Habari za Kimataifa kwa ufupi
 
 

Sheria za Viza Zarahisishwa Bahrain

MANAMAH: Taratibu za kutoa viza za kuingia na kufanya kazi nchini Bahrain zimebadilishwa ili kuwawezesha wageni wnaotembelea nchini humo kubadilisha kwa urahisi viza za matembezi kuwa kuwa viza za kufanyia kazi. Wataalamu wenye viza za matembezi wanapopata ajira bora zaidi sasa wanaweza kubadili wadhamini na kupata viza za kufanyia kazi bila ya kuondoka kwanza kurudi kwao. Hapo zamani, wataalamu wenye viza za matembezi ambao walipata kazi iliwabidi kwanza waondoke ndani ya nchi na kisha warudi na viza ya halali ya kufanyia kazi chini ya mdhamini mpya.. Katika sheria hii mpya, viza ya matembezi ya masaa 72, au wiki moja, inaweza kubadilishwa kuwa viza ya ajira kwa gharama ya Dinar za Bahrain 60, kwa ulazima kwamba mdhamini mpya amepata viza ya halali ya ajira toka Wizara ya Kazi na Mambo ya Jamii.


Eid el fitr ndani ya Ikulu ya Marekani

Kwa mwaka wa tatu mfululizo mke wa Rais Clinton, Bibi Hillary Clinton aliwaalika kiasi cha Waislamu 100 wa Marekani kuja Ikulu kuadhimisha sikukuu ya Eid el Fitr siku ya tarehe 25 Januari 1999. Wakati Bibi Hillary Clinton alipowasili, ukumbi ulishajaa waalikwa. Aliwakaribisha wageni na kuwahutubia juu ya uzuri wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambapo aliutaja kuwa ni mwezi wa kutafakari, kujikumbusha na kutia nguvu mwenendo mzuri wa muumini katika mahusiano yake na binadamu wengine.

Hillary Rodham Clinton alielezea kwa kirefu kuhusu safari yake ya Jerusalem, ambako ni sehemu takatifu kwa dini zote tatu kubwa ulimwenguni na mchango wa Uislamu katika elimu na muelekeo wa fikra na elimu ya Ulaya. Baada ya hotuba yake Bibi Clinton alichanganyika na waalikwa na baadaye akawakaribisha kupata vinywaji katika ukumbi mwingine wa Ikulu.


Wasomi wapata Zawadi za Mfalme Faisal

RIYADH: Wasomi 8 toka Mashariki ya Kati, Ulaya, Asia na Australia wameshinda zawadi za kila mwaka zijulikanazo kama King Faisal International Prizes zenye thamani ya dola za Kimarekani 200,000 kwa kila mmoja, maafisa wa Saudi Arabia wamesema hivi karibuni.

Zawadi hutolewa kwa mchango katika kuupeleka mbele Uislamu, elimu ya tiba, Sayansi, Elimu ya dini ya Kiislamu na Fasihi ya lugha ya Kiarabu. Sherehe ya kuzawadia itafanyika baada ya mwezi mmoja, King Faisal Foundation walisema.

Kauli hiyo ilisema Juma Al-Majid Abdullah wa Umoja wa Falme za Kiarabu alikuwa mshindi kwenye tuzo ya mchango wa kuupeleka mbele Uislamu katika "kuutambua mchango wake mkubwa wa ubinadamu, hasa katika upande wa elimu ya dini ya Kiislamu".

Jumuiya yake Bwana Abdullah yenye makao makuu Dubai, inayojulikana kama Kituo cha Utamaduni na Urithi (wa mila za Kiarabu) hutoa huduma za bure pamoja na missada mingine kwa wanafunzi wa utamaduni wa Kiislamu na Kiarabu.

Ripoti ilitolewa na King Faisal Foundation iliwataja washindi kuwa:

Sheikh Mohammed Nasireddin al-Albani, Msomi wa Syria, katika Elimu ya dini ya Kiislamu.

Ryoji Noyori wa Japan na Dieter Seebach wa Ujerumani katika upande wa Sayansi. -Maprofesa Patrick G. Holt wa Australia na Stephen T. Holgate wa Uingereza katika elimu ya tiba.

Makarim Ahmad al-Ghamri wa Chuo Kikuu cha Ain Shams kilichopo Misri na Said Abdel Salam Allouche wa Morocco katika fasihi ya Kiarabu.

Tuzo hizi zilianza kutolew mwaka 1979 na kituo kijulikanacho kama King Faisal Foundation kama kumbukumbu ya Mfalme wa tatu wa Saudi Arabia.



Stempu za Malcolm X zaendelea kuuzwa

NEW YORK: Stempu ya posta ya kumbukumbu ya Malcolm X (Al Hajj Malik Shabazz) zilianzwa kuuzwa kwa heshima ya mtu ambaye hapo mwanzo aliandamwa na FBI (Shirika la upelelezi la Marekani) kwa sababu ya harakati zake za kudai haki sawa kwa watu wote.

Malcolm X, ambaye aliuawa katika ukumbi wa Harlem mwaka 1965, "alikuwa mtu mwenye kuona mbali, mtu aliyekuwa na mtazamo wa dunia bora zaidi na akathubutu kuchukua hatua kuleta mabadiliko" alisema gavana wa huduma za posta S.David Fineman katika uzinduzi wa stempu hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Apollo uliopo Harlem New York.

Malcolm X alijiunga na Taifa la Kiislamu mwaka 1952 na akawa msemaji mkali na hodari ambaye alihubiri utaifa kwa watu weusi wa Amerika katika miaka ya mwanzo ya mwaka 1960. Alikuwa akifuatiliwa na makacero wa Serikali ambao walikuwa na mashaka na malengo ya mahubiri yake na mtazamo wake kwa wazungu.

Mwaka 1964 baada ya kutengana na mwanzilishi wa Taifa la Kiislamu Elijah Muhammad na kisha kufanya Hijja iliyompelekea kurejea Uislamu sahihi, alianzisha umoja ulioitwa Organization of Afro-American Unity (OAAU), na kuanzisha msikiti mwingine Harlem. Wamarekani weusi watatu walipatikana na hatia ya mauaji ya Malcolm X, ambayo pia yalishuhudiwa na familia yake yote.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook