Unyama tuliotendewa Waislamu
 

1.Bismika jalia
Naomba kwakosatua
Niweze kuhadithia,
Unyama tulotendewa.

2.Si mazuri kusikia,
Yabidi kusimulia
Kuweka historia
Yapata kuhifadhiwa.

3. Wajao waje kujua
Mambo yalivyotokea
Sababu ilochangia
Ndugu zao kuuwawa.

4. Kanisa lilipania
Kwa hofu iloingia
Fitina wakazitia
Serikalini kuzuwa.

5. Uongo wakatumia
Wakatoliki kwa nia
Ya kufitini raia
Waliyotaka yakawa.

6. Wakuu wa Parokia
Njuga wakatuvalia
Kashfa kutuzulia
Eti wanakashifiwa.

7. Wao walitangulia
Kusambaza Bibilia
Kila tulipopitia
Mabuku tuliyapewa.

8. Mabuku tukapokea
Kwa nia kuyasomea
Kutaka kweli kujua
Tusije kuhadaiwa.

9. Luka, Waebrania
Mathayo, Wagalatia
Buku tukalibukua
Vyema tukalielewa.

10.Ngariba kawakomoa
Kiranga akawatoa
Mabuku wakajutia
Kwa nini wameyagawa.

11. Mihadhara ikakua,
Wahadhiri wakapea
Wakasilimu mamia
Misalaba yavuliwa.

12. Yesu tumeshuhudia
Kuwa yeye ni Nabia
Kifo hakukifikia
Wala hakusulubiwa.

13. Uungu kaukataa
Wala Mungu hakuzaa
Yesu ameshajitoa
Kagoma kusujudiwa.

14. Kweli imehudhuria
Uongo umekimbia
Hawana la kutwambia
Majutoni wamekuwa.

15. Wakadai kutetea
Kujibu kwa Bibilia
Hawana wanalojua
Matusi yakatumiwa.

16. Jukwaani akakwea
Hoja za saikolojia
Zilipomminikia
Simbaulanga karowa.

17.Ndimbo naye kachomoa
Kashindwa kulitetea
Kanisa kwa Bibilia
Kabaki anazomewa.

18. Mambo yalipokolea
Myoyo ikawasongoa
Mbinu walizotumia
Dafu hazikulifuwa.

19. Uzushi wakauzua
Kashfa kusingizia
Mihadhara kuzuia
Kwa mabavu na adawa.

20. Serikali kupitia
Kwa mkuu wa mkoa
Vyombo ikavitumia
 Islamu kuvamiwa.

21. Ikawauwa raia
Wasokuwa na hatia
Kwa makusudi na nia
Mihadhara kuzuiwa.

22. Polisi ikanuia
Ikazizusha ghasia
Kupata pa kuanzia
Yale yalokusudiwa.

23. Lengo wakalifikia
La Mwembe Chai kuuwa
Kwa bunduki za milia
Umma ukafyatuliwa.

24. Leo mbiu twaitoa
Waisilamu sikia
Wakati umewadia
Wa dini kupigania.

25. Budi la kujitetea
Limesha tuhalalikia
Kafiri wameamua
Kuuwa kwao ni sawa.

26. Ukatili kwa raia
Dola imefurahia
Vyombo vimeshabikia
Makamba akasifiwa.

27. Bunge limeshangilia
Kanisa limeridhia
Kuvurugwa kwa sheria
Pongezi zimetolewa.

28. Muislamu tambua
Huna wa kukutetea
Kaa makini na nia
Kupinga kuonelewa.

29. Chuki Athumani poa
Allah atakulipia
Kilema walokutia
Kwa Mola kitafidiwa.

30. Ndugu yetu vumilia
Mola yote anajua
Yeye amekuchagua
Shujaa wetu ukawa.

31. Je hivi twadhania
Peponi tutaingia
Bila ya kutufikia
Za walopita Beluwa.

33. Ewe Mola wa dunia
Kwako tunashitakia
Hali zetu wazijua
Wanyonge twadhulumiwa.

34. Imani twahitajia
Imara zilizotulia
Nyoyoni zilizokithiria
Tupambane twaudhiwa.

35. Kufuru imeenea
Watu inawazuia
Imanini kwelekea
Waumini twauwawa.

36. Kwako tunategemea
Mwenye nguvu ya kutoa
Mpaji wa wahitajia
Tuhami tunaonewa.

37. Wito tunawanadia
Islamu Jumuiya
Tusipoipigania
Dini tutaadhiriwa.

38.Unyonge si wakuridhia
Tusiishie kulia
Tuipite kila njia
Upatikane usawa.

39. Mwembe Chai walofia
Na wote waloumia
Leo twawakumbukia
Mashahidi wamekuwa.

40. Na walotumikia
Kwa mateso ya hisia
Afya zikawanyongea
Gerezani kufungiwa.

41. Peponi wataingia
Aya zinashuhudia
Wala hawana udhia
Kwa Mola watapokewa.

42. Hasa hii ndio njia
Mtume alopitia
Na Masahaba jamia
Kuifata twatakiwa.

43. Ndiyo suna ya Nabia
Yapasa kuigizia
Vitendo na nadharia
Ndipo tutafanikiwa.

44. Tuzikatae sheria
Za viranja wasojua
Za kuharibu tabia
Na misingi ya murua.

45. Matwaghut twajua
Daima watuvizia
Chaguzi zikiwadia
Kwa hila tunatumiwa.

46. Tugome kuwa sinia
Chombo cha kupakulia
Cha walaji kutumia
Mlo wao kuwekewa.

47. Nani wa kumteua
Kwa kura kumchagua
Wote tuwe tunajua
Tusije kuhanithiwa.

48. Uislamu ni njia
Ndio chama asilia
Vyama visivyo murua
Si haki kukumbatia.

49. Tamati namalizia
Salam namtakia
Sala na Rehema pia
Nabii Mheshimiwa.

50. Amina Mola pokea
Yote tukubalia
Utuongoze na njia
Tuifate sawa sawa.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook