Mkutano wa Bakwata Dodoma batili - Sheikh Yahya
 

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Habari, Mjumbe wa Halmashauri Kuu na msemaji mkuu wa Bakwata nchini, Sheikh Yahya Hussein amesema mkutano wa Halmashauri ya Bakwata uliofanyika Dodoma hivi karibuni ni batili.

Sheikh Yahya amedai ubatili huo umetokana na kwamba baadhi ya waliohudhuria mkutano huo si wajumbe wa Halmashauri Kuu bali ni wafanyakazi wa Bakwata ambao waliingizwa katika mkutano kuziba nafasi za wajumbe halali.

Sheikh Yahya aliwataja baadhi ya wajumbe hao waliongizwa ‘kinyemela’ kuwa ni Bwana Musa Hemed bin Juma ambaye amedai ndiye aliendesha kikao hicho, Ameir Moyo, Bakari Yusuf, Abasi Kihemba, Rajab Mndewa na mtu mwingine aliyemtaja kwa jina la Mahanywa.

Sheikh Yahya alimuelezea Musa Hemed kama ni mtu aliyeteuliwa na Mufti wakati kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata wadhifa aliovikwa ulipaswa utokane na kuchaguliwa na Kamati Kuu.

Aidha, alisema ilikuwa ni kinyume na utaratibu wa Baraza hilo kwa Bwana Musa kuwa msemaji na kuendesha mkutano akiwa katika nafasi ya Ukatibu Mtendaji.

Bwana Musa Hemed ni mtoto wa Mufti wa Bakwata Sheikh Hemed bin Juma.

Kuhusu kuvunjwa kwa Kamati Kuu ya Bakwata, Sheikh Yahya amedai jambo hilo halikuzungumzwa wala kupigiwa kura na ‘Halmashauri kuu’ bali ‘lilichomekwa’ na baadhi ya watu ambao amesema waliteuliwa na Bwana Kundya.

"Watu hao saba nao hawakuchaguliwa na Halmashauri Kuu bali majina yao yalisomwa na tu na Mufti alikubali", amedai Sheikh Yahya.

Mtafaruku ndani ya Bakwata umekuja baada ya kuibuliwa tuhuma kwamba kuna watu ndani ya Baraza hilo wamekuwa wakitumia nembo ya Bakwata kujinufaisha.

Kwa upande mwingine zipo tuhuma kwamba Bakwata ni kampuni binafsi ambayo humilikiwa na kiongozi wake wa juu ambaye huweza kumteua au kumwondoa amtakaye.

Jitihada za kuwapata wahusika wengine wa Baraza hilo kuelezea mtafaruku huu hazikuweza kufanikiwa wiki hii.
 
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook