Tahariri
 
Njia ya kupata Radhi za Mwenyezi Mungu
 
 
Imesemwa katika Qur'an kwamba: Hamtaweza kuufikia wema khasa mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda; na chochote mnachokitoa basi hakika Mwenyezi Mungu Mungu Anakijua. (3:92).

Aya hii ndio msingi hasa wa Uislamu na imani. Utukufu hasa wa Uislamu upo katika msingi kwamba kile kilicho azizi kwako ndicho cha kutolewa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Bila shaka tunaona katika maisha yetu ya kila siku kuwa Mwenyezi Mungu Anatuongoza upande huu, na nafsi zetu zinakuelekezeni upande mwingine. Mwenyezi Mungu Anatuamrisha kufanya hili lakini nafsi zinawashawishi msifanye hilo eti kwa sababu litawaletea mashaka na hasara.

Mwenyezi Mungu Anakukatazeni msifanye jambo fulani, lakini nafsi zinakushawishini kulifanya, eti kwa sababu ni tamu na lenye manufaa. Sasa hapo kuna mambo mawili yenye kuvutana, upande mmoja kuna Radhi za Mwenyezi Mungu na upande mwingine kuna anasa chungu nzima. Kwa ufupi hukutana na njia hizo mbili katika kila hatua ya maisha yake. Njia moja ni Uislamu na njia nyingine ni kufuru na unafiki. Yule aliyepuuza yote ya ulimwengu huu na kukiri amri za Mwenyezi Mungu huyu amefuata njia ya Uislamu, na anayefuata matamanio ya moyo wake na vishawishi vya ulimwengu, huyo amefuata njia ya kufuru na unafiki.

Hali ya Waislamu wa leo ni kuwa wanakubali kwa furaha lolote lililo jepesi katika Uislamu, lakini mapambano yanapozuka baina ya Uislamu na kufuru mara moja hubadilisha msimamo wao. Udhaifu huu hujitokeza hata kwa wale wenye kudai kuwa ni Waislamu katika kiwango cha juu kabisa.

Watapiga kelele Uislamu, Uislamu, kwa ndimi zao mpaka zikauke kwa kuushangilia Uislamu, na pia watafanya kazi za kujionyesha kwa ajili ya Uislamu; lakini wanapoambiwa tu: "Hebu tuanze kutumia Sharia za Kiislamu ambazo tunazisifu sana", bila kusita watasema: "Kuna ugumu katika kufanya hilo na kuna kipingamizi hiki na kile, bora kwa hivi sasa tuache suala hilo".

Kwa hiyo, wana maana kwamba Uislamu ni kinyago kizuri cha kukionyesha katika kabati na kukiimbia nyimbo za kukisifu, lakini wala hafai kufikiria kuhusu kufuata Sharia zake juu ya nafsi zetu, jamii na ndugu zetu, na kuelekeza mambo yetu ya biashara na mengineyo kufuatana na mwongozo wake.

Hii ndio hali halisi ya watu wetu wa Dini siku hizi. Basi ni bora tusizungumze watu wa kilimwengu. Imefikia hatua ambapo Salah, Sawm, au kusoma Qur'an hakuleti kufuata Sharia za Kiislamu. Sababu yenyewe ni dhahiri kwamba roho inapokosekana, muujiza upi mwili mtupu uwezao kuufanya? (Yaani roho ya Uislamu ni kufuata Sharia zote za Uislamu kwa ukamilifu).

Tunaimarisha darsa zetu za watoto, watu wazima, vijana na akina mama. Lakini tuhakikishe kuwa darsa hizo mwelekeo na malengo yake ni kutujaza lengo la maisha yetu, nafasi yetu hapa duniani na lengo la Ibada maalum kama swala na swaumu. Kwa mwelekeo huo tutalea kizazi kitakachousimamisha Uislamu na kufuata Sharia zake zote.
 
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook