Na Rajab Rajab, Morogoro
MADRASAT Jabal-Rahma ni moja kati ya madrasa kongwe mjini hapa ambayo ipo eneo la Sultani, ilianzishwa mwaka 1972, mwalimu muasisi akiwa marehemu Sheikh Juma Hassan Sekidunda ambaye ilianza na wanafunzi wasiopungua 80 chini ya usaidizi wa mwanafunzi wake mkubwa Bwana Fadhil.
Miaka michache baadaye muasisi huyo alifariki ambapo ikabidi madrasa hiyo ishikiriwe na mwalimu Ramadhani Juma ambaye naye baada ya miaka michache alifariki. Ndipo madrasa hiyo iliposhikwa na wanafunzi waliosomea hapo akiwemo Ustadh Miraji Omar ambaye ndiye mwalimu mkuu wa madrasa hiyo kwa sasa.
Jabal-Rahma ni moja ya madrasa inayofanya vizuri mjini hapa katika mashindano mbalimbali ya usomaji Qur’an na Hadith, ina jumla ya wanafunzi 300 kati yao wapo watoto mayatima 25 wanaosomeshwa bure wakati wengine wakichangia shilingi 300 kila mwezi.
Madrasa hiyo inafundisha wanafunzi kwa muda wa miaka saba ambapo wakifika hapo walimu kwa kushirikiana na wazai wanawatafutia nafasi ya kujiendeleza zaidi nje ya mkoa wa Morogoro kujiendeleza zaidi.
Masomo yanayofundishwa katika madrasa hiyo ni pamoja na Qur’an, Lugha, Fiqh, Sira, Tawhiid, Hadith, Nahau, Kiarabu, Kiingereza na Hisabati.
Chini ya mwalimu Miraji Omar ambaye pia ni Imamu wa Msikiti wa Sultan, madrasa hiyo kwa kupitia wanafunzi waliosoma hapo imeweza kuanzisha darasa la kinamama kila siku baada ya sala ya Alasiri pamoja na kinababa baada ya sala ya Magharibi.
Madrasa ya kinamama wa Jabal-Rahma ambayo inaongozwa na Ustadhat Aisha bint Issa akisaidiana na Ustadhat Asma Rukago ina jumla ya wanafunzi 50.
Kwa upande wa madrasa ya kina baba inafundishwa na Ustadh Abdul Waziri Koba ambaye anasaidiana na Ustadh Wamara. Mbali ya walimu hao pia Ustadh Swalehe Funga ni Mwenyekiti na ni Diwani wa Kata ya Sultan. Katibu wa madrasa hiyo ni Ustadh Hamza Issa Mahagetila.
Malengo ya baadaye ya madrasa hiyo ni kuwa na miradi yake ya kiuchumi ili kuwza kujitatulia matatizo madogo madogo pasipo kusubiri misaada kutoka sehemu nyingine ambapo ambapo sasa hivi imekuwa ni bahati nasibu kuipata. Pia madrasa hiyo kama ilivyo madrasa nyingi nchini nayo ina mpango wa kuanzisha shule ya watoto wadogo wa Kiislamu (Muslim Nursery School).
Jabal-Rahma ambayo tangu mwaka 1972 imetoa Masheikh, Maimamu na Wahadhiri mbalimbali nchini inakabiliwa na matatizo lukuki yakiwemo ya ajira isiyo na uhakika kwa walimu pamoja na wazazi kutotilia umuhimu malipo ya kila mwezi ambapo wengi wanachelewesha kulipa na wengine kutolipa kabisa.
Aidha, madrasa hiyo inafundishwa katika mazingira magumu hususan wakati wa mvua ambapo mapaa ya mabati yametoboka na kufanya maji yajae ndani ya madrasa hiyo. Pia madrasa hiyo inakabiliwa na tatizo la vikalio (majamvi) na kufanya wanafunzi wakae chini kwenye vumbi na muda wote kuonekana wachafu na wengine kupata ugonjwa wa mafua kutokana na vumbi.
Suala la ‘tuition’ linachangia kwa kiasi kikubwa mahudhurio mabaya ya wanafunzi wa madrasa hiyo ambapo watoto wengi wanalazimishwa kusoma huko na kuacha madrasa.
"Suala la ‘tuition’ kwa kweli linachangi kurudisha nyuma maendeleo ya vijana wetu na tunajaribu kuwasiliana na wazazi ili masomo hayo yaweze kupatikana hapa chuoni", amesema Mwalimu Mku Ustadh Miraji Omar.
Matatizo mengine yanayoikabili madrasa hiyo ni eneo dogo la kusomea, hata hivyo kwa muda wa miaka mitatu sasa wamepata eneo pembeni mwa madrasa hiyo ili wajenge, lakini mpaka sasa wamefanikiwa kupata roli nne tu za mchanga na uwezo ndio ulipoishia.
"Tunamshukuru Diwani ambaye ndiye Mwenyekiti wa Madrasa hii Bwana Swalehe Funga kwa kupigania mpaka tumepata eneo ambalo lilikuwa linatakiwa na watu wengi, sasa kazi ipo kwenye kujenga ambapo uwezo wetu na Msikiti umekuwa mdogo kutekeleza hilo", amesema Ustadh Miraj Omar katika mahojiano rasmi na gazeti hili.
Aidha, mwalimu huyo ametoa wito kwa wazazi wote nchini kutilia mkazo elimu ya dini kama wanavyofanya katika elimu za shule ya msingi na sekondari.
"Hapa madrasa kila mwanafunzi anatakiwa awe na sare, lakini wazazi wamekuwa wagumu kuwashonea watoto wao isipokuwa wamekuwa wepesi kuwashonea sare za shule", amesema Ustadh Miraji kwa masikitiko ya kuona wazazi wengi wa Kiislamu bado hawajajua umuhimu wa elimu ya dini na kujikuta watoto wanaathirika kimaadili.
|
|