WAKATI Rais wa Zanzibar Alhaj Dk. Salmin Amour alipohudhuria sherehe za kuapishwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Zanzibar Bw. Augustine Shayo mwaka 1996 alisema kwamba serikali yake italipa Kanisa msaada wowote linalohitaji. Haukupita muda mrefu tangu kutolewa kwa kauli hiyo zilisikika taarifa za kulipuliwa Kanisa moja dogo nje ya Manispaa ya Zanzibar.
Katika kujaribu kauli ya Dk. Salmin Askofu huyo alivilaumu vyombo vya dola hususan polisi kwa kutolishughulikia vyema suala hilo hasa pale polisi waliposema kwamba wameshindwa kupata ushahidi wa kutosha wa kuwawezesha kuwakamata watuhumiwa wa suala hilo na kudai kwamba suala hilo atalifikisha kwa Mheshimiwa Rais.
Kama hilo halikutosha, katika kipindi cha siku zisizozidi tatu kukatangazwa tishio la kulipuliwa kwa Kanisa jingine na mara hii polisi walikamata mlolongo wa watu na kuwaweka ndani kwa masiku kadhaa kwa madai ya kwamba walihusika katika mpango huo wa kulipua Kanisa.
Kufuatia kadhia hizo wananchi kadhaa waliitaka serikali kufanya utafiti wa kina juu ya madai yanayotolewa na Kanisa ili isije ikawa ni mbinu yao tu ya kutaka kujitanua. Wasiwasi huo wa wananchi sasa umedhihirika kuwa ni kweli baada ya Kanisa kuwa na nguvu si tu katika masuala ya kiroho bali hata katika uendeshaji mzima wa mambo hapa Unguja.
Katika kushukuru juhudi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake mkubwa inaotoa kwa Kanisa mwandishi wa gazeti la Kikristo litolewalo kila Jumapili (la Wapetekoste, Kurasini Jijini Dar) kwa lugha ya Kiswahili anaeleza kwamba: "Kwanza ilikuwa ni vigumu hata kutembea na Biblia hadharani, lakini sasa hali si hivyo", na anasema kwamba upo uhuru mkubwa wa kuhubiri Injili na serikali inajitahidi kuulinda.
Mchungaji Obedi Fabian Muani wa Kanisa la Kipentekoste visiwani hapa anasema kwamba Kanisa lake huendesha huendesha vipindi ya mahubiri ya neno la Mungu kwa kupigia TVZ na sauti ya Tanzania Zanzibar bila ya budhudha yoyote na wamepatiwa muda wa kutosha.
Hakuna shaka kwamba shukrani hizo zinazotolewa kwa vyombo vya SMZ ni ushahidi tosha kwamba serikali imeliridhisha Kanisa kutokana na ulinzi unaolipatia. Kanisa halina budi kutoa shukrani hizo kwani kulikuwa na Wakristo wasiozidi asilimia mbili (2%) kwenye visiwa hivi ambao karibu wengi ni wa kutoka nchi za jirani Kanisa limepewa muda wa kutosha wa kutumia Radio na TV, muda ambao hata vipindi vya Kiislamu havipatiwi.
Hivi karibuni kilifunguliwa kituo kijulikanacho kama Stone Town Youth Centre ambacho kinamilikiwa na Kanisa. Kituo hicho kilifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Vijana Bibi Mariam Hamdun naye kuahidi kwamba atahakikisha kituo hicho kinapewa msaada wowote kitakaohitaji toka SMZ.
Wakati kituo hicho kikipatiwa usajili bila mizengwe yoyote, kumekuwa na urasimu mkubwa juu ya kupatiwa usajili jumuiya za Kiislamu ambapo hutakiwa lazima zipate baraka za Wakfu na hata pale zinapopata baraka hizo huishia kunyimwa usajili huo au husajiliwa kwa muda mchache na baadae kufungwa kwa visingizio mbalimbali kama vile vya kujishughulisha na siasa badala ya dini ingawaje mara zote serikali imeshindwa kutoa ushahidi juu ya madai yao hayo.
Mwananchi mmoja aliwahi kuuliza ni wapi vikundi vya Kikristo huenda vikapata baraka ili visajiliwe. Hata hivyo suala hili limeshindwa kupatiwa jawabu muafaka hadi hii leo.
Kikundi cha Stone Town Centre kinafadhiliwa na Serikali ya Finland. Ni Finland hawa hawa ambao walikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kukataa kuendelea kuifadhili Zanzibar mara tu baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 kwa madai ya ukiukwaji wa Demokrasia visiwani hapa. Miongoni mwa miradi iliyokuwa ikifadhiliwa na Finland ni pamoja na mradi wa mazingira na ule wa usambazaji wa maji safi mijini na vijijini.
Tulitegemea kwamba SMZ ingeizuia Finland kudhamini kituo hicho kwa vile ilidai kwamba kuna unvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu hapa, lakini badala yake wamekuwa wakishirikiana nayo katika kulijenga Kanisa.
Kuna taarifa kwamba kiwanja kimoja ambacho kilikuwa kijengwe madrasa huko Machui umekwamishwa kutokana na shinikizo la Kanisa. Machui ni sehemu ambayo mbali na Wakristo kujenga shule na hospitali wamekuwa wakiwekeza miradi yao mingi mikubwa ambayo inatia wasiwasi kuwa inaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za nchi.
Hivi sasa kiwanja cha kufurahishia watoto kilichojengwa na serikali mapema miaka ya sabini kimekuwa ni sehemu ya Makanisa ambapo misa huendeshwa kuanzia Ijumaa hadi Jumapili kwa kila wiki.
Wananchi kadhaa wamelalamika juu ya kugeuzwa
matumizi kwa kiwanja hicho na kuwanyima watoto wao uhuru wa kutumia kwa
malengo yaliyokusudiwa. Hata hivyo kilio hicho cha wananchi kinaonekana
kutoishughulisha serikali wala Kanisa lenyewe.
|
|