Katika kuiamrisha ibada hii Mwenyezi Mungu anatueleza: Na (Kumbukeni) tulipoifanya nyumba ya (Al-Ka’ba) iwe mahali pa kuendewa na watu, na mahala pa amani. Na mahali alipokuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia. (2:125).
Aidha, Mwenyezi Mungu anasema ..."Na kuwa Mwenyezi Mungu amewawajibishia watu kufanya Hijja kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwenye nyumba hiyo... (3:97).
Katika kipindi cha Hija takriban kuanzia Ramadhani mpaka mwisho wa Dhulhija, limejitokeza vuguvugu na ari kubwa ya kidini duniani kote kutokana na harakati za safari za kwenda na kurejea kutoka Makka.
Vuguvugu hili huchochea hisia za kidini na ari mpya ya kushikamana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Kwa vile hii ni Ibada ambayo kwa wengi ni ya mara moja katika uhai wa mtu ni vyema kabla ya kufunga safari Mahujaji wakaelewa nini wanawenda kulifanya huko na kwa malengo gani.
Isije ikawa mtu akapoteza muda muhimu kwa kutokuelewa nini cha kufanya. Ni kwa kuzingatia hoja hiyo tungependa tuchukue fursa hii kuipongeza taasisi ya ‘Tanzania Hajj Trust’ kwa kuandaa semina kwa ajili ya Mahujaji.
Ni matumaini yetu kwamba katika semina hizi Mahujaji wetu wataelimishwa juu ya mambo yote muhimu ikiwa ni pamoja na taratibu na katiba za ibada.
Tungependa tutoe wito maalum kwa Mahujaji wote wasikose kuhudhuria semina hizo na wawe makini kuyasikiliza na kuyachukua kwa kuyafanyia kazi mafundisho ya semina hizo.
Lakini la mwisho na la muhimu zaidi ni kwa Mahujaji kuelewa kwamba lengo la Hija sio kujipatia anwani ya Alhaj au Hajat fulani. Hija kama zilivyo ibada nyingine ina lengo lake maalum na lisipofikiwa inakuwa zoezi zima limeruka patupu.
Kama kilele cha Ibadat maalum Hija humuandaa mja afikie kilele cha Ucha Mungu ili awe tayari kujitoa muhanga kwa mali na nafsi, kuihuisha, kuisimamisha na kuilinda dini ya Allah.
Ni imani yetu kwamba mahujaji wetu wakifunga safari huku wakizingatia lengo hili Uislamu utasonga mbele.
|
|