katika dini. Waislamu walihitilafiana kwa rai hata wakati wa Mtume (s.a.w), wanaendelea kuhitilafiana hivi sasa, na wataendelea kuhitalifiana. Lakini juu ya ikhtilafu hizo hawatakiwi wafarikiane. Ikhtilafu ya kwanza katika Uislamu ni ile iliyotokea baina ya masahaba na Mtume (s.a.w.) mwenyewe bado yu hai. Mtume (s.a.w.) aliwaagiza masahaba wake waende kupambana na Bani Quraidha, Mayahudi waliokuwa wakiwasumbua Waislamu na waliokuwa wakiishi katika viunga vya Madina.
Aliwaambia, "Asisali mmoja wenu Alasiri isipokuwa kwa Bani Quraidha". Masahaba wakafunga safari kwenda huko. Alasiri ikawaingilia na wao wako njiani. Wakahitalifiana juu ya kusali sala hiyo. Wengine walidai kuwa madamu wakati wa sala ya Alasiri umeingia, kulikuwa hapana sababu yo yote ya kuichelewesha, basi wakasali. Hapana shaka hawa walifuata kauli ya Allah (s.w) isemayo, "kwa hakika sala kwa Waislamu ni faradhi iliyowekewa wakati mahususi" (An Nisa 4:103. Na waliobaki wakakataa kusali njiani. Walidai Mtume (s.a.w) aliwaagiza wasisali mpaka wafike kwa Bani Quraidha. Kwa hivyo, wakaenda kusali huko huko kwa Bani Quraidha. Bila shaka nao hawakuwa na makosa kwa sababu nao huenda walitegemea kauli ya Allah (s.w.) isemayo, "Mwenye kumtii Mtume amemtii Mwenyezi Mungu". An Nisaa 4:80.
Jambo la kuzingatia ni kuwa habari za ikhitilafu hiyo zilipomfikia Mtume (s.a.w.) hakuwalaumu wale waliosali njiani, wala wale waliokataa kusali na kwenda kusali kwa Bani Quraidha.
Kwa vyovyote vile baina ya makundi hayo mawili lazima liko kundi lililosibu na lipo lililokosea katika kutekeleza agizo hilo la Mtume (s.a.w). Lakini inaonekana Mtume (s.a.w) hakutaka kujua nani alisibu na nani alikosea. Aliona madamu wote nia yao ilikuwa ni kutelekeza agizo lake, lakini kwa bahati mbaya wakatofautiana katika kulifahamu agizo hilo, basi watahukumiwa kwa nia zao na siyo kwa matendo yao.
Moja katika mambo yanayoleta ikhtilafu baina ya Ahli Sunna Wal Jamaa ni kuleta Qunuti katika sala ya Alfajiri. Madhehebu ya Shafii yanaleta Qunuti, lakini madhehebu ya Hanafi hayaleti. Safari moja Imam Mohammad bin Idris As-Shafii (ra) alitembelea Msikiti wa Imam Abu Hanifa. Wanafunzi wa Imam Abu Hanifa wakamkaribisha Imam Shafi awasalishe sala ya Alfajiri. Imam Shafii akakubali kuwasalisha, lakini hakuleta ile Qunuti, kama ilivyo kawaida yake.
Wanafunzi wa Imam Abu Hanifa walipomwuliza kwa nini hakuleta Qunuti na hali yeye ndiye mwenye kusisitiza Qunuti. Imam Shafii aliwajibu kuwa ingawa anatofautiana na Imam Abu Hanifa, lakini alikuwa anaiheshimu rai yake. Wakati huo Imam Abu Hanifa alikuwa amekwisha fariki juu ya hivyo Imam Shafii hakumkhalifu mwanachuoni mwenziwe. Na wale wanafunzi wa Imam Abu Hanifa hawakusema kuwa madamu Imam Shafii analeta Qunuti na mwalimu wao, Imam Abu Hanifa haleti Qunuti, basi wasimpe nafasi ya kuwasalisha. Mbona huyo Imam na hao Maustadh wao huo Msikiti wa Magogoni Morogoro wanakataa kusali na watu wanaosoma maulidi na hitima?
Waislamu yahitaji kuzinduka. Tuziache ikhtilafu zetu ndogo ndogo kuwa ndiyo sababu ya kutugawa na kudhoofisha umoja wetu. Kama kulikuwa na wakati ambao Waislamu walihitaji umoja na mshikamano basi huu ndio wakati wenyewe.
Ili kudai haki zetu inabidi tushikamane na kuwa kitu kimoja, mbona tunakubali mambo kama hitima, maulidi, qunuti, tawassul na kuandama kwa mwezi yawe ndiyo vikwazo kwa ajili ya umoja wetu?
Huu sio wakati wa kufarikiana, bali ni wakati
wa kushikamana. Tusahau tofauti zetu, tujenge umoja baina yetu. Tukiwa
na jukwaa moja la kudaiwa haki zetu tutasikilizwa; lakini kila mmoja akipiga
kelele peke yake, tutapuuzwa. Tumekwisha wasilisha rasmi malalamiko yetu
mbele ya kiongozi mkuu wa nchi yetu naye amekubali kuyapokea. Ni wajibu
wetu kuungana na kuishinikiza serikali ikafuatilia kwa makini malalamiko
yetu na kuyashughulikia ipasavyo. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo tunapoweza
kupata mafanikio.
|
|