Uchambuzi/hoja binafsi
 
Siku ya ibada - Jamaa ni siku ya Ijumaa

Na Salim K. Muhammed

KWANZA namshukuru Mwenyezi Mungu (s.w.) aliyeniwezesha kupata nafasi hii adimu kunijaalia kuandika haya machache kwa Rehma yake, na sifa Njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu Allah (s.w.).

Kuhusiana na suala lako, Mwinjilisti Bunga E. Dettu ambalo ni zuri, na hasa jinsi ulivyojaribu kulielezea kwa undani jinsi unavyolifahamu na kulitupa wazi jambo hilo ili uweze kupata ufafanuzi ulio mzuri na ili uelewe, sasa ukisha elewa ni juu yako, kwa vile umekwisha fahamishwa.

Katika suala lako la pili ambalo umeuliza ya kwamba, hivi kweli Mungu hakutufunulia wazi jambo hili? Jibu Mwenyezi Mungu Allah (s.w.) ambaye Yeye ndiye aliesema "KUWA" tukawa yaani kwa lugha ya Kiebrania "YEHOVA" na kwa jila lake halisi kwa lugha hiyo "ELO". Ambaye Yeye ndiye aliyesema "Mimi niko ambaye Niko" amefunuliwa wazi jambo hili katika Haki.

Kwa wakati uliopita na wana wa Israeli yaani Uma zilizopita na wakati huu tuliopo, hivi sasa ukiwemo wewe na mimi pamoja na wengineo; yaani umati wa Mtume Muhammad (s.a.w.). Hivyo basi inakubidi Mwinjilisti ufanye uvumilivu uyaelewe haya kutokanana kwamba hujayafahamu haya, ndio maana unasema: "Hivyo yatupasa tuelewe wazi kwamba kuna mahali tumefanya makosa, maana haiwezekani Mungu huyu mmoja atuwekee siku mbalimbali za ibada kiasi hiki, na kutufanya tuchanganyikiwe na kujiuliza ipi ni ipi".

Ukweli ni kwamba Mungu tunamzisingia bure maana yeye ameweka wazi kila jambo linalohusu wokovu wa maisha yetu. Wenye shida ni sisi wenyewe.

Na shida hii Mwinjilisti Dettu ni kwa sababu pameharibiwa hapo, na hali palipo na ukweli pameachwa na wengi hawapafuati. Hivyo wale ambao wanapafuata hapo palipokuwa na hiyo kweli wao hawana wasiwasi; na hiyo siku ya ibada kwa wote pamoja, kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye ameumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake na kuitawala hiyo arshi yake.

Sasa tukianzia mafundisho yako uliyopokea unasema kwamba; Mungu aliumba mbingu na nchi na vyote vilivyomo kwa muda wa siku sita ya saba akapumzika, akaacha kufanya kazi zake zote alizoumba na kufanya, Mwanzo 2:1-4. Maneno haya huoni kwamba yanapingana na mafundisho aliyoyatoa Nabii Isaya 40:28. Je! Wewe hukujua? Yeye Mungu wa milele Bwana, Muumba Miisho ya dunia, hazimii wala hachoki; akili zake hazichunguziki.

Kwa hiyo, Mwinjilisti, anayechoka anapumzika na kupumzika ni kuacha kufanya kazi; kwa vile Nabii Isaya anasema Mwenyezi Mungu hachoki, hivyo hapumziki na kwa vile hakupumzika pia hawachi kufanya kazi yake, ndio maana wanaadamu na viumbe vingine vinazidi kuumbwa au kuumbika kwa neno "Kuwa" na hata ardhi nayo inatosha mimea kwa kunyesha mvua, hivyo Mwenyezi Mungu hana udhaifu wa "uchovu". Hayo ni ya viumbe, ya "uchovu" na kustarehe.

Sio siku sita ni nyakati sita:

Kwa mapokeo yako Mwijilisti unadhani kwamba Mwenyezi Mungu, ameiumba dunia hali ya kuwa usiku na mchana upo; kwa sababu huo usiku na mchana unapatikana wakati sayari ya dunia inapolizunguka jua, ndio siku nayo inaingia au inapatikana. Hivyo sivyo; bali Mwenyezi Mungu anasema katika sura ya 57:4: Yeye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita kisha akakaa katika ENZI (yake). Anayajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo na yanayoteremka kutoka mbinguni na yanayopatikana humo. Naye Yu pamoja nanyi pomoja nanyi popote mulipo. Na Mwenyezi Mungu anaona mnayoyatenda (yote). Kwa kupambanua kuhusiana na nyakati, ni wakati + wakati, mpaka zifike sita = na nyakati sita. Kwa kupambanua kuhusu siku; ni siku + siku = na siku hadi zifike siku sita; hizo ni siku, usiku hadi asubuhi, navyo pia vinahitajika kuumbwa. Na hizo nyakati ni mfano wa mara ya kwanza na mara nyingine na nyingine hadi hizo mara zifike sita; kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa "Subra" na huwapenda wenye kusubiri katika kila jambo.

Hivyo dhana ya siku ya kuumba ya sita haiingii akilini; na siku ya kustarehe pia haiingii akilini yaani siku ya Jumamosi, kwa sababu ya kustarehe na kupumzika, kwanini isiingie akilini? Kwa sababu ya mafundisho hayo tuliyoyaona.

Pia kwa vile Mwinjilisti umetoa mfano wa kujipatia uhuru kwa taifa la Tanganyika hiyo tarehe 9/12/1961, na kwa sababu ya kukumbuka siku hiyo na kuelezea kwamba itakuwa, je, atatokea mtu aibadilishe siku hiyo; mimi nakuuliza kidogo kwamba je! Ikiwa katika tarehe hiyo 9/12 palitokea mwaka mmoja taifa letu likapata msiba mkubwa wa maafa usioweza kulinganishwa na maafa yoyote yaliyowahi kutokea duniani, Je, bado watu watakaobakia watasheherekea tena kwa kumbukumbu hiyo katika tarehe hiyo? Sasa akisema kiongozi kuibadili tarehe iwe ni mgogoro mkubwa? Nadhani mgogoro wetu sio tarehe bali ni siku ya ibada kwa wote.

Wakati tulipompa madaraka Rais wa Taifa la Tanganyika, hiyo siku ya kwanza hakupumzika au hakustarehe, na kama ni mapumziko ya kawaida kwa vile yeye ni mwanaadamu na anao udhaifu huo. Bali Rais wetu alianza kazi yake kwa "kutawala nchi yake rasmi" nae aliendelea na kazi yake hadi muda wake ulipoisha. Kwa udhaifu wa maumbile ya kibinadamu ndipo alipoona sasa upo uwezekano wa "kustarehe" na "kupumzika".

Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.) Yeye hana udhaifu huo wa kibinadamu, ndio maana anasema katika Isaya 40:28 Je! Wewe hukujua? Nadhani sasa tumejua ya kwamba aliyeumba hazimii wala hachoki na akili zake hazichunguziki.

Kutafutwa kwa sharia ya Mwenyezi Mungu

Sasa Mwinjilisti tuje katika sharia yake Mwenyezi Mungu (s.w.) kama anavyosema katika Isaya 33:22: Kwa maana Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu, ndiye atakayetuokoa. Isaya 46:9: Kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine, mimi ni Mungu, hapana aliye kama mimi.

Hao tunaowakumbuka ni wa zamani za kale watu au umati uliopita pia katika Qur’an sura 45:28: Na utauona kila uma utaitwa kwenda (kusoma) kitabu chao (waambiwe)" Leo mtalipwa yale mliyokuwa mkiyatenda".

Kwa hiyo mafundisho haya ya sharia za Mwenyezi Mungu yanatuambia kwamba kila uma utafika na kitabu chao ili ithibitike iliyo kweli. Na Mwenyezi Mungu anasema katika sura 22:34: Na kila uma tumewafanyia mahali pa kuchinjia mihanga ya ibada ili kulitaja jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile alivyowaruzuku katika wanyama hao wenye miguu minne, basi Mungu wenu ni Mungu mmoja tu. Jinyenyekesheni kwake. Na waambie khabari njema wale wanyenyekevu.

Kwa mafundisho haya ni kwamba uma zilizopita tunazikumbuka kwamba zilipewa sehemu ya kufanyia ibada hii muhimu ya kuchinja, yaani kwa kuelekeza ibada hiyo katika sehemu aliyowaridhia Mwenyezi Mungu: (i) Katika milima ya Sinai. (ii) Katika Misikiti (Hekalu) takatifu alilolijenga Nabii Daud pamoja na mwanawe Nabii Suleimani (a.s). (iii) Na uma huu wa Nabii Muhammad (s.a.w.). Tumeamrishwa tuelekeze ibada hii muhimu katika Msikiti mkongwe wa Al-Ka’aba.

Jambo la msingi ni ibada ya Mwenyezi Mungu ipo pale pale ya kuchinja na mabadiliko ni mwelekeo, ambao nao uwe umeridhiwa na Mwenyezi Mungu Allah (s.w.). Na pia mabadiliko hayo alianza kuyafundisha Bwana Yesu katika Yohana 4:21: Yesu akamwambia mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu wala kule Yerusalem.

Na katika sura 22:43: Kwa ajili ya kutakabari kwao katika ardhi, na kufanya vitimbi vibaya haviteremkii ila yule aliyevifanya. Basi hawangoji ila desturi (ya Mungu) iliyokuwa (aliyoipitisha) kwa watu wa zamani! Wala hutapata mabadiliko katika kawaida (dasturi) ya Mwenyezi Mungu (aliyoiweka) wala hutakuta mageuko katika kawaida ya Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo katika ibada ya Mwenyezi Mungu amri yake ya kuchinja na pia ibada ya pamoja haibadiliki, hizo ni ibada za milele. Bali Mwenyezi Mungu hutupa lile jepesi na lililo bora. Kama anavyotuambia katika sura 2:106: Aya yoyote tunayoifuta au kuisahau tunaleta iliyo bora. Kuliko hiyo au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu?

Sabato - Sabathlyum - Siku ya saba

Katika Mambo ya Walawi 16:29: Amri hii itakuwa amri ya milele kwenu; katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi mtajitaabisha roho zenu, msifanye kazi ya namna yoyote, mzaliwa na mgeni akaaye kati yenu.
Walawi 16:30-31: Kwa maana siku hiyo upatanisho utafanya kwa ajili yenu ili kuwatakasa ninyi mtakaswa wa dhambi zenu zote mbele ya BWANA. Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika sabato kuiangalia sana hiyo sabato katika vizazi vyao vyote ni agano la milele.

Zaburi 50:5: Nikusanyieni wacha Mungu wangu waliofanya agano nami kwa dhabihu. Na hiyo dhabihu na hiyo sabato ni amri za milele.

Nini maana ya neno Sabato? Maana ya neno sabato ni siku ya saba au kwa Kiarabu lugha ambayo inafanana na Kiyahudi ni "Sabahthlyum" wanaadamu wanatakiwa wamuabudu Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa kulitaja jina lake na kumshukuru kwa sababu Yeye Ndiye aliyetuumba na aliyetuumbia tunavyoviona na vinginevyo kwa hiyo tunahitajika kwa siku maalum kukusanyika pamoja kumshukuru. Siku ambayo ameiridhia Mwenyezi Mungu (s.w.). Sabato ni siku ya Jumamosi wanadamu wanaiabudu siku, bali wanamuabudu Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaiabudu siku ya Jumamosi ambayo hiyo siku yenyewe nayo imeumbwa na Mola, itakuwa ibada yako siyo sahihi. Ila tu kama umepata maelekezo ya sharia ya Mwenyezi Mungu barabara. Kwa hiyo Sabato ni siku tu ya saba; kinachohitajika ni ibada ya sawa sawa; hali kadhalika dhabihu.

Katika umma uliopita tumejifunza kwamba hicho kizazi cha wana wa Israeli walipewa siku hiyo ya sabato yaani siku ya Jumamosi na masharti magumu kwa ajili ya uma wao ulivyo kwamba asietii amri hiyo kwa kufanya kazi atauawa au nafsi hiyo itakataliwa mbali na watu wake. Ina maana atapewa adhabu kali au aina fulani ya adhabu. Kwa hivi sasa tunahitajika kuujuwa muongozo wetu au (ramani yetu) halisi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Vinginevyo utapata "tabu".

Itaendelea toleo lijalo

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook