Njaa yakithiri Wilayani Karatu
 
 

Na Said Njuki, Babati

UKAME ulioikumba nchi hii mwaka 1997 na kuzidi kwa mvua za El-Nino za mwaka 1998 ndizo sababu kuu zilizobainika kusababisha upungufu wa chakula nchini hususan kaskazini mwa Tanzania.

Hayo yalisemwa na Mbunge wa Karatu Mh. Wilboad Slaa (CHADEMA) wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya jimbo la Mbulu mjini Arusha hivi karibuni.

Alisema kuwa mavuno hayakupatikana miaka miwili mfululizo, hivyo kuweo njaa nchini si jambo lakustukiza.

Akizumzuia hali ya njaa jimboni kwake, Mh. Slaa alisema hali ya njaa ni mbaya sana na inazidi kuwa mbaya pale mifugo inapokosa wanunuzi.

Alitoa mfano kwa kusema kuwa ng'ombe huuzwa kati ya shilingi 10,000 na 20,000 tu na mbuzi ni shilingi 1500 na 3000, wakati debe la mahindi kati ay shilingi 3,500 na 4,200.

"Taarifa ya njaa ni mbaya, pamoja na kwamba Mkuu wa Mkoa amekataa, lakini taarifa ya njaa ni mbaya. Vijiji vyangu karibu vyote hali ni mbaya, sina hata kijiji kimoja kizuri", alisema Mh. Slaa mbele ya waandishi wa habari.

Aliendelea kusema kuwa pamoja na kuuzwa mahindi kati ya shilingi 3,500 - 4,200 kwa debe, bado wananchi wanashindwa kununua kwa bei hiyo kutokana na uchumi mbaya na badala yake wanamudu kununua galoni tu.



Michango yaleta migongano Lushoto

Na Abu Abdullah, Tanga

MICHANGO ya fedha kwa ajili ya uendelezaji wa Madrasat Shadhily iliyoko kijji cha Bazo, Kata ya Vuga Wilaya ya Lushoto imekuwa ndiyo chanzo cha uhasama baina ya waumini wa maeneo hayo.

Hayo yamefahamika katika mazungumzo baina ya mwandishi wa habari hizi na Katibu wa Madrasat, Bwana Musa Mohammed Kiuwa kwenye ofisi za ANNUUR mjini Tanga hivi karibuni.

Ustadh Musa alieleza kwamba mzozo huo ulianza kuibuka kwa kasi kuanzia alipochaguliwa (mwaka 1997) kushika nafasi hiyo badala ya Bwana Abdulkarim Omar Jambia.

Bwana Abdulkarim alikuwa haelewani na mwalimu wa madrasa hiyo Bwana Hashim Salim. Hata hivyo kamati ya madrasa ilikuwa upande wa mwalimu, ndipo Abdulkarim alipoamua kujiuzulu.

Katibu wa sasa, Bwana Musa amelalamika kuwa Katibu huyo wa zamani ameweka vikwazo kila sehemu.

Kutokana na mzozo huo kukua kati yake na uongozi wa sasa, Bwana Abdulkarim aliamua kuhama Msikiti pamoja na wale wanaomuunga mkono na kuhamia Msikiti wa Kiluwai badala ya Msikiti wa Chongo waliokuwa wakisali Ijumaa zamani pamoja na wanakamati.

Kubwa zaidi lililolalamikiwa na Bwana Musa ni uamuzi wa Bwana Abdulkarim kuamua kutumia jina la madrasat Shadhily ya Vuga - Bazo kwa ajili ya michango ya Msikiti na Madrasa za Kiluwai.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Madrasat Shadhily unataka ieleweke kuanzia sasa kuwa kuwa hauhusiki na michango ya aina yoyote inayofanywa na Bwana Abdulkarim kwa jina la Madrasa hiyo.



Fufueni moyo wa kuwasaidia Masikini - Sheikh Mbukuzi

Na Said Shariff

IMAMU wa Masjid Mujahidina Sheikh Mbukuzi Juma Salim amewataka matajiri wafufute moyo wa kuwasaidia masikini badala ya kusaidia mambo ya kipuuzi.

Sheikh Mbukuzi ameyasema hayo wakati wa swala ya Ijumaa iliyofanyika Msikitini hapo hivi karibuni.

"Moyo wa matajiri kuwasaidia masikini umekufa na kuibuka mtindo wa kudhamini na kusaidia vilabu vya michezo, mashindano na warembo huku masikini wakiwa hawana msaada wowote. Wakati umefika matajiri kufufua moyo wa kuwasaidia masikini ili kuinua hali zao za maisha", amesema Sheikh Mbukuzi.

Sheikh Mbukuzi amesema limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa matajiri kutumia mamilioni ya pesa kudhamini na kusaidia vilabu vya michezo na kusahau wajibu wao wa kusaidia masikini.

Amesema kuwa kuacha kuwasaidia masikini na badala yake kusaidia mashindano ya warembo na vilabu vya michezo kwa mamilioni ya fedha ni kinyume na maadili.

Aidha, Sheikh Mbukuzi amesema kwamba matajiri hawana budi kufahamu kwamba utajiri huo wamepewa na Allah (s.w.) kama dhamana na Allah (s.w.) ameelekeza matumizi yake, moja ya matumizi hayo ni kuwasaidia masikini na mbele ya Allah (s.w.) wataulizwa juu ya hilo.
 
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook