Wakati Ukigoma na Uimanye ukishamiri Moro mjini:
 
Wakristo waritadisha Waislamu Mwidu
 

Na Mussa Ally, Morogoro

WAKRISTO wa mjini hapa hivi karibuni wameitumia vyema fursa ya misuguano ya Masheikh wa Morogoro kwa kuritadisha mamia ya Waislamu wa Kijiji cha Mwidu akiwemo Imamu wao Sheikh Nadhiru Muhammed.

Kwa mujibu wa Katibu wa Msikiti wa Kijiji hicho kilichoko jirani na Magereza Bwawani mpakani mwa mkoa wa Morogoro na Pwani, Bw. Ramadhani Shaaban Machupa, Waislamu wa Kijiji hicho hivi sasa wamebaki wameduwaa baada ya ‘ulamaa’ wao ‘ ‘kuvunwa’ na walokole.

Akiongea na gazeti hili kijiji hapo hivi karibuni, Bw. Machupa ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Serikali ya kijiji hicho alisema kuwa Sheikh Nadhiru ambaye ana elimu ya sekondari na cheti cha Maarifa ya Uislamu toka Markaz Gongo la Mboto Dar es Salaam alikuwa mwalimu pekee anayetegemewa na Waislamu katika shughuli mbalimbali za Kiislamu, hivyo kuritadi kwake kumewasambaratisha Waislamu.

"Kibaya zaidi ni pale alipoingia Msikitini akiwa ndani ya suti nyeusi, tai na rozali shingoni pamoja na Biblia na kutuambia kwamba kile chote alichotufundisha kwa zaidi ya miaka miwili (Uislamu) tangu 1997 si sahihi, kisha akatutaka tumfuate Yesu Kristo na kutuambia kuwa hiyo ndiyo njia sahihi. Zaidi ya nusu ya Waislamu wakamfuata, inahuzunisha sana", alisema Katibu huyo kwa majonzi.

Uchunguzi uliofanywa na ANNUUR umegundua kuwa Sheikh huyo alipelekwa eneo hilo na wana Tabligh wa Markaz Gongo la Mboto ambao ni Bw. Abdallah Swaalihiin (maarufu Sheikh Mzee) na Bw. Amir Baba wakazi wa Dar es Salaam.

Alianza kazi katika kijiji hicho ambacho asilimia 95 ya wakazi wake ni Waislamu mwaka 1997, kabla ya kuritadishwa na walokole kwa mbinu ya kumuinua kiuchumi na kiroho mwishoni mwa mwaka 1998.

Tangu Januari 1999 hadi sasa Sheikh huyo aliyepewa jina la Mchungaji Erick na kuzawadiwa pikipiki ya kutembelea, amekuwa akiwaritadisha Waislamu kwa kasi akitumia maneno matamu ya Hadith, Lugha fasaha ya Kiingereza na Kiarabu cha Misri pamoja na vivutio vya kiuchumi kuwanasa wafuasi wake hao wa zamani.

Mwandishi wa habari hizi alipotembelea Kanisa hilo kumuona Mchungaji Erick Muhammed alijibiwa na mmoja wa wafuasi wake kuwa kiongozi huyo mpya wa kilokole yuko ndani katika kikao nyeti cha ‘Ushuhuda’.

Nao Maustadh Ally Omar wa Ghazal Muslim, Mshashi na Shaaban Chande wa Jabal Hira Islamic Centre wamejitolea kusaidia kuokoa jahazi la kijiji cha Mwidu, ambapo wamekwisha kwenda kijijini hapo kuona hali halisi ya mambo, halikadhalika wako mbioni kumuona Mchungaji Erick kwa mazungumzo naye katika ofisi yake mpya iliyoko Boma Road mjini hapa.

Wakati hayo yakijiri, magwiji wa kuwagawa Waislamu kwa miavuli ya kiitikadi ambao ni maarufu kwa majina ya ‘Kigomalism’ ( watu wenye asili ya Kigoma), ‘Tuimanye’ (makundi ya Kiruguru) na Masheikh wa BAKWATA na BAMITA wanaendelea kuchuana.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook