Taarifa toka ndani ya Manispaa ya Moshi zimethibitisha kwamba Bw. Malya ameliuza jengo hilo na tayari alishatia kibindoni shilingi milioni mbili (2,000,000).
Pamoja na hujuma hiyo
aliyofanya dhidi ya mali za Waislamu Kilimanjaro, Bw. Malya amezawadiwa Ukatibu wa Kamati ya muda ya utendaji ya Bakwata Taifa.
Taarifa za awali ambazo zilichapishwa na gazeti hili ziliarifu kwamba jengo hilo limeuzwa na sasa walokole wanalitumia kama sehemu ya kuimbia kwaya zao.
Januari 29, kupitia barua yake Na. BMK/BWZMK/19/13, Bw. Malya aliwaarifu Maimamu wa Misikiti yote ya Mkoa wa Kilimanjaro akisisitiza kwamba "Jengo hilo halijauzwa".
Katika barua hiyo Bw. Malya alidai kwamba habari za ANNUUR zilikuwa za "kupotosha na kufarakanisha Waislamu" na kuongeza kwamba: "Ukweli ni kuwa jengo hilo halijauzwa".
Idara ya Elimu Manispaa Moshi ambao ndio iliyouziwa jengo, Februari 19, 1999 ilitoa barua ikithibitisha kwamba ni kweli wameuziwa jengo hilo kwa gharama ya shilingi milioni sita (6,000,000).
Katika barua hiyo Na. KNM.18/2/009/164 kwa Katibu wa Bakwata Moshi Mjini, Afisa Elimu Manispaa ameeleza kwamba Bw. Malya alipokea hundi ya malipo ya awali ya shilingi milioni mbili Juni 9, 1998 na akazitoa Benki Juni 10, 1998. Namba ya hundi hiyo ni 002358696 iliyoandikwa na kusainiwa Juni 8, 1998.
Kwa mujibu wa makubaliano, Bw. Malya anatarajiwa
kupokea shilingi milioni mbili (2,000,000) za awamu ya pili hivi karibuni.
|
|