KATIKA moja ya makala zangu zilizopita za chakula na lishe niliikumbusha serikali kutokukwepa wajibu wake wa kulinda afya za Watanzania kwa kuwadhibiti wafanyabiashara wanaotengeneza maji ya chupa na kuyauza bila leseni.
Makala yetu ya wiki hii itaweka wazi zaidi hatari ya maji ya kunywa yasiyokuwa safi wala salama.
Ukosefu wa kiwango cha kutosha cha maji na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama ni chanzo kikubwa cha maradhi katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Magonjwa ya tumbo (kipindupindu, homa ya matumbo , n.k) ni kundi moja kati ya makundi kumi yanayoongoza kwa kusababisha vifo hasa kwa watoto wadogo katika nchi hizo zinazoendelea.
Kwa mujibu wa takwimu za watafiti za mwaka 1984 - 1985, magonjwa ya tumbo yanayosababishwa na maji ya kunywa yasiyokuwa safi wala salama yanachangia vifo kwa asilimia 8.7 - 10 (nane nukta saba mpaka kumi) katika nchi ya Tanzania.
Zaidi ya kusababisha vifo kwa Watanzania, magonjwa ya tumbo yanaleta kero kwa wageni kama vile watalii wanaokuja Tanzania.
Kwa kuzingatia hali hiyo, maji ya chupa yalitarajiwa kuwa mkombozi wa tatizo la wananchi hasa wasafiri ambao hawawezi kuchemsha maji ya kunywa. Lakini hali ni mbaya zaidi hasa pale wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wanavyoweza kupata fursa ya kuzalisha maji ya chupa na kuyauza bila ya leseni.
Wiki iliyopita vyombo vya habari viliripoti makampuni yaliyokamatwa na vyombo vya serikali kwa kufanya biashara (ikiwemo ya maji ya chupa) bila ya kuwa na leseni. Hata hivyo adhabu waliyopewa wafanyabiashara hao ni ndogo kiasi cha kuhuzunisha ukilinganisha na kosa lenyewe.
Vile vile namna vyombo vya habari vilivyowasilisha jambo hilo aghalabu kwa mwananchi wa kawaida kuelewa undani wa kosa lenyewe na anaweza kuona kuwa adhabu hiyo ni sawa.
Tukijaaliwa wiki ijayo tutawaletea uchambuzi
wa kina wa kadhia hiyo na kuonyesha udhaifu uliopo katika sheria za Tanzania
kuhusu watu wanaofanya biashara bila leseni.
|
|