Polisi kuua Waislamu Mwembechai
 
Waumini Dar waitaka serikali iache vitisho
 

Serikali iache kuwatisha waumini na kusambaza propaganda zisizo na mashiko badala yake waseme ukweli na wachukue hatua dhidi ya wale waliowaua Waislamu pale Mwembechai.

Hayo yamesemwa na Waislamu mbalimbali hasa wa Msikiti wa Tungi kufuatia juhudi za Mkuu wa Wilaya ya Temeke Kapteni John Chiligati kutaka kuzuia kumbukumbu ya mauaji ya Waislamu Mwembechai.

Katika juhudi hizo, Mh. John Chiligati alidai mbele ya uongozi wa Msikiti wa Tungi kwamba nia ya kufanywa shughuli hiyo ni kuibua chuki na kupanda mbegu ya uhasama na kuvuruga amani.

Aidha, alidai kwamba wanaoandaa shughuli hizo wanapewa mamilioni ya mapesa kutoka nje.

"Si bure, bali kuna mapesa yanaletwa kutoka nje, wengine tunacheza mdundiko tu", alidai Bw. Chiligati na kuongeza "watu wanataka wawe mamilionea kupitia Mwembechai na shibe yao iwe kero kwetu sisi".

Akizungumza hayo ofisini kwake mbele ya kiongozi wa Msikiti wa Tungi hivi karibuni , Kapteni John Chiligati alihoji ni mbegu gani inayopandikizwa kwa kuandaa kumbukumbu hizo kama sio chuki.

Hata hivyo, uongozi huo wa Msikiti ulimwambia Bw. Chiligati kwamba wao wanaisaidia serikali kwani ndiyo ambayo ingepaswa iwaonyeshe wananchi mkanda huo ili kuwaeleza ukweli hasa ikizingatiwa kwamba hii ni serikali ya ukweli na uwazi.

"Tunachokifanya sisi ni kuisaidia serikali kuwaonyesha watu ukweli wa mambo yalivyokuwa pale Mwembechai", alisema Ustadh Shaaban Ibrahim Katibu msaizidi wa Kamati ya Msikiti huo.

Kama ni chuki na uhasama wamesema kwamba wanaoujenga ni Luambano aliyeishinikiza serikali hata ikatumia vyombo vya dola vikafikia kuwaua Waislamu.

Aidha, wamesema chuki zaidi na uhasama utajengwa kwa serikali kufumbia macho mauaji haya na kukataa kufanya uchunguzi na kuwafikisha wahusika mahakamani.

Kuhusu suala la mapesa, Waislamu wengi waliotoa maoni yao kufuatia tuhuma hizo za Afande Chiligati wamemtaka akawahoji kwanza wale waliouwa wamelipwa kiasi gani.

Aidha, wamesema awahoji kwanza wale walioishinikiza serikali na wale viongozi walioitikia shinikizo hilo hata wakaua na kuwadhalilisha wanawake wa Kiislamu kinyume na Katiba na sheria za nchi wamelipwa kiasi gani na nani huyo mfadhili wao.

Akiongea na gazeti hili mswaliji mmoja wa Msikiti wa Tungi aliyejitambulisha kwa jina la Hashim alisema kwamba kama ni kupewa mapesa basi wamepewa wale waliokuwa wamepewa tenda ya kupotosha ukweli walioibuka na madai yasiyo eleweka ambayo leo hawathubutu kuyatamka tena.

"Hatukukusanyika kucheza mkinda (ngoma ya Wazaramo na Wandengereko), tunapinga mauaji ya ndugu zetu Waislamu kule Mwembechai", alisisitiza muumini huyo.

Awali uongozi wa Msikiti wa Tungi ulipata habari kwamba unahitajika kituo cha polisi Chang’ombe. Hata hivyo walipofika wakaelekezwa waende kituo kikuu cha Polisi (Central).

Waumini wa Msikiti hawakuwaacha viongozi wao waende peke yao bali kundi la watu takriban thelathini waliwasindikiza. Kabla ya kuonana na wahusika kituo kikuu cha polisi walifanya dua ya pamoja.

Hata hivyo, badala ya kukaribishwa kuonana na wahusika waliambiwa suala lao liko kwa Mkuu wa Wilaya kwa hiyo waende huko.

Wakati huo huo, Hitma kwa ajili ya waliouawa Mwembechai ilifanyika Jumapili iliyopita (Februari 21, 1999).

Katika khitma hiyo iliyofanyika Msikiti wa Tungi Temeke, waumini pamoja na mambo mengine walipata fursa ya kutazama kanda ya mauaji yaliyofanywa na polisi dhidi ya Waislamu Mwembechai mapema mwaka jana.

Aidha, taarifa ya kamati juu ya kadhia nzima ya Mwembechai, mawaidha, utenzi na dua kwa ajili ya waliouawa viliwaacha maelfu ya waumini wake kwa waume waliohudhuria hafla hiyo wakibubujikwa na machozi.

Shughuli hiyo ya aina yake iliandaliwa na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini ambapo ‘Screen’ ziliwekwa kila kona ili kuwawezesha maelfu ya watu kuona kanda hiyo.

 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook