MKUU wa Wilaya ya Temeke Kapteni John Chiligati mwishoni mwa wiki iliyopita ameripotiwa akidai kwamba hafla zinazoandaliwa hivi sasa kama kumbukumbu ya mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai zinafanywa kwa msaada wa mapesa kutoka nje.
Aidha, Kapteni huyo amedai kwamba wenye kutoa mapesa hayo wana lengo la kujenga chuki na uhasama miongoni mwa wananchi na kwamba Waislamu wanatumiwa tu kama wacheza mdundiko wasiojua lengo la mlipia waimbaji na wapiga zeze.
Maneno haya ya Bw. D.C. Chiligati yanakuja takriban mwaka mmoja baada ya serikali yenyewe katika ngazi ya taasisi ya Urais kufuta propaganda za awali zilizotolewa katika ngazi ya Baraza la Mawaziri kwamba tukio zima la Mwembechai lilichochewa na balozi kutoka nje ya nchi.
Aidha, kauli hii imekuja muda mfupi tu baada ya kiongozi mkuu wa nchi Mh. Rais Mkapa kuahidi kulishughulikia suala la Mwembechai kutokana na malalamiko ya Waislamu kwamba vyombo vya dola havikutenda haki wala kufuata sheria katika kulishughulikia.
Katika uwanja wa siasa hizi zisizomtanguliza Mungu mbele; suala la propaganda ili kuficha ukweli ni la kawaida sana duniani kote.
Lakini huwa zikiendeshwa kwa ufundi mkubwa kiasi kwamba wananchi wa kawaida ambao ndio wengi huamini kwamba ndio kweli yenyewe.
Umakini na urazini wa watendaji wa serikali waweza kupimwa kutokana na uwezo wao wa kucheza na propaganda.
Mfano akiibuka mtu leo na kusema kwamba mauaji ya Mwembechai yalichochewa na ugomvi baina ya Waislamu wenyewe wakigombea Msikiti, kwanza atakuwa anajidhalilisha mwenyewe kwa kutangaza ujinga wake hadharani. Baya zaidi kama atakuwa Afisa wa serikali atakuwa ameidhalilisha serikali, lakini jingine ni kwamba anawafanya wananchi wakate tamaa kabisa na serikali yao kwamba kwa kuwa na "watu wa aina" yake hakitegemewi kuongoka chochote.
Suala la msingi hapa ni kwamba watu wameuliwa kwa amri ya watendaji wa vyombo vya dola. Lakini kabla ya mauaji aliibuka Paroko akawachagiza viongozi wa serikali wawachukulie hatua watu aliodai wanamtukana Yesu.
Bila ya kufuata taratibu na sheria za nchi, viongozi wa serikali wakachukua hatua hadi kufikia watu kuuliwa. Kama ni kuuliza basi swali la kwanza lingekuwa huyo Paroko anamtumikia nani na nguvu gani iko nyuma yake inayompa kujiamini hadi kuthubutu kuipa serikali kauli za kiamri na shinikizo. Na nini kiliwapa nguvu wale waliotoa amri "piga shaba" kwamba wangeweza kuua na wasiulizwe na serikali bali wapongezwe.
Lakini kubwa zaidi nini kiliipa nguvu serikali ya kutuma askari Msikitini kwamba hata wakiua mradi watanadi harakaharaka kwamba wanapambana na "siasa kali" wanaotumiwa na balozi za nje (za Kiarabu) basi sio OAU, UNO wala shirika lolote la kutetea haki za binadamu litakalowauliza.
Kama ni chuki na fitina iko hapa wala si kwa yule anayesoma khitma kwa ajili ya ndugu yake aliyeuliwa kidhalimu. Fitna na chuki hujengwa na hawa wenye fikra na uwelekeo hasi (negative attitude) dhidi ya Waislamu kwamba wanaweza kuwapa jina baya, wakawaua na isiwe kitu.
Fitna na chuki hupandikizwa na wale wanaofanya kazi kwa shinikizo la Paroko wakakiuka Katiba, sheria na taratibu zote za nchi.
Fitna na chuki hupandikizwa na viongozi wa serikali wanaokataa kuchunguza suala la mauaji ya Mwembechai kwa madai kwamba hakuna fedha au kwa kudai kwamba ukweli unajulikana kwamba Waislamu wenyewe walisababisha.
Wakristo wenyewe wamekuwa wakihudhuria mihadhara na wengi walisilimu.
Na kikao cha mwisho kilichoitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Wakristo wenyewe walieleza kwamba hakuna kashfa katika mihadhara, hivyo iendelee na vyombo vya usalama vitoe ulinzi.
Sasa kama ni mapesa kutoka nje basi watakuwa wamepewa hao Maparoko, Maaskofu na viongozi wa serikali waliolivalia njuga suala hilo bila ya kuombwa au kutumwa na waumini.
Pamoja na yote hayo, tunasema kila mwananchi mwenye uchungu na nchi hii hatakubali kuona maslahi binafsi ya watu wachache yakiangamiza maslahi ya kudumu ya nchi yetu. Ndio maana mapambano dhidi ya ubaguzi, unyanyasaji, upendeleo na uonevu yataendelea mpaka haki na usawa kwa wote upatikane.
Na lililo mbele yetu ni kudai uchunguzi wa kina ufanywe juu ya kadhia nzima ya Mwembechai na walioua wafikishwe mahakamani.
|
|