Upo utata wa Yesu kubatizwa
 

WIKI chache zilizopita nilionyesha kupitia gazeti hili utata uliopo juu ya kuthibiti (kuwepo) kwa tukio la Nabii Issa ama Yesu (a.s.) kubatizwa na Nabii Yahya au Yohana (a.s.) katika mto Jordani kama inavyodhaniwa na Wakristo wengi. (Rejea ANNUUR Ramadhani 1419, Januari 8-14, 1999, Uk. 15) Katika toleo hilo nilitoa vigezo kadhaa vya msingi kutoka ndani ya Biblia vinavyochangia kwa kiasi fulani kuleta utata juu ya kuwepo kwa ubatizo wa Yohana ambao ulikuwa ni kwa ajili ya "ungamo la ondoleo la dhambi" (tazama Marko 1:4-5). Ambapo Yesu (a.s.) amekaririwa akithibitisha kutokuwa na dhambi (tazama Yohana 8:45-46). Na kwa hiyo ikadhihirika kuwa ubatizo wa Yohana kamwe haukumhusu Yesu (a.s). Lakini uliwastahili wenye dhambi peke yake.

Aidha, ili kuondoa dhana potofu iliyojengeka kwa Wakristo wengi wanaposhikilia msimamo huo (wa kubatizwa Yesu), katika makala yangu hiyo, nilibainisha kuwa kama wanadamu wengine, Yesu (a.s.) naye hakurithi dhambi ya asili hata uhitajike kwake ubatizo huo wa Yohana. (Tazama Kumbukumbu la Torati 24:16 na Ezekieli 18:20). Na kwa kweli hiki pekee ni kigezo tosha kinachomvua Yesu (a.s.) na dhana ya kubatizwa na Yohana.

Pamoja na kigezo hicho, kwa upande mwingine, nilionyesha jinsi maandiko mengine ya Biblia yanavyodhihirisha kutokuwepo na mawasiliano yoyote kati ya Yohana (a.s.) na Yesu (a.s) ya kubatizana. Ambapo imedhihirika kuwa Yesu (a.s.) akiwa yu mtoto mdogo alikimbizwa Misri na mama yake kwa hofu ya kuangamizwa na mfalme Herode. (Tazama Mathayo 12:13-15)

Nikabainisha kuwa mtoto Yesu (a.s.) baada ya kukimbizwa Misri, hakuweza kurejeshwa Israeli ila baada ya kufariki mfalme Herode na nafasi yake kuchukuliwa na mwanaye, aitwaye Arkelao. (Tazama Mathayo 12:19-22)

Aidha, nilionyesha maandiko ya Biblia yanayomuonyesha mfalme Herode akihusika kikamilifu na kuchinjwa kwa Nabii Yohana (a.s.) (tazama Marko 6:17-29). Na shuhuda hizo tukawa tumejifunza kuwa:

• Kati ya mfalme Herode na Nabii Yohana (a.s.) aliyetangulia kufa ni Nabii Yohana (a.s.).

• Yesu alirejea Israeli baada ya mfalme Herode aliyemwua Nabii Yohana (a.s.) naye kufariki.

• Yesu aliporejea Israeli alikuta mtawala mpya aitwaye Arkelao ndiye aliyerithi kiti cha baba yake Herode. Kwa hali hiyo, Yesu (a.s.) aliporejea kutoka Misri hakumkuta Herode wala Nabii Yohana (a.s.) huko Israeli. Wote wawili alikuta wamekwisha kufa.

•Maandiko ya Biblia yanaonyesha kuwa Yesu (a.s.) alirejea Israeli akiwa bado mtoto mdogo. (Mathayo 2:19-22)

Zaidi ya hivyo, kuhusu yakini ya kuwepo kwa tukio la kubatizwa Yesu (a.s.); nilikiri kuwa maandiko ya Biblia yanapingana wazi hasa unapolinganisha masimulizi ya dhana hiyo (ya kubatizwa Yesu) na shuhuda hizo nilizozitaja hapo juu. Na hata hayo masimulizi yenyewe kama yalivyorejewa na Mathayo 3:13-17, Marko 1:9-11 na Luka 3:12-22, kama tutakavyokuja kuona hapo baadae yanapolinganishwa na kauli za Bwana Yesu (a.s.) mwenyewe yanaleta utata wa kimsingi wa kuthibiti kwa tukio hilo.

Pamoja na uchambuzi huo mfupi, alikuwa ni Bw. Bernard B. Mwenda aliyejitokeza na kujaribu kuikosoa makala yangu ile. Hata hivyo, katika jumla ya hoja na shuhuda zote nilizozitaja katika makala yangu hiyo, Bw. Bernard hakuweza kukanusha hoja yoyote.

Lakini pamoja na kuingiza yasiyohusika na mjadala huu, kitu kikubwa kilichodhihirisha katika makala yake hiyo iliyochapishwa na gazeti hili toleo Na. 188 la Shawwal 1419, Februari 12-18, 1999, ukurasa wa 15 ni kwamba baada ya kunukuu mistari ya Luka 1:13, 26, 31 na 36, Bw. Bernard alidai:

"Hapa bila mashindano tunaona wazi kabisa kuwa Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji walipishana miezi sita tu katika kuzaliwa au katika kutunga mimba. Kutokana na hayo, sasa tunaweza kufahamu kuwa wakati Yohana anabatiza ule ubatizo wa toba tayari Yesu Kristo alikuwa na umri wa mtu mzima na pia alibatizwa na Yohana Mbatizaji. Marko 1:19 Ikawa siku zile Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mathayo 3:13, Mathayo 3:16, Luka 3:21. Maandiko yote haya yanatuthibitishia ya kuwa Yesu Kristo alibatizwa na Yohana Mbatizaji". Mwisho wa kunukuu.

Nimesema kuwa Bw. Bernard ameshindwa kukanusha hoja na shuhuda nilizozitaja hapo awali zinazoonyesha utata wa kuwepo dhana ya kubatizwa Yesu (a.s.). Kushindwa kuzipinga, kunaonyesha wazi kwamba shuhuda hizo zilikuwa sahihi na zimeeleweka.

Pamoja na maelezo hayo ya Bw. Bernard hapo juu, lakini hoja yangu ya msingi haikuhusu umri waliopishana Yesu (a.s.) na Yohana (a.s) katika kuzaliwa au katika kutunga mimba zao. Bw. Bernard ameshindwa kuelezea wazi anamaanisha nini anapoingiza hoja hiyo wakati anajua wazi kuwa hoja yangu ya msingi ilikuwa ni "Je, Yesu alibatizwa? Ni Yohana gani aliyembatiza wakati tunaambiwa kuwa aliporudi Israeli akitokea Misri alimkuta kishachinjwa na Herode? Na nini lilikuwa lengo la kubatizwa naye wakati tumeelezwa kuwa ubatizo wake (Yohana) haukuwahusu watu wasiokuwa na dhambi kama yeye (Yesu)?"

Lakini kabla sijayajadili masimulizi yanayodai kuwa Yesu (a.s.) alibatizwa na Yohana (a.s.) kama yalivyorejewa na Bw. Bernard hapo juu, kwanza ningependa kumpongeza Bw. Bernard kwa juhudi yake ya kutusaidia kugundua jinsi maandiko ya Biblia yanavyogongana. Bw. Bernard kwanza ametaja maandiko yanayoonyesha kupishana kwa Yesu (a.s.) na Yohana (a.s.) kwa umri wa miezi sita.

Japokuwa hakueleza wazi, lakini Bw. Bernard ameamua kuibua maandiko hayo akimaanisha kwamba wakati ule Yesu alipokimbizwa Misri akiwa yu mtoto mdogo, Yohana naye alikuwa bado yu mtoto, hivyo, kazi ya kubatiza alikuwa bado hajaanza kuifanya. Lakini alianza kubatiza akiwa yu mtu mzima na wakati huo Yesu naye alikwisha kuwa mtu mzima.

Hata hivyo, kama nilivyotangulia kusema ni kwamba maelezo hayo yanazidi kutuonyesha mgongano mwingine mkubwa wa maandiko ya Biblia na kwa kweli ni vurugu tupu! Hasa unapolinganisha na shuhuda zile nilizozitaja hapo awali kwamba Yesu alirejea Israeli akitokea Misri akiwa bado yu mtoto mdogo baada ya mfalme Herode aliyemwua Yohana naye kufariki. Ambapo nafasi yake kama maandiko ya Biblia yanavyoonyesha, Yesu (a.s.) alikuta imechukuliwa na mtoto wake (Herode) aitwaye Arkelao.

Sasa, tazama hapa mgongano wa maandiko ya Biblia unavyokuja. Sehemu moja kama alivyotutajia Bw. Bernard, tunaelezwa kuwa kiumri Yohana (a.s.) na Yesu (a.s.) walifikia pamoja kwenye utu uzima. Lakini kwingine tunaambiwa kwamba ni Herode (na siyo mwanae Arkelao) ndiye aliyemwua Yohana (a.s.) ambapo baadae naye alifariki. Ndipo Yesu (a.s.) akiwa bado yu mtoto mdogo ilipopatikana nafasi ya kurejeshwa Israeli akitokea Misri alikokimbilia kwa kuhofia asiangamizwe na mfalme Herode.

Na kwa hiyo, alipofika Israeli hakumkuta Herode wala Yohana. Lakini aliyemkuta ni mfalme Arkelao aliyerithi kiti cha baba yake Herode.

Mbali ya kuwa mgongano huo unaleta utata, lakini pia unazidi kutuonyesha vurugu za maandiko ya Biblia zilivyo ambazo kamwe hutozipata katika Qur’an tukufu. Kwa hali hiyo, hoja hiyo bado haijathibitisha kuwa Yesu (a.s.) alibatizwa.

Baada ya kuibua utata huo wa maandiko ya Biblia, Bw. Bernard aliendelea kudai: "Tuje sehemu nyingine sasa! Kwa nini alibatizwa wakati maandiko yanasema kuwa Yesu Kristo hakuwa na dhambi kwa kuzaliwa na kutenda? Mathayo 3:15 Yesu akajibu akamwambia kubali hivi sasa (kunibatiza) kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki zote. Basi akamkubali. Hapa tunaona kuwa Yesu ni kielelezo. Hangeweza kusema tubatizwe yeye akiwa mwalimu wetu bila kutupa kielelezo". Mwisho wa kunukuu.

Pamoja na madai hayo, lakini jambo ambalo ingepasa Bw. Bernard afahamishwe hapa ni kwamba Bwana Yesu (a.s.) kamwe hawezi kuwa kielelezo (mfano mzuri wa kuigwa) katika jambo ambalo kuwepo kwake kuna utata au halikutendeka kabisa. Na ni wazi kuwa masimulizi ya kubatizwa Yesu (a.s.) aliyoyagusia hapo juu (Bw. Bernard) kama tutakavyokuja kuona hapo baadae ukweli wake bado una utata wa kimsingi.

Kauli za Yesu zapinga masimulizi ya yeye kubatizwa

Kabla sijazitaja hizo kauli za Bwana Yesu (a.s.) zinazopinga masimulizi ya Wainjilisti waliojaribu kusimulia kwamba Yesu (a.s.) alibatizwa, ni vyema kwanza nikayarejea hapa chini neno kwa neno maelezo ya Wainjilisti hao kama yalivyonukuliwa na Biblia:

Tukianza na Mwinjilisti Mathayo, yeye alisimulia hivi:

"Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordarni kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye". (Mathayo 3:13-17)

Marko naye akasimulia hivi:

"Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbinu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake, na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu, nimependezwa nawe". (Marko 1:9-11)

Luka naye akasimulia hivi:

"Ikawa watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa naye anaomba, mbingu zilifunuka, Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua, sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe".

Kwa ujumla, haya ndio masimulizi ya Wainjilisti hao yanayoshikiliwa na Wakristo wengi wakidai kwamba Bwana Yesu (a.s.) alibatizwa!

Hata hivyo, pamoja na masimulizi hayo kutofautiana kimaelezo na hivyo kutojua ni Muinjilisti gani anayeeleza kiusahihi hapo juu, mambo ya msingi yanayopingwa vikali na Bwana Yesu (a.s.) katika masimulizi ya Wainjilisti hao ni haya yafuatayo:

• Sauti inayodaiwa kusikika kutoka mbinguni.

•Dai la kuonekana Roho Mtakatifu kwa mfano wa kiwiliwili kama hua (yaani njiwa).

• Dai linaloonyesha kwamba Yesu (a.s.) alivunja ahadi yake kwa kutengua maelezo ya Nabii!

Kuhusu dai la sauti ya Mungu kusikika, Bwana Yesu (a.s.) aliwahi kuwaambia Wayahudi wote kwamba:

"Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura yake hamkuiona". (Yohana 5:37)

Tunachojifunza kutokana na maelezo haya ya Bwana Yesu (a.s.) ni kuwa katika zama zake hakuna yeyote aliyewahi kuisikia sauti ya Mungu wala hakuna aliyeiona sura yake. Hivyo, kwa kauli hiyo ya Yesu (a.s.) ni dhahiri kuwa sauti ile tuliyosimuliwa na Wainjilisti wale kuwa iliandamana na kubatizwa Yesu (a.s.) ni uzushi mtupu.

Kuhusu dai la Roho Mtakatifu kuonekana,, nalo pia Yesu alilipinga vikali alipowaambia wafuasi wake kama ifuatavyo:

"Mimi nitamwona Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali nyinyi mnamtambua maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu". (Yohana 14:16-17)

Kufuatana na maelezo hayo ya Yesu hapo juu, Wakristo wengi hudai kuwa Roho wa kweli anayetajwa hapokuwa ni Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, wanapokubali hivyo, ni lazima pia wakubaliane na maelezo hayo ya Yesu yanayoonyesha kuwa Roho Mtakatifu haonekani. Na kwa maelezo hayo ya Yesu, ni wazi kuwa dai lile la Wainjilisti wale la kwamba Roho Mtakatifu aliwahi kuonekana dhahiri mithili ya Njiwa, ni uongo na ni la uzushi wa wazi.

Aidha, kutokana na uongo na uzushi huo pekee wa Wainjilisti hao imekuwa vigumu kukubali kirahisi dai hilo lao lile la kubatizwa Yesu hasa unapozirejea hoja na shuhuda nilizoziainisha hapo awali zinazopingana vikali kuwepo kwa tukio hilo.

Ama kauli inayodaiwa na Wainjilisti hao kutolewa na Yohana akimweleza Yesu kwamba "Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu". Kisha Yesu naye eti akamjibu na kumwambia Yohana kuwa "kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavvyo kuitimiza haki yote", inamwonyesha Yesu hapa akipinga wazi maelezo ya Nabii Yohana (a.s.) jambo ambalo katu haliwezi kufanywa na Yesu (a.s.) kwani Yesu anajua wazi kuwa Nabii yoyote hasemi kitu ila ni Wahyi (ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu. (Tazama 2Petro 1:21).

Aidha, kumpinga Nabii kama Yohana (a.s.), Bwana Yesu anajua pia kuwa ni kukiuka ile ahadi yake kwamba "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati wala Manabii...". (Mathayo 5:17-19)

Kwa upande wake, Nabii Yohana (a.s.) naye kamwe hawezi akathubutu kutoa maelekezo ya uongo kama hayo anayodaiwa katika masimulizi hayo kama ilivyodaiwa kwamba ilitakiwa Yesu ndiye ambatize Yohana.

Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa jambo hilo katu haliwezi kufanywa na Bwana Yesu (a.s.) na wala Nabii Yohana kamwe hawezi kusema uongo. Na kwa hali hiyo, masimulizi hayo yanabaki kuwa ni uzushi unaochangia kuleta utata wa kimsingi juu ya kuwepo kwa tukio la kubatizwa Yesu (a.s.).

Pamoja na kuwepo utata huo, Bernard hakuishia hapo, lakini alitilia mkazo suala zima la kukimeza kizima kizima kila kinachoandikwa na Biblia kwa kusema: "... napenda kuwaelimisha wasomaji na Bw. Muhibu Said kuwa Biblia ni maandiko ya Mwenyezi Mungu na kila lililoandikwa katika Biblia hatuna budi kulichukua kama lilivyo na kulitendea kazi". Mwisho wa kunukuu.

Kwa dai lake hilo, yafaa Bw. Bernard akakumbushwa kuwa, kwa mtindo kama huo tuliouona wa Wainjilisti wale kusimulia habari za matukio ya "uongo na uzushi", kamwe haitowezekana kuchukuliwa na kufanyiwa kazi kila linaloandikwa katika Biblia. Hilo ni katika Qur’an tukufu peke yake. Na kama yupo mtu mwenye tabia hiyo ya kumeza kizima kizima kitu kinachoandikwa na Biblia, basi atambue kuwa maandiko hayo ya Biblia yanamshutumu mtu huyo kama ifuatavyo:

"Mjinga huamini kila neno; Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo". (Mithali 14:15)

Kwa maantiki hiyo, yafaa sana tuyachunguze na kuyaangalia sana maandiko ya Biblia kabla ya kuyapokea na kuyafanyia kazi.

Hatimaye, Bw. Bernard hakusita kutusihi Waislamu katika kusoma kwetu Biblia kwa kutuambia, "Pale tunapoona mashaka tuwaulize wale wanaohusika na hicho kitabu wanaoamini nguvu ya Roho Mtakatifu hakika watatusaidia". Mwisho wa kunukuu.

Hii kwa kweli ndio kauli ya Wakristo wengi ya kuwabagua watu wengine na kujipachika wao katika Biblia kwamba ni kitabu kinachowahusu peke yao. Haya ni madai potofu hasa tunapoyalinganisha na kauli zao (Wakristo) wenyewe kwamba "Biblia ni neno la Mungu" na Mungu pia anaposema:

"Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili..." (Yeremia 32:27)

Kwa hiyo, kama inaaminiwa kuwa Biblia ni neno la Mungu, basi Mungu kishasema kuwa "Yeye ni Mungu wa kila chenye mwili". Kwa mantiki hiyo, watu wote Biblia inawahusu. Na siyo Wakristo peke yao.

Aidha, madai hayo yanadhoofisha pia na mabango yanayoandikwa juu ya majalada (Covers) ya Biblia, yakiielezea Biblia yenyewe kuwa ni "Habari Njema kwa watu wote". Haiyumkini kwa tangazo hilo. "Watu" wawe ni Wakristo peke yao! Lakini hata Waislamu nao wanastahili kabisa kuulizwa kuhusu maandiko ya Biblia.

Mwisho, nimefurahishwa na uungwana aliouonyesha Bw. Bernard kwa kuchangia mjadala huu bila jazba, ukereketwa wala kutoa hoja za mashambulizi binafsi kama ilivyozoeleka kwa Wakristo wengi; na ninamshukuru kwa dua zake alizoniombea kwenye makala yake hiyo, nami namuombea kwa Allah (s.w.) amuongoze katika njia ya sawa.

AMIN.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook