Wakati ‘Kiti moto’ kikipewa ruksa Dar...
Cha ‘kuzimulia’ makali ya Waislamu chang’amuliwa Moro
 

UTITIRI wa vyama visivyo rasmi vijiitavyo "vya kufa na kuzikana’ umezagaa mjini hapa ambapo Waislamu wameutilia shaka kuwa huenda ni miongoni mwa vyombo vya ‘kuzimulia’ makali ya Waislamu dhidi ya wahujumu wa haki zao.

Wakiongea na ANNUUR kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki kufuatia nyama ya nguruwe (kiti moto) kupewa ruksa isiyo mipaka kuuzwa jijini Dar es Salaam, Waislamu wa Morogoro walisema kwamba hatua hiyo ni mlolongo wa dhulma dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini na kutilia wasiwasi kuwa ruksa hiyo inaweza ikawa mfano kwa maeneo mengine nchini kuiga, kwani uzoefu unaonyesha kwamba kila kipitacho Jijini basi ni nadra kutopita Manispaa na mijini huko mikoani.

Walisema kuwa kwa upande wa mkoa wao tayari kuna vyombo wanavyovitilia wasiwasi kwamba lengo lake ni kuwaondoa katika agenda ya kudai haki zao ikiwemo ya kulishwa ‘kiti moto’ kwa lazima.

Walivitaja vyama vya kufa na kuzikana ambavyo ndani yake kuna ‘mchanganyiko usiolika’ kuwa ni mojawapo wa vyombo hivyo.

"Kuanzishwa vyama vya kufa na kuzikana vyenye mchanganyiko mkubwa wa Waislamu na wasio Waislamu, kwa muavuli wa kusaidia mwanachama anapofariki au kufiwa ni miongoni mwa vitu vinavyowavua Waislamu wanachama Uislamu wao na kuzimua makali ya madai yao ya kudhulumiwa haki zao za msingi", amesema Bw. Suleiman Said Mdigo mkazi wa Nanenane mjini hapa.

Ustadh Said Ramadhan wa Misufini Morogoro, nae alihoji mantiki ya Waislamu kujiunga na kile alichokiita "chombo cha hujuma", kwani dini yao pekee ni chama tosha cha kufa na kuzikana.

"Ni Muislamu gani kati ya hao wanachama wa vyombo hivyo vya hujuma au mwingine yoyote aliyewahi kufa, kufiwa au kupatwa na tatizo lolote lile na akaja Msikitini kuwafahamisha Waislamu asisaidiwe? Sasa kuna sababu gani ya kujidhulumu nafsi zetu na kuidhulumu dini yetu juu ya dhulma za makafiri", alihoji Ustadh Said.

Baadhi ya wanachama wa vyama hivyo walipohojiwa na gazeti hili walisema kuwa, zaidi ya "maslahi", vyombo hivyo pia husaidia kujenga (kuunga) undugu wa mnyororo wa chama kati yao na wasio Waislamu.

"Tunasaidiana katika shida na raha, tunazikana na kuoleana, sasa tatizo liko wapi", alisema mtetezi mmoja wa chama cha kufa na kuzikana Kata ya Mafiga Bw. Hashim Adulfallah madai ambayo jirani yake Mama Saida Mkondya aliyapinga vikali na kusisitiza kuwa vyama hivyo ni sawa na kile chama cha "Umoja wa Waislamu na Wakristo Rufiji’, ambacho kilishakufa muda mfupi baada ya kuasisiwa.

"Kiuhakika mwanangu (mwandishi wa habari hizi) vyama vya kufa na kuzikana havina tofauti yoyote na UWAWARU, hapa unatujia kwa mango wa nyuma", alisema mama Saida Mkondya.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook