Kauli ya Waziri Mkuu, Mh. Frederick Sumaye katika kikao cha Bunge Februari 2, 1999 imetutia simanzi Waislamu na kutufanya tumtilie mashaka. Ni vigumu kuamini kwamba ile ilikuwa ni kauli ya serikali! Serikali isingeweza kutoa kauli ya namna ile baada ya yote ya aliyoyazungumza Mh. Rais Benjamin William Mkapa kwenye Baraza la Idd, pale Diamond Jubilee. Isipokuwa tu, Mh. Sumaye ametumia nafasi yake aliyopewa na serikali Bungeni kuleta kauli binafsi. Walau namna hii mantiki inapatikana.
Serikali inaendeshwa kwa kanuni ya uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility) katika hoja ya upendeleo wa kidini, Mh. Sumaye kama serikali alipaswa kuunga mkono hotuba ya Rais (kiongozi mkuu wa serikali) aliyoitoa kwenye Baraza la Idd katika ukumbi wa Diamond Jubilee. Kusema kwamba udini ni suala "nyeti" kwa hiyo halipaswi kuzungumzwa bungeni, wakati Mh. Rais Mkapa ameshalitambua rasmi, ni kuendekeza "ukereketwa" na kukiuka itifaki. Mh. Sumaye hakujali hata msimamo wa serikali (ukweli na uwazi) katika jitihada ya kuzuia "udini" usiwekwe wazi Bungeni. Labda swali la msingi ni hili: "Udini" unafichwa kwa manufaa ya nani? wanaodhulumu au wanaodhulumiwa? Mnategemea wanaodhulumiwa nao wafiche?
Eti! Suala "nyeti" kwa hiyo halipaswi kuzungumzwa kwa kina Bungeni! Kama matatizo ya wananchi hayazungumzwi kwa uwazi na ukweli bungeni, yakazungumziwe wapi? Waheshimiwa mbona mnatuweka njia panda! Tukipeleka matatizo yetu bungeni, hamyataki! Tukizungumzia katika mihadhara mnasema uchochezi! Sasa tufanyeje?
Tulidhani masuala nyeti yanayoigusa jamii ndiyo yanayopaswa kuzungumzwa na kujadiliwa bungeni. Kumbe yanapokuwa na manufaa kwa Waislamu watayakwamisha kwa kucheza rafu! Udini una unyeti gani? Udini huu na ule wa OIC una tofauti gani? Mbona suala la OIC limejadiliwa kwa mapana na marefu na hatimaye likakwamishwa? Au lilikuwa si la kidini?
Waheshimiwa Wabunge wameshawahi kujadili mambo nyeti na ya siri zaidi kuliko udini. Bado hatujasahau mswaada wa sheria ya kujamiiana ulipokuwa unajadiliwa bungeni. Mambo ya kiutu uzima yalikuwa yakifafanuliwa mpaka wengine tulikosa pa kuweka sura zetu. Lakini tulikaa kimya kwa sababu tulifikiri waheshimiwa Wabunge walikuwa takitafuta dawa ya tatizo la ubakaji katika jamii yetu. Basi ni jambo gani la siri, nyeti na linalostahili umakini wa kuzungumzwa kuliko hili la jimai? Kama Wabunge waliweza kuzungumza hili mbali na unyeti wake kwa lengo la kutatua tatizo, hili la udini linashindikanaje?
Kauli ya Mh. Sumaye kwamba: "Maana ukisema magerezani wako Waislamu kwa wingi, unataka kusema kana kwamba polisi wanapokamata wanakuuliza jina lako nani ukisema Mohamed ndani, ukisema Frederick ah huyo hapana".
Huku ni kupotosha kwa makusudi maudhui ya hoja aliyokusudia Mh. Kitwana Kondo. Mh. Waziri Mkuu ametumia "porojo" kukwepa lengo la hoja ya msingi aliyoitoa Mbunge wa Kigamboni. Bila shaka Mh. Kitwana Kondo alikusudia ni kwa nini Waislamu wanakuwa wengi Magerezani? Hakuwa na maana ya namna polisi wanavyokamata wahalifu. Hoja ya msingi ni kwanini Waislamu wengi wanakuwa wahalifu? Serikali kupitia Mh. Sumaye ilipaswa kujibu swali hili.
Watu wanaponyimwa elimu na kubaguliwa katika nyanja muhimu za kijamii, wanakosa mwelekeo, ajira za maana na hivyo kujiingiza katika vitendo vya kihalifu vinavyowapelekea kuvunja sheria za nchi na hivyo kurundikwa magerezani. Walau Mh. Sumaye angesema hivi tungemuona mkweli na muwazi kama sera kuu ya utendaji ya serikali ya awamu hii inavyomtaka.
Isitoshe Mh. Waziri Mkuu atatueleza vipi kuhusiana na wahubiri wa Kiislamu walionyimwa dhamana na Wakristo walioruhusiwa kwa kosa la aina moja na katika mazingira mamoja? (ANNUUR Na. 138, Februari 5, 1998).
Mh. Sumaye anasema: "Kinachotakiwa, tuseme jamani hapa pana tatizo, sasa namna ya kulitatua, lakini si kwamba kuna watu wanaonewa makusudi. Wanafunzi hawachaguliwi kwa majina ya Ukristo wala Uislamu hata kidogo".
Kwa hakika inatia hofu sana kwa Mh. Waziri Mkuu kutoa majibu ya namna hii kwa hoja iliyotolewa kwa kuzingatia ushahidi wa kitakwimu! Mh. Waziri Mkuu aelewe kwamba tatizo lililo mezani ni udini. Kuna watu wanaonewa makusudi (Waislamu) sasa tutatatuaje tatizo hili bila ya kukiri kwanza kama lipo! Mh. Waziri Mkuu hataki kukiri kwamba Waislamu wanaonewa makusudi na wakati huo huo anatutaka tutatue tatizo! Tatizo linalolalamikwa na Waislamu ni kuonewa kwa makusudi.
Dawa ya Malaria ni chungu, lakini tunainywa kwa lengo la kutibu malaria. Huwezi kumung’unya ‘ Cofta; kwa woga wa ‘Chloraquine’ halafu utegemee kupona malaria!
Mh. Waziri Mkuu ameshasahau kilichomuhamisha Almarhumu Prof. Kighoma Malima kutoka Wizara ya Elimu na Utamaduni. Wizara ambayo haikuwahi kuongozwa na Muislamu kabla ya Prof. Malima. Hana habari kwamba Prof. Malima alishamuandikia dokezo Rais kuhusiana na tatizo hili? Prof. Malima alianzisha mfumo wa haki wa usimamizi na usahihishaji wa mitihani ya shule za msingi. Mfumo ambao ulidhibiti dhulma iliyodumu kwa muda mrefu. Makanisa yakapiga kelele, kwa msaada wa serikali na vyombo vya habari Prof. Malima akaondolewa Wizara ya Elimu. Mh. Waziri Mkuu hana habari na hayo?
Nadhani Mh. Waziri Mkuu ametumia hisia binafsi na maono katika kujibu hoja za Mh. Kitwana Kondo. Na hii siyo njia muafaka ya kuyaendea mambo ya kitaifa. Hoja za Kitwana Kondo ni nzito na bado zinahitaji majibu sahihi.
Inashangaza sana kiongozi Mkuu wa serikali
Bungeni anapotumia neno "nyeti" kama uchochoro wa kukimbia hoja halali
za Wabunge. Kutokana na wadhifa na uzoefu wa Mh. Sumaye asingeweza kutumia
kauli ile kwa bahati mbaya. Anajua anachokifanya. La msingi tu Waislamu
na Watanzania wengine kwa ujumla wajiulize kauli hii ya Waziri Mkuu Bungeni
inatusaidiaje kudumisha umoja na mshikamano wetu wa kitaifa?
|
|