KATIBU wa BAKWATA Kata ya Lisekese wilaya ya ya Masasi, mkoani Mtwara, Mwalimu Ally S. Kasinje amemtaka Katibu wa Baraza hilo Wilaya hiyo amfukuze wilayani hapo Amiri wa Taasisi ya Al-Azizu Islamic Centre ya mjini humo, Sheikh Yusuf Shaban Kayungilo kwa madai ya kuleta uchochezi na kuvunja amani na utulivu wilayani hapo.
Katika barua yake yenye Kumb. Na. BAK/WT/99/02 ya Februari 10, 1999 aliyomwandikia Katibu huyo wa wilaya, Mwalimu Kasinje amedai kuwa BAKWATA katika kata yake inafahamu kuwa Sheikh Yusuf ndiye anayechochea chuki baina ya Waislamu katika Misikiti ya Masasi.
Mwl. Kasinje katika barua yake hiyo ambayo nakala yake imesambazwa pia kwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Kamanda wa Polisi wa Wilaya, Afisa Usalama wa Taifa wa Wilaya, Sheikh wa BAKWATA Mkoa wa Mtwara, Maimamu wa Misikiti ya Masasi na kwa Sheikh Yusuf S. Kayungilo mwenyewe, ameendeleza kudai kuwa Sheikh Yusuf pia ndiye aliyehalalisha kuvunjwa kwa Msikiti wa Ahli Sunni Wal Jamaa uliopo maeneo ya kituo cha mabasi hapo Masasi.
Aidha, amedai kuwa Sheikh Yusuf kwa kutumia kikundi chake cha vijana anaowaita wanaharakati, alipinga tamko la BAKWATA lililowataka Waislamu wote kuswali Id siku moja.
Kwa hali hiyo, Mwalimu Kasinje kupitia barua yake hiyo ambayo gazeti hili limebahatika kupata nakala yake, amemwagiza Katibu wa BAKWATA wa Wilaya hiyo kwamba "Tunataka (Sheikh Yusuf Kayungilo) aondolewe hapa Masasi kwa kuhamishwa".
Hata hivyo, barua hiyo haikumtaja ni muda gani ambao Mwl. Kasinje na kamati yake wanataka Sheikh Yusuf awe amekwishaondolewa Masasi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka Masasi, Sheikh Yusuf alisema yeye hana wasiwasi wala hatishiki na njama hizo za BAKWATA zenye lengo la kuvuruga maendeleo na harakati za kituo cha Al-Azizu Islamic Centre.
"Hiyo ndiyo kawaida ya ndugu zetu wa BAKWATA wanaposhindwa kwa dalili juu ya jambo lolote, hukimbilia kuwatisha Waislamu na kuwasingizia mambo, kama kuwaita wenye siasa kali, mawahabi n.k. kwa lengo la kuwafitini serikalini na jamii inayowazunguka ili waonekane kuwa ni watu hatari wanaoweza kuhatarisha amani", alisema Sheikh Yusuf.
Kuhusu suala la yeye kuondoka Masasi, Sheikh Yusuf alisema jambo hilo halipo chini ya mtu au kikundi cha watu fulani.
"Mimi nina haki kikatiba kuishi mahala popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kushurutishwa kuhama na mtu au kikundi cha watu maadhali sijavunja Katiba", alisema.
Aidha, Sheikh Yusuf alisema jambo la kuwaelimisha waumini kuswali swala ya Idd siku moja kabla ya BAKWATA au kuzika bila Tahlili siyo sababu ya kumfanya mtu afukuzwe kwani hiyo pia ni haki ya Kikatiba ya mtu kuamini apendavyo.
"Siyo hilo tu, bali zipo pia njama nyingine ambazo zimepangwa na BAKWATA za kunifukuza Masasi kwa madai kuwa eti mimi siyo raia wa nchi hii na kwamba ni raia wa Burundi. Watu hao wamekuwa wakionekana wakiwasiliana na baadhi ya maaskari wa mjini hapa ili kufanikisha njama zao dhidi yangu", alisema Sheikh Yusuf na kuongeza kuwa yeye ni mzaliwa wa Kurasini, wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
"Wazazi wangu ni wazaliwa wa mkoa wa Kigoma na makazi yao kwa sasa yapo Kaliua wilaya ya Urambo mkoani Tabora", alisema Sheikh ambaye pia alituma kivuli cha cheti chake cha kuzaliwa katika gazeti hili.
Kuhusu tuhuma za kuhusika na kuvunjwa kwa Msikiti huo, Sheikh Yusuf alisema kuwa amri ya kuvunjwa kwa Msikiti huo ilitolewa na mzee mmoja "machachari" kutoka kijiji cha Mumburu nje kidogo ya mji huo maarufu kwa jina la "Daruweshi kuswali Naleke" akishirikiana na wafuasi wa BAKWATA, wakidai kwamba wanazuia Msikiti huo kugeuzwa kuwa Msikiti wa harakati za Kiislamu.
"Pia kipo kitendo kingine cha kusikitisha kilichofanywa na Sheikh wa BAKWATA wa mkoa wa Mtwara cha kuifunga madrasa ya vijana wa Kiislamu iliyokuwa imeshamiri na kutoa changamoto kubwa kielimu katika Msikiti wa Mkuti wa mjini hapa", alisema Sheikh Yusuf.
Sheikh Yusuf amewataka Waislamu wote wake kwa waume wilayani Masasi kupuuza njama hizo za BAKWATA dhidi yake na kuendeleza mshikamano katika harakati za kuleta maendeeo ya Uislamu na Waislamu.
Sheikh Yusuf ni mkuu wa kituo cha Kiislamu cha Al-Azizu Islamic Centre, kituo ambacho kipo chini ya Waislamu na ambacho kimeandikishwa kisheria serikalini chini ya Hati Namba Cap 375 ya Juni 9, 1992. Makao yake makuu kituo hicho kwa sasa yapo mjini Masasi.
Kituo hicho, pamoja na mambo mengine, kinaendesha programu ya kuwafundisha vijana wa Kiislamu Uislamu sahihi kama ulivyofundishwa kikamilifu na Qur’an tukufu na Sunnah za Mtume (s.a.w.).
Endapo Katibu huyo wa BAKWATA wilaya ya Masasi atalipokea na kulifikisha serikalini agizo hilo la akina Mwl. Kasinje na kamati yake na kuchukuliwa hatua, hilo litakuwa ni jaribio la pili dhidi ya Sheikh Yusuf kufukuzwa Masasi kwa madai kama hayo.
Mnamo mwaka 1993, mkuu wa wilaya ya Masasi zama hizo, kwa kushinikizwa na BAKWATA kinyume na sheria za nchi, kupitia barua yake Kumb. Na. CM.8/1/30 ya Julai 13, 1993, alimpa Sheikh Yusuf siku kumi na mbili awe amekwishaondoka katika wilaya hiyo.
Hata hivyo, jaribio hilo lilizimwa siku chache na Mawakili wa Shirika la Sheria Tanzania (The Tanzania Legal Corporation) kupitia barua yao ya Julai 22, 1993, iliyomtaka Mkuu huyo wa Wilaya afute mara moja amri yake hiyo kabla hajafikishwa katika vyombo vya sheria kwa kukiuka katiba ya nchi.
"Mpaka sasa jalada bado lipo wazi katika vyombo vya sheria tayari kukabiliana na wale wote wenye tuhuma dhidi yangu na kituo cha Al-Azizu Islamic Centre zinazolenga kudhalilisha, hivyo, sina wasiwasi wowote na njama hizo. Nadhani hawa ndugu zangu wanajaribu kuamsha mambo yaliyolala", alisema Sheikh Yusuf.
Wakati huo huo, Mama mmoja kutoka Masasi aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Mbise ameliambia gazeti hili kuwa amewashuhudia kwa macho yake watu wanaojiita maaskari wakikaa milangoni nyakati za swala katika Msikiti wa Mkuti, uliopo mjini Masasi wakiwazuia Waislamu wasiingie Msikitini hapo kuswali kwa madai kwamba Waislamu hao hutikisa kidole katika Tashahudi wanaposwali na kwamba wanaonekana wakiswali Idd kabla ya BAKWATA.
Bi. Fatuma amesema kuwa zoezi la kuwafukuza waumini hao katika Msikiti huo linafanywa na wazee ambao alisema mara nyingine wazee hao huacha kuswali na kukaa milangoni wakizuia watu wasiingie kuswali.
"Hatua hiyo imefikiwa kufuatia fat’wa iliyotolewa na Sheikh wa BAKWATA mkoa wa Mtwara, Sheikh Ali Mkumba kwa Waislamu wa Msikiti huo kuwa yeyote watakayemuona akitikisa kidole mtupeni nje au hata mumpige", alisema Bi. Fatuma.
|
|