Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Bakwata Mkoani Kilimanjaro ameupa uongozi wa Manispaa Moshi siku saba kusafisha jina lake vinginevyo ataupeleka mahakamani.
Tishio hilo la Katibu wa Bakwata Bw. Malya limekuja kufuatia taarifa ya Manispaa kwamba ameuza ukumbi wa Waislamu kwa shilingi milioni sita na tayari ashapokea milioni mbili.
Kufuatia taarifa hizo maelfu ya Waislamu wa Mkoa wa Kilimanjaro mwishoni mwa wiki iliyopita walikusanyika mjini Moshi kutafakari juu ya hatua za kuchukua.
Katika mkutano huo iliamuliwa kwamba hatua za kisheria zichukuliwe mara moja kusitisha uuzaji huo na pili ziandaliwe taratibu za kudai majengo na ardhi
ilipo shule ya Msingi ya Mwenge ambapo ndipo lilipo jengo la ukumbi huo ambao awali lilitolewa kama Wakfu.
Kufuatia mkutano huo ambao umeonekana kutikisa kiti cha Bw. Malya, kama alivyofanya awali, Bw. Malya amejibu mapigo kwa barua kali yenye kukanusha madai ya kuuzwa jengo hilo la Wakfu.
Katika barua yake yenye Kumb. No. BMK/HOLI/101/127 ya Februari 25, 1999 Bw. Malya anakubali kupokea shilingi milioni mbili, lakini amedai kwamba si sehemu ya malipo ya mauzo.
Hata hivyo, hakueleza fedha hizo alizipokea toka Manispaa kwa lengo gani au kama malipo ya nini.
Bw. Malya amedai kwamba amefanywa na Manispaa aonekane muongo mbele ya Waislamu na hivyo kutokuwa na imani naye.
Aidha, amedai kwamba vurugu zinaweza kutokea kutokana na Waislamu kuja juu kudai ukumbi wao na kwamba hilo likitokea uongozi wa Manispaa ndio utakaowajibika.
Katika barua hiyo ambayo nakala yake imesambazwa kwa makamanda wa Polisi katika ngazi mbalimbali mkoani Kilimanjaro, Bw. Malya ameshikilia kwamba hata kama amepokea shilingi milioni mbili, lakini hakuna mkataba wala makubaliano yoyote ya kimaandishi kuthitibisha kwamba Manispaa wameuziwa jengo la Waislamu.
Jana ANNUUR iliwasiliana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi ambaye alisema kwamba asingependa kulizungumzia zaidi suala hilo kwani lipo kwa Mkuu wa Mkoa na wao Manispaa wanatakiwa wapeleke taarifa yao kwake.
Hata hivyo, kuhusu utata uliojitokeza Mkurugenzi huyo alieleza kwamba wao hawana tatizo kwani makubaliano yapo na kama lipo tatizo ni la Malya na wenzake (Bakwata na Waislamu).
Alisema fedha za serikali haziwezi kulipwa bila ya taratibu zenye kueleweka. Hivyo kudai kwamba hayapo makubaliano wakati sehemu ya fedha ishalipwa tena kwa hundi ni jambo lisiloeleweka; "na hiyo fedha alipokea ya nini", alihoji Mkurugenzi wa Manispaa.
Waislamu mbalimbali waliohojiwa na gazeti hili wameeleza kwamba hawana tamaa yoyote ya kusalimisha mali za Waislamu zinazohujumiwa.
Wameeleza kwamba wajumbe wa Kamati na vikao mbalimbali ambao ndio wangewatia adamu na kuwawajibisha viongozi wanaokwenda kinyume na maadili ya majukumu yao; wamekuwa kama ndio waajiriwa na watumishi wa viongozi. Wamekuwa ni watekelezaji tu yale wanayoambiwa na waajiriwa wao ili muradi tu wanapata posho zao za vikao.
Kwa upande mwingine imeelezwa kwamba hali ya Waislamu kuzembea na kutofuatilia mienendo na utekelezaji wa majukumu ya wale waliowapa ‘amana’ ya uongozi imechangia sana kuzorota kwa maendeleo ya Waislamu.
Bw. Abufatah Mushi akiongea na mwandishi wa habari hizi nje ya Msikiti wa Riadha, alisema kwamba mambo yanaharibika kwa sababu ama Waislamu hawafuatilii mambo au wanakuwa wasemaji tu wasiochukua hatua madhubuti za kiutekelezaji.
Tatizo lingine amesema kwamba wamekuwa waoga
sana kiasi cha kushindwa hata kudai haki zao au kumkabili yule anayewadhulumu
au kuwavurugia maendeleo yao.
|
|