Kutoka magazeti ya zamani
 
Hapakuwa na fujo wala mgogoro wakati...
Maelfu katika Tanganyika wapiga kura
 

Mwafrika No. 855 Ijumaa Novemba 2, 1962

MAELFU ya watu wa Tanganyika jana walipiga kura zao kumchagua Rais wa kwanza wa jamhuri ya Tanganyika. Katika vituo vingi kura zilikwenda kwa usalama na bila ya rabsha ye yote.

Karibu ya watu milioni wanatazamiwa kupiga kura zao katika muda wa siku tano.

Ingawa uchaguzi hasa ulianza saa mbili asubuhi lakini polisi ilisema kwamba katika sehemu nyingine wapiga kura walianza kufika katika vituo hivyo saa 11 alfajiri.

Mwandishi wetu wa Dar es Salaam na ambaye alizinguuka mji mzima akichungua unavyoendelea anasema:

"Tangu mapema kabisa maelfu ya wapiga kura yalijazana katika vituo hivyo, na huko Arnoutoglu mistari mirefu ya watu ilizunguka karibu jumba zima.

Baadhi ya wale waliopiga kura zao mapema ni Rais wa TANU, Bw. Julius Nyerere ambaye alipiga kura yake katika kituo cha Magomeni ya Yuno.

Waziri Mkuu, Bw. Rashid Kawawa pamoja na Mawaziri wengi walipiga kura zao katika jumba la Arnautoglu.

Mpinzani wa Bw. Nyerere katika uchaguzi Bw. Zuberi Mtemvu, Rais wa Congress pia naye alipiga kura yake katika jumba la Arnautoglu.

Jambo la kusisimua mjini Dar es Salaam katika kituo cha Arnautoglu hasa, wanawake walijipanga katika misitari minne ya urefu wa nusu maili kila mmoja.

Wakati huu ulikuwa pale Meya wa Dar es Salaam Diwani Muharami Mfaume alipokuwa anafika kujipanga msitari na kupiga yake.

Kama walivyo raia wengine wo wote wa kawaida, Diwani Mfaume alijipanga safu, nyuma yake akiwapo dereva wake. Walichukua muda mrefu mpaka kufika kwenye masanduku ya kupigia kura.

Baadhi ya watu wengine katika kituo cha kupigia kura cha Arnautoglu walikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi, Bwana Oscar Kambona ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha TANU. Akiwa pamoja na mkewe.

Mara baadaye, Bwana Kambona alikwenda Magomeni kumtia mashamsham Rais wa TANU, Dr. Julius Nyerere, ambaye alipiga kura yake huko.

Dr. Nyerere alifika katika kituo cha Magomeni akiwa anafuatana na nduguye Bwana Joseph Nyerere ambaye ni mjumbe wa Parliament ya Tanganyika kwa sehemu ya Musoma.



Maoni: Televishen

Uhuru No. 1817, Jumatano Juni 24, 1970

WAKATI ndugu zetu huko Ugogo wanapokuwa katika hekaheka kuanzisha maisha mapya ya ujamaa vijijini na kuyatelekeza maisha ya zamani yaliyokuwa yakiwaletea dhiki ya njaa mara kwa mara, huku nyuma tunasikia eti kuna baadhi ya watu ambao wanataka serikali ianzishe mambo ya ufahari na anasa ambazo haziwezi kumsaidia lolote Mtanzania kwa wakati huu tulio nao. Jambo hili la Tanzania kuwa na televisheni yake, lilianza mara tu baada ya uhuru.

Wengine walidai eti kwamba kwa kuwa jirani zetu wanazo televisheni, sisi pia lazima tuwe na televisheni. Wengine walidai eti Tanzania ikiwa na televisheni, wananchi watafaidika zaidi kuliko ilivyo hivi sasa. Kwa nini tunapoteza muda kuuliza mambo ya televisheni, ni swali ambalo linastahili kujibiwa na wale wanaouliza hivyo Bungeni ama mitaani. Lakini ukweli wake umekwisha elezwa kiasi cha kutosha.

Alipokuwa akilijibu swali la mbunge wa Kilimanjaro Rombo, Bwana Maskini, ambaye aliuliza Serikali ina mpango gani wa kuanzisha televisheni, Waziri wa Habari na Utalii, Bwana Makame, alitoa jibu ambalo sisi tunaamini litafunga mlango wa ubishi kuhusu kuleta televisheni katika Nchi hii. Bwana Makame alijibu hivi:

"Sifikirii kamwe kuwa na televisheni katika Jamhuri yetu kwa muda wa miaka michache ijayo, kwa sababu, ikiwa wananchi wa Tanzania hivi sasa hawawezi kumudu kununua redio ndogo ya shilingi mia mbili au mia tatu, wataweza vipi kununua televisheni ya shilingi 2,000/-? Tukiileta televisheni ya matajiri watupu na sio ya wananchi, jambo ambalo litakuwa kinyume cha siasa yetu ya Ujamaa." Hilo ndilo jibu la bwana Waziri ambalo tunaliunga mkono.

Mpaka leo hii wananchi wengi hawana redio, mpaka sasa wananchi wengi hawana nguo nzuri za kuvaa sembuse nyumba safi za kuishi. Maelfu kwa Maelfu ya watoto wa Kitanzania wanatembea miguu mitupu bila viatu. Wananchi huko ugogo wanasumbuliwa na njaa mwaka hata mwaka. Wananchi wengi huko vijijini hawana maji safi ya kunywa, majembe wanayolimia ni yale yale yaliyoachwa na mjerumani. Vipi tunaweza kusimama hadharani na kudai eti Serikali ifanye mpango wa kuleta mambo ya ufahari kama vile televisheni ambayo kusema kweli, ingawa ina faida, lakini faida itawafaa watu wachache sana?

Kipato cha Mtanzania kwa mwaka hivi sasa siyo zaidi ya Shilingi 400/-, Mtanzania huyu atapata wapi Shilingi 2,000/- za kununua Televisheni, na atapata wapi fedha nyingine za kuifanyia matengenezo yanayopasa ikiwa itapatwa mushkeli kidogo? Tulikataa nini na tunadai tuletewe nini? Tunakubali kabisa jirani zetu , kwa mfano Kenya, Uganda na Zambia wanazo televisheni, lakini tusisahau kamwe kwamba kila nchi ama taifa lina mazingira yake. Mazingira na umaskini wa Mtanzania anaufahamu Mtanzania mwenyewe.

Kama tulivyosema hapo juu, jibu la Bwana Makame halina budi kuwa la mwisho na kuzingatiwa na kila mmoja. Tanzania haijawa na wananchi wa kuweza kumudu gharama zote za televisheni. Tanzania mpaka sasa ina watu wachache sana ambao wanamudu kununua redio hizi za kawaida za shilingi 200/- ama 300/-, Wananchi katika vijiji vingi nchini hawajui huo muundo wa redio unafananaje, sembuse kusikia mlio wake wa mbali au karibu. Je, kutaka Serikali ilete televisheni tunataka kumkoga nani na kwa nini? Mwsho, tunatumaini Wabunge Waheshimiwa pamoja na wale wenye fedha za kuwawezesha kununua televisheni watang’amua ukweli wa maneno ya bwana Makame. Kama ndugu zetu hawa wanazo fedha za kutosha kununua televisheni, ingefaa fedha hizo, wazitumbukize katika mfuko wa vijiji vya Ujamaa ili wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo waweze kujinunulia majembe au redio za kawaida. Haya madai ya kuwa na televisheni katika Tanzania lazima tuyasahau WAKATI WAKE BADO.


Young Africans yaichakaza Aga Khan

Uhuru, No. 1553 Alhamisi Agosti 14, 1969

MABINGWA wa Ligi ya Taifa Young Africans, wameudhihirisha umma, kwamba wao ni mabingwa halisi, baada ya kuicharaza Agha Khan Club kwa mabao 3-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa juzi kwenye viwanja vya Gymkhana mjini Dar es Salaam. Mpaka hafutaimu Young Africans ilikuwa ikingoza kwa bao 1 - bila.

Mchezo ulikuwa supa. Timu ya mabingwa ya Young Africans ilipoteza nafasi nyingi mno za ushindi ambazo zilikuwa za wazi kutokana na mashuti yao ya juu na pembeni mwa mlango. Isitoshe vile vile golikipa wa Aga Khan alifanya kazi kubwa sana ya kuvinyakuwa vibao vikali vilivyokuwa vikitoka kwa mafowadi wa Young Africans.

Mpira ulipoanza, mnamo dakika ya 3 tu, Chitete wa Young Africans alichomoa kiki kali sana, lakini kipa wa Aga Khan alikinyakuwa kibao hicho bila ya wasiwasi. Sifa nyingi katika mchezo huo zilikwenda kwa golikipa wa Aga Khan maana kukosa yeye magoli yangeliingia bila ya idadi.

Katika dakika ya 20 Aga Khan Club nao walikosa bao la wazi kabisa ambapo golikipa Elias wa Young Africans alikwishajivunga. Bao la kwanza la Young Africans lilifungwa na Juma Bomba kwenye dakika ya 25 baada ya kupatiwa pasi murua na Chitete.

Haukupita muda mrefu Kilambo hafubeki lefti wa Young Africans alijikweta na boli kisha akafyatua bomba kali, lakini nje. Dakika ya 35 Mwinyi wa Young Africans alikosa bao la wazi ambapo kwa vyovyote vile angeweza kufunga bao la pili. Sehemu ya kwanza ilipomalizika Aga Khan Club walikuwa wameshalala kwa bao 1-0.

Katika kipindi cha pili, Young Africans walikuja juu kweli kweli. Muda wote wa sehemu ya pili mpira ulionekana kuchezwa nusu uwanja upande wa goli la Aga Khan Club. Licha ya hivyo timu ya Yanga ilikuwa na mabadiliko kidogo yaani Selemani, Mwinyi na Elias walitoka na nafasi zikashikwa na Gilbert Mahinya, Kitwana na Zuberi.

Boi wa Yanga alifunga bao la pili kwa peneti mnamo dakika ya 70. Mchuano uliendelea hadi ziliposalia kama dakika 3 hivi mpira umalizike Kitwana akafunga bao la tatu na la mwisho.


Muhamed Ali amuoa Muislamu mwenzake

UHURU, No. 941, Jumatano, Agosti 23, 1967

BINGWA wa ngumi za uzito wa juu ulimwenguni, Mohamed Ali au kwa jina lake la zamani Cassius Clay, mwishoni mwa wiki iliyopita alimuoa mchumba wake mwenye umri wa miaka 17, Belinda Boyd katika sherehe iliyoendeshwa Kiislamu.

"Ilikuwa harusi ndogo", Clay alisema baada ya sherehe hiyo iliyoendeshwa na Rev. Morris Tynes muhubiri wa Dini ya Kiislamu.

Harusi hiyo ilifanyika huko kwenye nyumba ya bondia huyo ambae ana umri wa miaka 25 iliyoko upande wa kusini mwa Chicago. Ni rafiki na jamaa kidogo tu waliokuwepo kwenye harusi hiyo. Clay na Bi. Boyd ambaye pia ni Muislamu walichukua leseni ya kuoana siku ya Alhamisi iliyopita tu. Wazazi wa Clay waliruka kutoka Atlanta, Georgia kwa ajili ya harusi hiyo lakini walichelewa. Badala yake walihudhuria karamu iliyofuata baadaye.

Mkewe Clay alikuwa amevaa kanzu nyeupe ndefu inayoburuzika mpaka chini. Wazazi wa msichana huyo Bwana na Bibi Boyd walikuwako kwenye harusi hiyo.

Clay alimwacha mkewe wa zamani mwaka jana akidai kwamba hakufuata mafundisho ya Kiislamu. Alishitaki kwamba miongoni mwa mambo aliyokuwa hakuyafuata alivaa nguo nyepesi na alitumia manukato makali.


Sunderland yailaza Mwadui kwa 3-1
(Na. Shaaban S. Madega)

Timu ya Sunderland Sports Club ya Dar es Salaam, jana ilionyesha kwamba ina nguvu zaidi kuliko Mwadui Football Club ya Shinyanga baada ya kushinda mabao 3-1 katika mchezo mkali uliochezwa kwenye uwanja wa Ilala hapa Dar es Salaam kwa madhumuni ya kutafuta msaada wa fedha za ujenzi wa makao makuu ya TANU ya wilaya ya Dar es Salaam. Wakati timu zilipokwenda mapumziko, matokeo yalikuwa sawa bao moja kwa moja.

Katika mchezo huo Mwadui ambayo ndio timu inayotegemewa kuwa Klabu Bingwa ya mpira katika Tanzania, walicheza kufa na kupona kwa muda wote wa mchezo ili wadhihirishe ushujaa wao, lakini walishindwa na wapinzani wao katika dakika za mwishoni baada ya kufanya makosa wao wenyewe.

Mpira ulianza wakati wakati ambapo Mwadui walioelemewa huku wakiwababaisha maadui zao na huku Sanda walionekana kiutulivu ikiwa ni ishara ya kutaka kutambua ni hekima zipi wanazozitumia maadui zao. Baada ya Yahya wa Mwadui na Changamwe wa Sanda kukosa kufunga mabao ya wazi kabisa mnamo dakika tano tangu mpira kuanza, haikuchukua muda mrefu Mwadui iliona mlango mfungaji akiwa Kamaka.

Baada ya dakika tatu tangu kupatikana kwa bao hilo, Clement (Sharp shooter) wa Sunderland aliwasawazisha bao hilo baada ya washambuliaji wa mbele wa Sanda waliposogea na mpira vizuri kwenye lango la Mwadui.

Mwadui ingeweza kuhesabu bao la pili katika dakika 30 lakini kama Mbanda angelenga shabaha yake barabara alipokuwa amesalia pekee na mlinda mlango Mbaraka ambaye alikuwa ni mchezaji hodari hapo jana kwa kuzuia mipira iliyokuwa ikitazamiwa kuwa ni magoli halisi. Wachezaji wa nyuma wa kila timu walikuwa wanashika nafasi zao vyema na ndio maana hakukuwa na urahisi wa kupata ushindi katika safu hii ya kwanza.

Kipindi cha pili kilianza moto moto na hakuna mchezaji aliyekuwa akizubaa na mpira. Mlinda mlango Mbaraka wa Sanda aliuokoa mpira hatari ambao ulitazamia kuwa bao halisi kutoka kwa Kamaka katika dakika nne mwa safu hii ya pili. Ingawa Clement wa Sanda alikuwa akijaribu kutoa michomo mikali kwenye lango la Mwadui, lakini hakuwa na bahati ya kutikisha wavu.

Bao la pili kwa upande wa Sanda lilipatikana mnamo dakika 75 za mchezo kwa bao safi alilofunga Arthur Mambetta alipolenga mpira kwa Fri-kiki hadi kimiani akimwacha mlinda mlango Isihaka ameduwaa kwa jinsi mpira huo ulivyoingia wavuni. Kabla Mwadui hawajasawazisha makosa hayo, Sanda iliongeza kufunga bao la tatu kwa mpira aliopiga Idd Balozi ambapo mlinzi mmoja wa Mwadui alipojaribu kutaka kuuokoa, la haula, alijistukia anausindikiza moja kwa moja nyavuni bila ya kutegemea.

Leo uwanjani hapo kutakuwa na pambano lingine la kirafiki baina ya Young Africans ya Dar es Salaam na timu ya Dundee United Sports Club ya Dodoma. Na ule mchezo wa mwisho wa kugombea ‘Marin Cup’ uliotazamiwa kuchezwa jana kwenye uwanja wa Taifa kati ya Yanga na Cosmo, umeahirishwa mpaka siku za baadaye.


Kanyang’anywa mke atoke Congress
 

BWANA M. Sh. Marijani, Mwenyekiti wa Congress katika mji wa Dar es Salaam, amenyanyang’anywa mke wake na wakweze kwa sababu hawataki aendelee kuongoza chama cha Congress.

Katika taarifa yake Bw. Marijani amesema kuwa yeye yuko tayari kumkosa mke kuliko kuiacha Congress kwa sababu, alisema ‘siasa ya chama hiki ndio hasa ninayo iamini’.

Hata hivyo, Bwana Marijani anafikiri kwamba TANU ndio iliyokwenda chini juu hata anyang’anywe mkewe.

Anasema, "hivi karibuni tu nimesikia maneno ya kuaminika kutoka kwa marafiki zangu kuwa kunyang’anywa kwangu mke kumetokana na fikira za viongozi wa TANU, eti kufanya hivyo walifikiri nitakuwa tayari kuacha Congress na kumbe sivyo".

Bwana Marijani amesema kuwa yeye bado ni kiongozi wa Congress na ataendelea mpaka ameipatia Tanganyika serikali ya Waafrika wenyeji".

Akitilia mkazo imani yake na chama cha Congress Bwana Marijani anasema kuwa yuko tayari hata kukosana na wazazi wake kuliko kuacha kile anachokiamini".

 
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook