Kutoka magazeti ya zamani
 

Uchaguzi kwa Unguja 1963?

Mwafrika, No. 808, Jumanne, Agosti 28, 1962

UCHAGUZI Mkuu katika visiwa vya Unguja na Pemba unatazamiwa kufanyika kati ya Januari na Juni mwaka kesho, 1963.

Uamuzi huo unatokana na maafikiano yanayofanyika hivi sasa baina ya vyama vikubwa vya siasa - Afro Shiraz na Zanzibar Nationalist Party (Hizbu).

Katika maafikiano baina ya vyama viwili hivyo ili kuharakisha uhuru kwa Unguja, Hizbu ambayo zamani ilikazania usifanyike uchaguzi mpaka mwaka 1964, sasa inakubali kuwa uchaguzi ufanyike mwezi Juni mwakani, lakini mradi uchaguzi huo utanguliwe na serikali ya wananchi yenye madaraka kamili ndani ya nchi.

Afro-Shiraz

Kwa upande wa Afro-Shiraz inadai kuwa uchaguzi huo ufanyike Januari mwaka kesho. Ingawa hivyo inasadikiwa kuwa maafikiano juu ya swala la uchaguzi yatapatikana baada ya Komiti inayochungua mipaka ya majimbo ya uchaguzi kumalizika kazi zake.

Inasadikiwa kuwa maafikiano baina ya vyama viwili hivyo yametokana na mazungumzo marefu na makubwa kati ya vyama viwili hivyo na Katibu Mku wa Pafmeca, Bwana Mbinu Koinange.

Bwana Koinange alitumwa na Pafmeca baada ya mkutano wake wa Mbeya huko Unguja ili kuchungua mambo yalivyo na kuripoti jinsi ya kuleta maafikiano baina ya vyama viwili hivyo.

Baada ya mazungumzo marefu yaliyokuwa yakiendeshwa baina ya viongozi wa vyama viwili hivyo na Bwana Koinange maafikiano yamefikiwa kwamba Afro Shiraz na Hizbu vishirikiane na Komiti inayochungua mipaka ya majimbo ya uchaguzi.

Pili, vyama vyote viwili vimekubali kwamba vitashirikiana katika kupunguza mikwaruzano ya kisiasa iliyoko hivi sasa katika uchaguzi ujao ili kuihimiza serikali ya Kiingereza ichukue hatua kutoa uhuru kwa Unguja.

Pia Afro-Shiraz imekubali kushirikiana na serikali ya hivi sasa.



Kambona katufanya ngazi - Umma
 

Uhuru No. 941, Jumatano, Agosti 23, 1967

WANANCHI zaidi ya elfu moja, miongoni mwao wakiwemo wenyeviti 31 wa matawi ya TANU katika wilaya ya Morogoro jana walifanya maandamano makubwa kupitia katika mitaa kadhaa mjini humo mpaka kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Bwana C. Kapilima ambako walisoma barua ya kumkataa Bwana Kambona kuendelea kuwa Mbunge wao.

Maandamano hayo ambayo yalianzia katika ofisi ya TANU ya wilaya yalikuwa ni ya kwanza kufanywa mjini Morogoro kumpinga Bwana Kambona tangu atangaze kujiuzulu kwake kama Katibu Mkuu wa TANU na Waziri wa Serikali nchini Tanzania tarehe 9 mwezi Juni mwaka huu.

Barua hiyo ambayo ilisomwa na Bwana Nicholas Kunambi, Mwenyekiti wa TANU, tawi la Matombo, Morogoro Mashariki, imedai kuwa Bwana Kambona amewafanya watu wa Morogoro wajinga na kuwatumia kama ngazi ya kujipatia manufaa yake binafsi; jambo ambalo ni kinyume cha matakwa ya wananchi na serikali ya ujumla.

Akijibu barua hiyo, Mkuu wa Mkoa Bwana Kapilima alisema, aliwashukuru waandamanaji hao ambao hawakusita kueleza wazi ubovu wa baadhi ya viongozi. Alisema kuwa baadhi ya viongozi wamefikia katika hatua ambayo hawajitambui walipo na hawajui la kufanya - kuwatumikia wananchi au kujinufaisha wenyewe.

Aliwaomba wananchi kuwa macho na viongozi wa namna hiyo.

Mjini Dar es Salaam yale maandamano yaliyopangwa kufanywa na wananchi hao wa Morogoro kuja Dar es Salaam kumwomba Rais Mwalimu Nyerere awaruhusu wamchague Mbunge mwingine badala ya Bwana Oscar Kambona yameahirishwa mpaka siku ya Alhamisi wiki hii.

Akitangaza habari hizi jana katika Makao Mkuu wa TANU, mjini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TANU Bwana Pius Msekwa alisema kuwa badala yake waandamanaji hao wameombwa kuandamana siku ya Alhamisi kwenda kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bwana Kapilima kabla ya kuendelea na safari yao ya kuja Dar es Salama siku hiyo ambapo Mwalimu atakuwa amekwisha rejea kutoka Tabora.

Juzi Jumatatu, wenyeviti 31 wa TANU wilaya ya Morogoro kwa niaba ya wananchi wa wilaya hiyo walikata azimio mbele ya mkutano mkuu wa mwaka wa wilaya kuwa hawana haja tena na Mbunge wao Bwana Oscar Kambona ambaye hivi sasa anaishi Ulaya na kwamba watafanya maandamano kuja Dar es Salaam kumwomba Mwalimu Nyerere awaruhusu kumchagua Mbunge mwingine badala yake.



Bibi Titi Unguja

Ngurumo Jumatano, Mei 3, 1961

HUKO Unguja hapo juzi siku ya Jumapili tarehe 30 Mei kulikuwa na hekaheka na sherehe ya wanawake na watu wa Unguja kumpokea Mheshimiwa Bibi Titi Mohammed M.L.C. wa Tanganyika akiwa anatoka hapa Dar es Salaam.

Raia wengi wa kisiwa cha Unguja wengi wakiwa Waafrika walionekana wamejipanga barabarani tangu kuanzia kiwanja cha ndege hadi mjini huku wakiwa wameshika wengine matawi ya majani wakipepea. Wafuasi wa chama cha Afro Shiraz Party walionekana wakiinonea motokaa aliyokuwa amepanda Bibi Titi Mohammed na Mheshimiwa Bw. Abeid Karume huku wakiruka ruka na kuimba nyimbo za uhuru.

Hapo juzi Bibi Titi alihudhuria karamu rasmi ambayo ilitayarishwa kwa heshima yake na chama cha Afro Shiraz kwa kusherehekea uhuru wa serikali ya Tanganyika.



Kwanini waniita kisura?

Ngurumo No. 616, Jumanne, Aprili 11, 1961

KIJANA mmoja wa kama miaka tisa alimwona msichana akienda kwenye mkwaju huko Manyoni Street, Ilala siku ya Jumapili kama saa moja za asubuhi.

Msichana aliporudi kakutana na yule kijana, na kijana alimwona msichana akasema: "Kisura huyu nimemwona kule kwenye mkwaju".

Kamrudishia

Msichana akakasirika na kumwuliza yule kijana; "kwanini waniita kisura?" Halafu akamtukana na baba yake. Kijana kuona mambo yanakuja hivyo naye akamrudishia. Ikawa kuna mashindano ya matusi.

Jamaa aliyesikia ambaye amemuona msichana ni mjukuu wake akauliza kuna nini matusi mabaya, akahadithiwa kuwa mjukuu wake akaitwa kisura halafu kukawa na ugomvi wa matusi. Hapo anayehusika na msichana akamshika yule kijana na kumchapa makofi.

Kapewa chochote

Baada ya kijana kuchapwa makofi akaenda nyumbani, mara akarudi na jamaa yake ambaye alimwuliza yule aliyemchapa makofi kijana kuwa kwa nini kamwadhibu mmoja na mmoja kamwacha kumbe wote walitukanana. Jamaa wa msichana akakubali kuwa kweli amekosa. Ndipo jamaa wa kijana akasema kama kweli kakosa iwepo alama ya kuonyesha kakosa.

Jamaa wa msichana akakubali kutoa chochote kumpa jamaa wa kijana aliyemchapa makofi. Hapo mambo yakamalizika kwa jamaa wa kijana kupewa chochote na jamaa wa msichana aliyeitwa kisura.



Watu elfu nne waliotaka kumuua Rais ndani

Uhuru, Alhamisi, Septemba 30, 1965

HUSSEIN Tawfiq anayeshitakiwa huko mjini Cairo kama kiongozi wa chama kiitwacho Muslim Brotherhood, amesema katika televisheni kwamba nia ya chama chake ilikuwa kumuua Mkuu wa nchi ya Misri kwa kufuatana na staili ile ambayo Rais wa Amerika Kenned aliuawa. Aliongeza ilikuwa ni nia ya chama hicho kutumia bunduki yenye darubini kali inayoweza kumvuta mtu karibu na kumuuwa kwa urahisi.

Hussein akiwa kiongozi wa watu wapatao elfu nne (wote wamekwisha kamatwa), alisema kuwa chama hicho kilianzishwa mnamo mwaka 1963, na baadhi ya mipango yao ni kuiomba nchi ya Ufaransa itoe msaada, lakini nchi hiyo haikutoa chochote.

Mnamo 1945 alihukumiwa kufa kwa ajili ya kosa la kumuua Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Bw. Amin Osman, lakini alitoroka na kwenda nchi ya Syria.

Akiwa huko Syria alihukumiwa tena hukumu ya kifo kwa kutaka kujaribu kumuua Rais wa nchi hiyo Bw. Adib Shishakly. Kwa wakati huu Hussein alikuwa mfanyakazi katika kampuni moja ya mafuta katika Misri, mpaka wakati alipokamatwa.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook