Mko wapi Wajahidi?
Dhulma inashtadi, kwenye uso wa dunia,
Kila siku inazidi, wanyonge twadidimia,
Madhalimu waturudi, zetu haki wakwapua,
Mko wapi wajahidi, viongozi wa dunia?
Mbona hali ni baridi, haki inatokomea,
Inashamiri fisadi, mizizi yajiotea,
Wanyonge wapi turudi, haki tupate kupewa,
Mko wapi wajahidi, viongozi wa dunia?
Enyi mlo maridadi, kanzu mnoziwatia,
Hizi aya za jihadi, kweli mwazizingatia,
Mbona hafifu juhudi, matendoni kuzitia,
Mko wapi wayahudi, dhulma msoridhia?
Natamka makusudi, jihadi kukumbushia,
Watokee mashahidi, haki wanopigania,
Haki ipate kurudi, dhulma wakaing’oa,
Mko wapi wajahidi, wanyonge tunaonewa?
Wajaao Masjidi, nashindwa kuwaelewa,
Mara tano wa-ahidi, Siraatwa wajiombea,
Sasa mbona mwaritadi, dhuluma mwanyamazia,
Mko wapi wajahidi, haki mnopigania?
Sala bila ya jihadi, peponi hutaingia,
Ametangaza Wadudi, kwa jihadi taingia,
Kwa maovu kuyarudi, haki kuipigania,
Mko wapi wajahidi, viongozi wa dunia.
Giza sasa linazidi, nchini nawaambia,
Mambo yaso maridadi, debe yazidi pigiwa,
Kwa fahari ufisadi, njia watengenezewa,
Mko wapi wajahidi, jamii kuiokoa?
Mbele, sitaki kuzidi, jihadi nawausia,
Mbele, giza lashitadi, lapaswa kuondolewa,
Mbele, nyuma tusirudi, dhuluma taing’oa,
Mko wapi wajahidi, viongozi wa dunia?
Idd S. Kikong’ona,
Morogoro.
Mno nimetafakari, dunia ina mazito,
Ina chuki na sururi, haitaki majikito,
Imeumbwa kwa kadari, ina baridi na joto,
Swahiba natoa wito, acha wako ujasiri.
Dunia ni ya duwari, yazunguka kwa mvuto,
Tena ni kubwa sayari, ina yake mitikito,
Ina mito na bahari, na samaki kama sato,
Swahiba natoa wito, acha wako ujasiri.
Dunia ina mapori, majoka na viroboto,
Ina wanyama khatari, mijusi na sorokoto,
Ina vibweha na ngiri, madovu yaso na kwato,
Swahiba natoa wito, acha wako ujasiri.
Siifanyie jeuri, dunia ina mapito,
Ina wengi wahubiri, Walokole na Sabato,
Kama hujui vizuri, utajiwashia moto,
Swahiba natoa wito, acha wako ujasiri.
Dunia ina zumari, na miziki motomoto,
Ina wacheza kamari, kirumbizi na zoroto,
Ina watu majeuri, wewe wafanya utoto,
Swahiba natoa wito, acha wako ujasiri.
Acha wako ujasiri, wa kunikata mikato,
Napenda kukushauri, mimi sitaki zegeto,
Kama wewe ni hodari, patia chako kipato,
Swahiba natoa wito, acha wako ujasiri.
Acha wako ujasiri, takumbwa na diringito,
Waja anguka kikiri, ukose na furukuto,
Enenda kwa tahadhari, kulia au kushoto,
Swahiba natoa wito, acha wako ujasiri.
Khamis Juma Sibura,
Box 164, Majengo,
Shinyanga.
Kwa jina la Rahmani, Allah mwingi wa Rehema,
Ametuletea dini, isiyokwenda mrama,
Imo ndani ya Qur’an, aliyotaka Karima,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
Mungu hawezi gawanywa, kwa mafungu kama nyama,
Nafsi zikatawanywa, ‘tatu’ nani amesema,
Vitabu vimekusanywa, ni wapi ninyi mwasoma,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
Nawaita kina Dettu, gazetini fanya hima,
Na wengine ndugu zetu, wanaojua kusoma,
Hasa wewe Bwana Dettu, sema wapi umesoma,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
Amewatuma Mitume, kufunza Uislamu,
Nuhu, Musa niwaseme, Isa na Ibrahimu,
Dini moja wasimame, wao na zao kaumu,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
Mwisho kaja Muhammad, katumwa kwa wote umma,
Warabu na Wayahudi, Afrika hadi Bama,
Ametumwa Muhammad, kwa ulimwengu mzima,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
Kumbukumbu la Torati, tano saba nenda soma,
Baada ya Taurati, Zaburi nayo yasema,
Tangia zile nyakati, Mungu mmoja inasema,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
Kwetu ‘Yehova’ ni Allah, hiyo wazi ninasema,
Mola wetu ndiye Allah, Mitume alowatuma,
Mfanowe hana Allah, hana baba wala mama,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
Iweje Mungu mmoja, dini zaidi ya mia?
Kama serikali moja, ‘Rais’ hawawi mia!
Dunia yetu ni moja, Allah ni mmoja pia,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
Pekua sura ya tatu, aya ya kumi na tisa,
Ndani ya Qur’an yetu, imetajwa dini ‘hasa’,
Hakina tone la shaka, ujumbe umetimia.
Kalamu naweka chini, hapa ninamalizia,
Mugu mmoja amini, ili usije jutia,
Vitabu vipekueni, ukweli kujionea,
Mungu mmoja dini moja, nayo ni Uislamu.
B.A. Meena,
P.O. Box 190299,
Dar es Salaam.
|
|