Hassan Omar
Desturi ya binaadamu ni kushitushwa na hali isiyo ya kawaida pindipo ikitokezea. Kwa mfano, kompyuta yako umeiacha nzima jana leo ukaikuta kila ukiiwasha haiwaki, hapana shaka utashituka sana. Utashituka kwa sababu kadhaa lakini mojawapo ni kwa tuhuma kuwa imeshaharibika jambo litakalozua zahama na udhia mkubwa wachilia mbali gharama zitakazohitajika kuitengeneza.
Lakini, mara nyingi tuhuma hizo huwa si kweli. Ushauri wangu ni kuwa siku utakayokuja kuiwasha kompyuta yako ikagoma kuwaka basi kwanza usitaharak! Tulia kimya na taratibu uanze kutafuta sababu ya kwanini kompyuta hiyo imegoma kuwashika, yaani kushindwa kuanza kufanyakazi kama kawaida.
Kwanza angalia kama waya wa umeme wa kompyuta hiyo umechomekwa sawa sawa kwenye ile soketi yake ya umeme na kwenye kompyuta yenyewe. Pia angalia kama soketi ya umeme imewashwa na inaleta umeme kama kawaida. Kuthibitisha hivyo unaweza kujaribu kuunga kwenye soketi hiyo kifaa chengine cha umeme kama vile printa au radio au pasi n.k. Vifaa hivyo vikiwaka basi soketi ya umeme haina tatizo na kama havikuwaka basi matatizo yako hapo - pengine fyuzi imeungua au umeme umezimwa, n.k. Mwite fundi wa umeme afanye uchunguzi na kurekebisha tatizo.
Pili angalia ule waya unaounganisha kompyuta yenyewe na monita yake kama umechomekwa vyema kwenye ncha zake zote mbili. Sikiliza kama feni la kompyuta linazunguka sawa sawa. Kama halizunguki basi kuna uwezekano kuwa "power supply" ya kompyuta imeungua au feni lake limeharibika na itabidi uipeleke kompyuta yako kwa fundi wa kompyuta aiwekee "power supply" nyingine au feni jengine. Kama feni linazunguka utausikia mngurumo kama kawaida.
Kama pamoja na kompyuta kunguruma na taa za mbele kuwaka lakini bado hakionekani kitu kwenye monita basi hakikisha kuwa monita nayo inapata umeme kama inavyotakiwa kwa kuhakikisha kuwa nyaya zake zimechomekwa kama zinavyotakiwa na ile taa yake iliyo mbele inawaka kama kawaida. Kama haiwaki, zima na kuiwasha tena swichi ya monita hiyo mpaka uone taa yake inawaka. Ikiwa bado haiwaki basi jaribu kuipeleka (yenyewe tu bila ya kompyuta) kwenye soketi nyingine ya umeme uone kama itaweza kuwaka au la. Jaribu pia kutumia waya tafauti wa umeme uone kama utaleta tafauti yoyote. Ikishindikana basi monita yako inawezekana imeharibika na itahitaji kupelekwa kwa fundi kutengenezwa.
Kama kompyuta inanguruma, monita inawaka lakini hakionekani kitu kwenye monita au inakwama katikati na kushindwa kuendelea basi inawezekana "hard disk" ina matatizo. Pengine mafaili yanayoifanya kompyuta ianze yameathirika. Hilo hutokezea mara nyingi kama kompyuta yako imeshambuliwa na virusi vya kompyuta (computer viruses).
Kama kompyuta inanguruma na kukwama kabla ya kutoa ule ujumbe "Starting MS-DOS..." au "Starting Windows 95...", inawezekana "master boot record", (MBR), imeharibiwa. MBR, ni programu ndogo inayohifadhiwa kwenye sector ya kwanza ya "hard disk" (hifadhi kuu ya kompyuta), kuifanya kompyuta iweze kujianzisha.
MBR inachokifanya ni kucheki "partition table" kuona kama "partitions" za hard disk yako ziko sawa sawa na kuitambua ni partition ipi ni "active" yaani yenye "boot sector" inayohifadhi "boot record" ambayo ni programu nyengine inayotumika wakati wa kuanzishwa kompyuta. Baada ya kujua ilipo "boot record" huianzisha programu hiyo. Kama MBR imeharibika, au haipo, au partition table imeharibika, basi utaona moja kati ya maneno yafuatayo kutegemeana na aina ya BIOS unayoitumia - AMI, AWARD, Phoenix, Compaq, n.k:
No boot sector on fixed drive - strike F1 to retry boot, F2 for setup utility
No boot device available - strike F1 to retry boot, F2 for setup utility
Invalid partition table
Kama boot sector imeharibika basi utaona maneno kama:
Error loading operating system Missing operating system
Boot record iliyo kwenye boot sector kazi yake ni kuanzisha program zilizo kwenye mafaili IO.SYS na MSDOS.SYS yanayoitwa "system files". Kama boot sector imeharibika, au mafaili hayo yameharibika, au hayapo mahali yanapotakiwa kuwepo, basi utaona maandishi:
Non-System disk or disk error replace and strike any key when ready
Kama inakwama wakati inapotoa ujumbe "Starting MS-DOS..." au "Starting Windows 95..." basi inawezekana pia "boot sector" imeharibika au mafaili IO.SYS na MSDOS.SYS yameharibika.
Kama hitilafu iko kwenye MBR, au boot sector, au system files, jaribu kwanza kuizima kompyuta yako na kuiwasha tena uone kama itawashika.
Fanya hivyo kwa mara kadhaa kabla ya kukata tamaa. Mara nyengine, hard disk hugoma kuzunguka kikawaida na kuna uwezekano wa kuishitua kidogo ukiizima na kuiwasha tena na ikaendelea kufanyakazi kama kawaida. Hali hii hutokezea sana kama hard disk ni ya zamani na ni ishara kuwa kuna siku isiyo ya mbali inaweza kugoma kabisa kabisa. Kwa hivyo ni vyema kuibadilisha. Inaweza pia kutokezea kama kompyuta yako iko kwenye mazingira ya joto sana au yenye mavumbi sana.
Ikishindikana kuwashika, baada ya kujaribu mara kadhaa, sasa itabidi utumie "rescue disk" yako. Kama huna rescue disk, nakushauri mara tu ukimaliza kuisoma makala hii uitayarishe na uiweke mahala dhahibu ili uitumie inapohitajika.
Kuitengeneza rescue disk ni kazi ndogo tu. Chukua disketi tupu (mpya), na kwenye Windows 95, bonyeza Start -> Settings -> Add/Remove Programs -> Startup Disk na ubonyeze kifungo cha Create Disk. Na kwa urahisi zaidi, ukiwa na DOS prompt, ingia kwenye directory C:\WINDOWS\COMMAND na utoe command ifuatayo:
bootdisk a:
Ndani ya disketi hiyo pamoja na kuwekwa mafaili ya kuiwezesha
kompyuta ianze kwa kutumia disketi hiyo, hakikisha kuwa mafaili yafuatayo pia yamo, kama hayamo yanakili kwenye disketi hiyo:
Kutoka kwenye jalada (directory) la C:\WINDOWS
DMDOS.EXE
PROTOCOL.INI
SYSTEM.INI
WIN.INI
WIN.COM
DBLBUFF.SYS
SMARTDRV.EXE
CONTROL.INI
Kutoka kwenye jalada (directory) la C:\WINDOWS\COMMAND
DEBUG.EXE
EDIT.COM
FDISK.EXE
FORMAT.COM
SYS.COM
ATTRIB.EXE
Mafaili, SYS.COM, FDISK.EXE, na FORMAT.COM ni muhimu sana. Utahitaji pia kuweka kwenye diketi nyengine programu ya kuweza "kuua" virusi vya kompyuta kama vile F-PROT au Norton Anti-Virus. F-PROT ni ya bure.
Kama unatuhumu kwamba ni MBR au "boot sector" ndiyo iliyoharibika, hatua za kufanya ni kuitumbukiza rescue disk kwenye kompyuta na kuizima na kuiwasha tena kompyuta. Isubiri mpaka imalize kuwashika na utaona "prompt" ifuatayo:
A>
Ukiona "prompt" hiyo inamaanisha kuwa kompyuta yako imeweza kubuti sawa sawa kwa kutumia disketi ya kubuti. Jaribu kutoa amri ifuatayo:
A> C:
Ukipata "prompt" ifuatayo:
C> basi mambo safi, kwani itaonyesha kuwa hakuna uharibifu mkubwa uliotokea kwenye partition table ya "hard disk" yako. Toa amri ifuatayo:
C> A: ili upate tena "prompt" ifuatayo:
A>
Sasa hapo kwanza tumia programu ya kuulia virusi kuhakikisha kuwa kompyuta yako haijashambuliwa na virusi vya kompyuta. Kama kuna virusi hakikisha umeviua vyote. Baada ya hapo utaitengeneza upya ile MBR kwa kutoa amri ifuatayo: A> FDISK /MBR Unaweza pia kuitengeneza upya ile "boot sector" na "system files" kwa kutoa amri: A> SYS C: Baada ya kutoa amri hizo, itoe ile disketi ya kubuti kutoka kwenye kompyuta yako na uizime na kuiwasha tena kompyuta yako uone kama itawashika kama kawaida. Mara nyingi huwashika. Ikishindikana basi tatizo ni kubwa zaidi. Kuna programu kama vile Norton Utilities zinazosaidia kuitengeneza upya hard disk ambayo imeharibika. Programu kama hizo zina nguvusana na usipokuwa muangalifu unaweza kusababisha upotefu mkubwa wa mafaili yaliyomo kwenye kompyuta yako. Ni vyema sana, kama ninavyosisitiza kila mara, kuweka kumbukumbu ya mafaili muhimukwenye disketi zitakazotumika pindipo kompyuta imekorofisha.
Ikifikia hatua ya kuhitaji programu kama Norton Utilities basi ni vyema kuipeleka kompyuta yako kwa fundi wa kompyuta anayeaminika ili akusaidia kuitengeneza. Mara nyingine sehemu mbali mbali zilizomo ndani ya kompyuta zinaweza kuwa zimechomoka kidogo na kusababisha kompyuta ishindwe kuwashika. Fundi wa kompyuta atahakikisha kuwa kila kitu kimechomekwa sawa kwenye sehemu yake kabla ya kuchukua hatua nyengine zinazofaa.
Cha muhimu cha kuzingatia ni kuwa kompyuta
kushindwa kuwaka hakuna maana kuwa ni tatizo kubwa siku zote. Inaweza kuwa
ni tatizo dogo tu ambalo ukifuata utaratibu kama nilioueleza hapo juu unaweza
kirahisi kabisa kugundua tatizo liko wapi na kuweza kulitatua wewe mwenyewe
bila ya kugharimika kwa kuipeleka kompyuta yako kwa fundi wa kompyuta.
|
|