Siku ya kuabudu ni ipi?
Na Elia Batendi
MWENYEZI Mungu katika Isaya 1:18 anasema: "Njooni tusemezane na katika Isaya 41:21 anasema: "Haya leteni hoja zenu zenye nguvu. Pia Mwenyezi Mungu katika Qur’an 16:125 anasisitiza majadiliano ya namna iliyo bora. Hivyo ni dhahiri kuwa Mwenyezi Mungu anapenda majadiliano yenye hoja; ikiwa ni hivyo nami naomba nafasi katika gazeti lako niweze kushiriki mjadala wa "Siku ya ya kuabudu ni ipi?"
Biblia inatueleza kuwa Mwenyezi Mungu alimaliza kazi zake za uumbaji katika muda wa siku sita na siku ya saba akasterehe (Mwa. 2:1-3). Hii haina maana kuwa Mwenyezi Mungu alipostarehe siku ya saba alichoka kama baadhi ya watoa hoja wanavyofikiri, bali alimaliza kazi zote alizokusudia kufanya, kilichobaki kazi ya uumbaji ilijiendeleza yenyewe kwa njia ya mbegu.
Tangu Mwenyezi Mungu alipomuumba Adam hadi wakati wa Ibrahim hakuweka sheria maalum aabudiwe siku gani bali watu wa wakati huo walimuabudu siku na wakati wowote.
Wakati wa Nabii Musa ndipo Mwenyezi Mungu alipoamua kuweka sheria kuwa siku ya saba aliyopumzika baada ya kazi ya uumbaji ambayo ni Jumamosi iwe siku ya mapumziko na siku ya Yeye kuabudiwa (Kutoka 20:8).
Siku ya Jumamosi yaani Sabato iliambatana na sheria kali za mtu kuuawa endapo ataivuruga Sabato (Kut. 31:14). Ukali wa adhabu ya kutoshika sabato kuliwafanya watu waishike sabato kwa unafiki kwa kuogopa adhabu na wala si kwa moyo mkunjufu, hivyo Mwenyezi Mungu aliona tatizo hilo na akaahidi kulivunja na kuikomesha sabato na siku za mwandamo wa mwezi (Moses 2:11), sambamba na hayo, Mwenyezi Mungu aliahidi kuleta agano jipya litakalokuwa bora kuliko hili la zamani (Yeremia 31:31-32). Agano hili jipya na bora mdhamini wake atakuwa Yesu Kristo (Ebr. 7:22).
Yesu mdhamini wa agano jipya, ndiye aliyekuwa kielelezo cha kuivunja sabato na kutoa ufafanuzi kuwa "Mwanadamu hakuumbwa kwa ajili ya sabato (Marko 2:27:28). Kama ambavyo Ibrahim hakuagizwa kushika sabato, ndivyo nasi leo hatukuagizwa kushika sabato. Katika Yoh. 19:16-19 kuna mtu aliyemuuliza Yesu afanye jambo gani ema ili apate uzima wa milele, lakini alielezwa ashike sheria zingine tu lakini siyo sabato. Watu wanaong’ang’ania kushika sabato leo wameitwa wanafunzi wa Musa siyo wa Kristo (Yoh. 9:28).
Sasa baada ya sabato kukomeshwa ni siku gani inayofaa kuabudu? Biblia inatoa jibu kuwa ni siku yoyote (Rumi 14:5, Gal. 4:9-10). Ni siku yoyote kama ilivyokuwa kwa Adam, Nuhu na Ibrahim. Hivyo anayeabudu Ijumaa au Jumamosi ni sawa, isipokuwa asiwe na dhana kuwa siku anayoabudu ndiyo Mwenyezi Mungu anayotaka aabudiwe siku zote sasa ni sawa (Kolosai 2:16).
Baada ya Mwenyezi Mungu kutuweka huru kuabudu siku yoyote kama ilivyokuwa kwa Ibrahim, Jumapili imechaguliwa na Wakristo kuwa ya kuabudu kutokana na umuhimu wake. Jumapili ni siku ya kumtolea Mungu malimbuko ya mavuno (Law. 23:10). Jumapili ni siku ya Bwana Yesu kushinda mauti (Yoh. 20:1-18). Jumapili ni siku Yesu kuwatokea wanafunzi wake kwa mara ya kwanza toka afufuke (Yoh. 20:19-20). Jumapili ni siku Roho Mtakatifu alipowatokea wanafunzi wa Yesu (Matendo 2:1). Jumapili ni siku ya Kanisa la kwanza lilipoanza mahubiri (Matendo 2:14-41). Jumapili ni siku ya waumini kukutana na kumega mkate (Matendo 20:7).
Hizi ndizo sababu za Jumapili kuwa siku ya kuabudu, lakini pia siku zingine zafaa kuabudu lakini hazina uzito sana ikilinganishwa na Jumapili hasa baada ya Mwenyezi Mungu kukomesha sabato na sikukuu za kuangalia mwezi kama wafanyavyo Waislamu ambazo zimekomeshwa hazipo.
|
|