BARUA
 

Serikali iache kuhadaa wananchi

Ndugu Mhariri,

Serikali ieleze kisa cha kweli ili raia tujuwe. Serikali na Waislamu wana ugomvi gani? Ama sivyo tutaamini malalamiko yao wenzetu (Waislamu) kwamba hapa Tanzania wao wamebanwa mno, sasa yawezekana Serikali inatumia kuuwa, vitisho, propaganda za uwongo ili kufukia madai ya wapigania uhuru wenzetu, mumeusoma kwa makini waraka wa kamati ya kutetea haki za Waislamu uliochapishwa katika gazeti hili na katibu wa kamati hiyo Ponda Issa Ponda, nimegundua waraka huo unatoa picha ya kweli kwa asilimia 99, kuliko maneeo ya serikali. Hata ombi lao la kutaka kumkamata Ponda kwa mujibu wa waraka huo ni kitendo cha dhuluma.

Hivyo serikali kama ina ugomvi na Waislamu wa nchi hii, ituambie au watafute uwongo nzuri, sio kusingizia Mihadhara ya kashfa kwani hali tunayoenda nayo, itaunda matabaka, Watanzania tutakufa sana na nyinyi viongozi mtakimbia nchi za nje? Rudisheni haki za watu hata kwa kujiuzulu.

Mmesema mengi mara kuna mkono wa siasa, mara balozi zahusika, mara wafanyi biashara, mara wanakashifu dini za watu.

Tuelezeje? Serikali isituhadae wananchi kwa kila jambo hata haya ambayo tunayashuhudia kwa macho yetu.

Josephinah Mbwambo,
S.L.P osta 846, DSM



Kama Rufiji wana Uwawaru na nyinyi mna Uwawata
 

Ndugu Mhariri

NITENGEE nafasi kidogo kwenye gazeti lako ili niwatanabaishe Waislamu juu ya unafiki tulio nao.

Masheikh pamoja na Waislamu tumepiga kelele sana na kuwalaani Waislamu wa Rufiji kukubali kujiingiza katika umoja na Wakristo. Lakini na sisi umoja huo pia si tunao! Tena wetu sisi na wa nchi nzima. Umoja wa Waislamu na Wakristo UWAWATA au kwa jina maarufu CCM.

Nasema hivi kwa sababu katika uchaguzi wa mwaka 1995 palikuwa na mgombea Muislamu katika nafasi ya Urais tena aliwashinda wote kwa sifa za kielimu na za kisomi.

Lakini Masheikh na Waislamu hao hao ndio walikuwa wakielezana kupanga njama asichaguliwe na kuwapa kura wale waliomo ndani ya umoja wao wa UWAWATA!

Huu ni msiba mkubwa sana Waislamu wa kutojifahamu sisi wenyewe, na baadaye tunaishia kutumiwa.

Mwaka 2000 unakaribia, karibu utawaona waliomo kwenye UWAWATA wakianza kupewa tenda. Waislamu tuwe na hadhari kubwa na umoja huo. Tusije tukawalaani Waislamu wa Rufiji wakati sisi pia tunastahiki kulaaniwa zaidi maana umoja wetu ni mkubwa zaidi, mpaka inafikia Waislamu kuuliwa pale Mwembechai na polisi wa serikali ya umoja wetu. Lakini bado twaipongeza na kuitetea. Laahaula!

Capt. Ahmad A. Al-Amoudi,
Box 5316,
Tanga.



Wahariri waenzi fani ya habari
 

Ndugu Mhariri,

NAOMBA nafasi katika gazeti lako nitowe wasi wasi wangu.

Fani yahabari na vyombo vyao ni muhimu sana na hili si jambo linalohitaji maelezo marefu.

Jambo linalotisha ni kasi ya kuanguka kwa maadili katika fani hii muhimu.

Linalotisha zaidi ni kule kuona wahusi kakatika kuanguka kwa maadili ya habari si wana habari wenyewe.

Haya ninayo yasema kwa zama hizi hayahitaji mtu kuwa mtaalamu sana kuyaona.

Ni jambo la kawaida sasa Mwandishi kuandika habari ya uzushi; matusi, habari bila utafiti, uchochezi n.k.

Ni jambo la kawaida kumsikia Mwandishi anaahidi "Kama hanijui ngoja nikamkandie". Mwandishi anaandika hali ya kuwa anayakini kabisa kuwa anachokiandika ni uongo lakini anaamua kukirusha hewani.

Hali hii sasa inapelekea wananchi Tanzania kuanza kudharau fani ya habari kama walivyo dharau siasa kwa kusema "Siasa ni uongo".

Dhana ya Waandishi wa habari ni waongo, wambea, wachochezi ina komaa na bila shaka kizazi kijacho haitakua dhana tena bali itakuwa "hakika".

Lakini katika hali hii wakulaumiwa ni nani? Wakulaumiwa ni Wahariri wa Vyombo vya Habari na hasa wale wa magazeti. Binafsi taasisi za serikali za kudhibiti habari sizikubali kwa kuwa haziko kwa lengo la kutoa uhuru wa kweli na kuinda maadili ndio maana tegemeo langu kubwa ni Wahariri..

Sifa za Mhariri zinazothibitisha umahiri wake huonekana katika habari anazo ruhusu katika chombo chake, mwenendo katika upokeaji na utoaji wa habari.

Nimelazimikakushika kalamu kutokana na kasoro na kero nyingi zinazojitokeza katika magazeti yetu.

Ni vema nikadondoa moja ya habari iliyochapishwa katika gazeti moja litolewalo kila siku Toleo Na. 1608 la Mei 29, 1998 Chini ya kichwa kisemacho KITWANA KONDO ANACHOCHEA VURUGU, AWAJIBISHWE.

Habari hii iliandikwa na Mwandishi Faustino Rwambali. Faustine alimshutumu KK kwa madai yake aliyoyatoa hivi karibuni dhidi ya serikali ya Tanzania.

Kwa kifupi Mwandishi baadaya shutuma zake alitaka mambo matatu yafanyike haraka:

A: Serikali imkamate KK mara moja. B. Mahakama imuingize kama shahidi wa kwaza katika kesi za Mwembechai. C. Chama cha CCM kimhoji kama kilivyomhoji hayati Kolimba.

Katika makala hayo Mwandishi aliueleza wasifu wa KK kwa sifa nne.

Mhaini Mnafiki Mropokaji Mchochezi.

Nikizungumzia mafungu A,B,C. Mwandishi anasahau alichokemea "Uchochezi" na yeye anarudia kwa "Kuichochea" serikali, Mahakama, na CCM kuwa vimkamate KK na kumuweka ndani.

Mwandishi pia alisema KK si msemaji wa Waislamu akasahau kuwa iliyoshutumiwa ni serikali na yeye si msemaji wa Serikali.

Mwandishi pia anauliza kwanini serikali haijamchukulia hatua KK wakati Mwandishi anajua serikali ipo hapa hapa Dar es Salaam na huko anaweza kupata jibu la swali lake ambalo sisi wasomaji ndio lingekuwa na maana kwetu.

Aidha, mwandishi anakiri kuwa KK hajaombwa ushahidi na serikali lakini yeye ana muhukumu kwa kumuita mhaini.

Lakini sahau ya Mwandishi isitushughulishe sana, jambo zito linalozua utata ni jinsi Mhariri wa gazeti letu alivyoridhika kuchapisha makala inayomuelekea mtu kwa lugha chafu za "Mnafiki, Mhariri, Mropokaji, mchochezi n.k.

Mtu anakuwa Mhaini, mchochezi na sifa kama hizi baada ya uchambuzi wa kisheria ambao hatudhani kama Mhariri aliletewa.

Picha inayojitokeza katika hali hii ni Mhariri kutoona tatizo katika lugha ya Mwandishi wake.

Hili ndilo linalotutia wasiwasi na mashaka juu ya fani hii ambayo ina uhusiano wa kila siku na wananchi.

Habari zilizochujwa vizuri huelimisha na kuleta mahusiano mazuri ndani ya jamii.

Kinyume chake huamsha hisia za chuki na malumbano ambauyo huenda yatakuwa na hatimae kuzihusisha koo.

Namaliza kwa kukumbusha kuwa Wahariri bado hawajachelewa wakijikomboa kutokana na kuchapisha au kutangaza habari kwa kuegemea sababu fulani kinyume na maadili ya habari, wanaweza kabisa kubadili kasi ya muelekeo mbaya wa habari nchini.

MFINAGA YUNUS,
NGARANARO ARUSHA.



Waislamu tumechoka kunyanyaswa

Ndugu Mhariri

Tunaomba utupatie nafasi katika gazeti lako tukufu ili nasi tutoe dukuduku letu kuhusu unyama uliofanywa na askari wa serikali ya CCM kwa kuingia kwa nguvu msikitini (mahali pa amani na salama) na kuwadhalilisha na kuwapiga mabomu Waislamu wasio ha hatia.

Kitendo hichi kinaonyesha kana kwamba Waislamu wa Tanzania hatupo katika nchi yetu bali tupo katika nchi ya ukimbizi. Hata hao wakimbizi huwa wanatetewa na Umoja wa Maraifa, lakini Waislamu wa Tanzania hawana wa kuwatetea.

Tulitegemea kuwa angalau vyama vya upinzani vingetutetea au hata kulaani tu mauaji yale lakini hakuna.

Tulitegemea labda vyama vya hiari (NGO's) vingetutetea lakini wapi.

Tulitegemea labda BAKWATA angalau ingetoa tamko hata la kutoridhishwa tu na mauaji hayo lakini wapi.

Kwa upande wa Serikali iliyofanya mauaji hayo sisi tunasema; tumehuzunishwa na kusikitishwa mno. Tumebakia na maswali mengi yasiyoweza kujibika kirahisi.

Je, sisi Waislamu wa Tanzania tumeikosea nini Serikali hii ya CCM?

Je, kuhubiri kwetu dini yetu tukufu na kuwaita watu kwenye njia ya "amani na ukweli" ndio imekuwa nongwa? Mbona walokole wanahubiri na kusema chochote wapendacho juu ya Uislamu lakini hawaambiwi wanakashifu?

Je, Serikali hii inayodai kuwa haina dini ina agenda gani ya siri dhidi ya Uislamu na Waislamu? Au tuseme ina dini rasmi ila inajaribu kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa?

Tunamalizia kwa kusema; mauaji ya Waislamu Mwembechai ni ukiukwaji wa Kitabu cha Allah (s.w), ni ukiukwaji wa sunnah ya Mtume (s.a.w), ni ukiukwaji wa mkataba wa haki za binaadam wa Umoja wa Mataifa ambao Tanzania imeuridhia, ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, ni ukiukwaji wa maadili na heshima ya wananchi wa Tanzania.

Vijana wa Kiislamu
Itigi - Manyoni



Radio Kheri tuleteeni ujumbe

Ndugu Mhariri

NIMESOMA makala ya Bwana Kawela Saidi toka Dodoma iliyochapishwa katika gazeti hili Na. 188 - Shawwal 1419; juu ya Radio Kheri Broadicasting Station.

Yote aliyoandika Bwana Kawela ni ya kweli kwani sasa inapata mwaka tokea tuanze kutangaziwa kuhusu kuchangia Radio Kheri tumeshindwa kutoa michango yetu.

Kwa upande mwingine ninathubutu kusema kuwa uongozi wa hiyo Radio na wao pia wanachangia kuzurota utoaji wa michango.

Ninakumbuka mwaka 1993 kulikuwa kuna matatizo ya sehemu ya kusalia kambi ya wakimbizi (wa Kisomali) kule Tanga. Baraza Kuu likaendeza barua katika Misikiti yote zinazowataka Waislamu wacangishane na baadaye michango viongozi wa Misikiti waiwasilishe Islamic Centre Magomeni. Nadhani lilifanikiwa.

Itakuwa ni vizuri na katika Radio wakatumia mkakati kama huo wa Tanga. Kwa vile uongozi wa Radio uwe unapita Misikitini, katika mihadhara pamoja na sehemu ambazo Waislamu wanakusanyika il wawahamasishe juu ya uchangiaji pamoja na kuwaeleza vipi Radio itakavyokuwa na manufaa kwao.

Kwa kuandika tu katika magazeti kuwa Waislamu tunatakiwa kuchangia kwa kupitia Account. Naona itakuwa hata miaka 35 kwa saabu kuna watu wana uwezo wa kuchangia kati ya shilingi 100 na 1000, lakini inakuwa ni vigumu kwao kutuma katika Account yenu.

Ali Baraka,
c/o Mwaruka,
S.L.P. 872,
DAR ES SALAAM.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook