SHEIKH maarufu ambaye ni miongoni mwa wahadhiri wa mlengano wa dini (comparative religion) hapa nchini Sheikh Kipozeo amesikika hewani akisema kuwa shirki ni pamoja na kubuni au kufuata chama kinachopingana na Uislamu.
Sheikh huyo aliyasema hayo hayo akiwa katika Msikiti wa Boma Road wakati akitoa mawaidha kabla ya sala ya Ijumaa mapema hivi karibuni mjini Morogoro.
Akiwa katika ‘kuichosha’ mada ya shirk, Sheikh Kipozeo amesikika akiwafafanulia Waisalmu waliokusanyika Msikitini hapo kwa ajili ya sala ya Ijumaa kuwa kujiundia chama chochote kinachokwenda kinyume na maamrisho ya Allah (s.w) na kukifuata chama hicho ni kumshirikisha Allah (s.w.).
Akiyatilia mkazo maneno yake alisikika akinukuu aya na Hadith mbalimbali za Mtume (s.a.w.) ambazo zinaonyesha ubaya wa kumshirikisha Allah (s.w.) na viumbe vyake kwa kuvipa sifa zinazomstahiki Muumba.
Aidha, Sheikh Kipozeo aliwataka Waislamu wajihadhari na shirk na kuwasisitizia umuhimu wa kumtambua vyema Allah (s.w.) na sifa zake ambazo si halali kupewa kiumbe iwe kwa maneno au kiutendaji. Alitoa mifano ya wale wanaosema "zidumu fikra sahihi" au "yule mwisho".
Sambamba na hilo, Sheikh Kipozeo amesikitishwa na kuwashangaa baadhi ya Masheikh wenye majoho na vilemba vikubwa ambao kwa kutaka ukubwa wanazipinda ndimi zao na hata kuzipindisha aya kwa kuchelea maslahi ya kulijaza tumbo. "Utamkuta Sheikh mkubwa anakasirika anaposikia kuwa "Yesu si Mungu".
Akizungumzia msimamo wa Uislamu juu ya Nabii Issa (a.s.) (Yesu) alisema kuwa ni mafundisho sahihi ya Uislamu yanayosema kuwa Yesu (a.s.) si Mungu, si mwana wa Mungu na wala hakusulubiwa, na ni haki ya Waislamu kuitangaza imani yao hiyo kama alivyofanya Mtume Muhammad (s.a.w.).
"Mtume (s.a.w.) alipoambiwa "Sema! Yeye Mwenyezi Mungu ni mmoja; ina maana ya kuwatangazia wengine", alisema Sheikh Kipozeo.
|
|