RAIS Benjamin William Mkapa anakabiliwa na mtihani kuhusiana na malalamiko ya wananchi juu ya kudhulumiwa haki zao na kufanyiwa vitendo vya kinyama na mamlaka au vyombo vya Dola.
Katika malalamiko ya hivi karibuni wananchi wa Yombo Vituka Lumo waliodai kuwakilisha familia 200 wamemlalamikia Mh. Rais kwamba wamebomolewa nyumba zao kinyume cha sheria na katika hali ya kudhalilishwa.
Wananchi hao wamedai kwamba hivi sasa wapo nje ikiwa ni pamoja na vikongwe, watoto na wagonjwa miongoni mwao wakinyeshewa mvua, kupigwa jua, kutafunwa na mbu na madhila mengine baada ya nyumba zao kubomolewa.
Katika barua yao ya wazi kwa Mh. Rais wananchi hao wameeleza kwamba zoezi la kuvunja nyumba zao limefanywa huku kukiwepo amri ya mahakama inayozuia kuvunjwa kwa nyumba zao mpaka walipwe fidia na kupewa maeneo mengine ya kujenga.
Ni kutokana na hali hiyo wananchi hao wanahoji kwa kutaraji msaada kutoka kwa Mh. Rais Mkapa kwamba je; mwananchi hana haki ya kisheria na mali yake? Na je; haki na uadilifu upo wapi kama atadhulumiwa tu kimabavu!
Aidha, wananchi hao wanahoji je; mwananchi hana haki mbele ya sheria? na je mwananchi anapokuwa mahakamani dhidi ya chombo cha Dola mahakama haina haki kumpa ushindi mwananchi huyo, kama ndivyo sheria inavyoelekeza?
Mwisho wa barua yao hiyo ya Februari 27, wananchi wa Yombo Vituka Lumo wanamuomba Mh. Rais awasaidie walipwe fidia ya mali yao iliyoharibiwa na Tume ya Jiji ikiwa ni nyumba na vifaa vyao pamoja na kupatiwa hifadhi huku wakisubiri kupewa viwanja vingine.
Kwa mujibu wa maelezo ya wananchi wa Yombo ambao wameongea na gazeti hili, mgogoro baina ya wananchi hao na Tume ya Jiji ulianza Februari mwaka jana 1998 ambapo Tume ya Jiji Kanda ya Temeke ilitoa notisi ya siku kumi na nne kwa wakazi wa eneo hilo wahame ili nyumba zao zivunjwe ijengwe shule.
Kabla ya ‘Notisi’ hiyo Februari 20, 1998 wananchi hao wanaeleza kwamba Tume ya Jiji iliwafahamisha kwamba inakusudia kujenga shule ya msingi na kwamba ingezifanyia tathmini nyumba zote zitakazoathiriwa ili wenyewe walipwe fidia.
Baada ya kupewa ‘notisi’ wananchi hao wamedai walifungua kesi mahakamani ambapo mahakama ya Kisutu Machi 9, 1998 ilitoa hukumu ya kusimamisha zoezi la ubomoaji nyumba mpaka shauri hilo litakapotolewa uamuzi na mahakama.
Mahakama hiyo hiyo ya Kisutu Januari 27, 1999 ilitoa hukumu kwamba nyumba za wananchi hao zisibomolewe mpaka walipwe fidia kamili, wapewe viwanja vingine na baada ya kulipwa fidia wapewe miezi mitatu kufanya maandalizi ya kuhama.
Pamoja na hukumu hiyo wananchi hao wanadai kwamba bila ya taarifa Februari 24, mwaka huu Tume ya Jiji Kanda ya Temeke iliendesha zoezi la kubomoa nyumba zao chini ya usimamizi wa askari wenye silaha.
Baadhi ya vielelezo ambavyo gazeti hili limebahatika kuvipata vinaonyesha kwamba waliofungua kesi mahakamani kuhusiana na mgogoro huu ni Mangenyule Irumba na Selemani Nassoro - kesi Na. 47/98 dhidi ya Mwenyekiti wa Tume ya Jiji.
Aidha, hukumu ya mahakama iliegemea vifungu vya Katiba Na. 29(1) na 29(2) vinavyolinda haki na mai za raia ikiwemo ardhi hata ile isiyosajiliwa.
Pamoja na kuegemea hukumu za kesi mbalimbali za nyuma za aina hiyo zilizohukumiwa na Majaji kadhaa, mahakama ilitamka wazi kwamba unapotokea mgogoro baina ya sheria yoyote na kifungu cha Katiba basi sheria hutupwa ikafuatwa Katiba.
Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na Mwenyekiti wa Tume ya Jiji hazikuweza kufanikiwa hadi linakwenda mitamboni.
|
|