Kiswahili kitumike kuendesha kesi - Dk. Saffari
Na Mwandishi Wetu

KUTUMIA lugha ya kigeni katika uendeshaji wa kesi mahakamani ni uvunjaji wa haki za binadamu.

Hayo yamesemwa na mwanasheria Dk.Abdallah Saffari alipokuwa akihojiwa na mmoja wa wataalamu wa lugha ya Kiswahili nchini Bwana Mohammed Mwinyi juu ya muswada wa kitabu chake "Sheria ya Mashitaka na Utetezi".

Dk. Saffari amesema wakati umefika kwa wanasheria nchini kuondokana na taasubi (ung’ang’anizi) kwamba Kiswahili hakijitoshelezi kuweza kutumika katika masuala ya sheria.

Mwanasheria huyo ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa taaluma ya sheria amesema ameandika kitabu cha "Sheria ya Mashitaka na Utetezi" kwa lugha ya Kiswahili ili kuonyesha hoja ya kutojitosheleza lugha ya Kiswahili katika masuala ya sheria haina mashiko.

Dk. Safari amesema kwa kuwa ni kitendo cha kumnyima haki mshitakiwa kuzungumza lugha asiyoifahamu , mahakama kama chombo cha utoaji wa haki, haina budi kuuacha mara moja mfumo huo.

Aidha, amesema kasoro ya kutumia lugha ya Kiingereza katika mahakama za hapa nchini umesababisha malumbano baina ya pande mbili zinazosigana kutokwenda inavyopasa na hivyo kuathiri mwenendo wa kesi na hukumu.

"Wanasheria wasijifarague kutumia lugha ya Kiingereza kuwaonyesha watu kuwa wao ni weledi zaidi wa lugha hiyo, hiyo si kweli", alisisitiza mwanasheria huyo ambaye pia ni wakili wa kujitegemea.

Amesema Kiingereza ni lugha ya tatu au ya nne kwa Watanzania walio wengi wakiwemo wanasheria, hivyo si busara kwa mahakama za hapa nchini kuendelea kutumia lugha ambayo haifahamiki na wahusika.

Wiki iliyopita katika Kipindi cha Malumbano ya Hoja kinachorushwa hewani na Kituo kimoja cha Televisheni Jijini, Dk. Saffari alizungumzia haja ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia badala ya Kiingereza.

Dk. Saffari alionyesha ugumu wanaoupata wanafunzi wa sekondari na elimu ya juu kutokana na utumikaji wa Kiingereza katika ufundishaji.

Alisema licha ya kukabiliwa na ugumu wa dhana za masomo mbali mbali wanafunzi hutatizwa na kikwazo cha lugha ya kigeni.

Mbali na kitabu chake cha "Sheria ya Mashitaka na Utetezi", Dk. Saffari pia ameandika kitabu chengine alichokiita "jinsi ya kufundisha sheria."

Hata hivyo ANNUUR imefahamishwa kuwa vitabu vyote viwili vimekwama kuchapishwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa mwandishi ikiwemo ya ukosefu wa pesa.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook