Na Muhibu Said
KATIKA hatua inayotafsiriwa na wengi kama juhudi za kulihami Kanisa, serikali wilayani Temeke imepiga marufuku mihadhara ya dini katika maeneo ya wazi kwa zaidi ya siku mbili.
Hatua hiyo ya uongozi wa Wilaya ya Temeke imekuja muda mfupi baada ya Khidmat Da’wah Islamia kupiga muhadhara mfululizo uliowaacha Wakristo 51 wakiwa wamerejea katika Uislamu.
Bw. Magezi ambaye mwaka jana Februari alikamatwa na polisi katika juhudi hizo hizo za kuzima mihadhara inayowarejesha watu katika Uislamu, ameelezewa kurejea jukwaani akiwa na nguvu mpya baada ya kukaa gerezani (rumande) takriban nusu mwaka. Kukamatwa kwa Ust. Magezi mwaka jana ndiko kulikozua balaa Mwembechai ambapo polisi waliwaua Waislamu kadhaa.
Pamoja na kutolewa kwa amri hiyo, Waislamu wameendelea na mihadhara yao ambapo mpaka sasa Wakristo zaidi ya 51 wameripotiwa kusilimu.
Aidha, Waislamu wameishutumu amri ya Mkuu wa Wilaya kwa kuiita kuwa ni ya "kidhalimu" na kuongeza kuwa hiyo ni sehemu ya mikakati ya Kanisa dhidi ya Uislamu ambayo walisema mara nyingi imekuwa ikitekelezwa kikamilifu na mawakala wake walio serikalini.
Shutuma hizo zinafuatia amri ya Kamanda wa Polisi Wilaya ya Temeke (SSP) Bw. Issaya Mngullu, kupitia barua yake Kumb. Na. TEM/C 13/4/Vol 11/100 ya Machi 11, 1999, inayoeleza kupigwa marufuku mihadhara ya wazi kwa zaidi ya siku mbili.
"Napenda kukufahamisheni kwamba uongozi wa Wilaya ya Temeke katika kikao chake kilichofanyika tarehe 10/3/1999 kimepiga marufuku kufanya mihadhara/mikutano ya dini zaidi ya siku mbili katika eneo/uwanja mmoja, pia isizidi saa 12.00 za jioni. Hivyo ninawashauri kuomba kwa siku mbili tu aidha mkitaka mfanye kwenye nyumba za kuabudia", alisema Bw. Mngullu kupitia barua yake hiyo kwa Katibu wa Khidmat Da’awat Islamia, Ustadh M. Ngubege.
Mapema akiwahutubia maelfu ya waumini katika muhadhara uliomalizika hivi karibuni katika uwanja ulio jirani na shule ya sekondari ya Nurulyakin, maeneo ya Mwembe- Yanga, Temeke - Yombo, Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kituo cha Kiislamu cha Khidmat Da’awah, Ustadh Magezi Shabani, pamoja na kuwatangazia waumini azma ya kumpandisha kizimbani mkuu wa wilaya, aliutahadharisha uongozi huo wa wilaya ya Temeke uache mara moja mpango wake wa kuiandama mihadhara ya Waislamu hatua ambayo Ustadh huyo aliita kuwa ni "sehemu ya uongozi huo kutekeleza kazi za Kanisa kwa kivuli cha serikali".
Alisema uongozi huo unafahamu fika kuwa si uongozi wa wilaya tu bali hata uongozi wa mkoa pia kisheria hauna mamlaka yoyote ya kutoa vibali kuruhusu kufanyika kwa mihadhara ya dini au kuifungia.
Ustadh Magezi aliongeza kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge la Jamhuri ya Muungano waumini wanaagizwa tu kutoa taarifa polisi kuomba ulinzi katika mikutano yao ya dini na wala siyo kuomba tena ruhusa ya kuhubiri.
Alisema sheria hiyo imepitishwa kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 19 kifungu cha 1 na 2 kinachotoa uhuru wa kuabudu na kutangaza dini.
Kinyume na msimamo huo wa Katiba na sheria, Ustadh Magezi aliutaka uongozi huo uchague moja, ama uendelee na kazi za serikali kama ulivyoteuliwa au ujiuzulu mara moja serikali na ufanye rasmi shughuli za Kanisa.
"Kwani amri hiyo haiashirii isipokuwa viongozi wa serikali hapa wanafanya kazi za Kanisa ... na kwa hiyo ni lazima Mkuu huyu wa Wilaya tukamtundike mahakamani", alisema Ustadh Magezi huku akiungwa mkono na waumini wa dini mbalimbali waliofurika kwenye muhadhara huo.
Ustadh Magezi aliwataka waumini kupuuza amri hiyo na kuuonya uongozi huo kuacha fitina dhidi ya Waislamu ni sehemu kubwa ya wananchi walipa kodi ambazo hutumiwa kwa viongozi wote wa serikali kulipwa mishahara yao.
"Pamoja na hivyo, Waislamu tunasema iwapo zitatumika nguvu zozote kutunyima haki tutatumia nguvu kutetea haki hyo ... na watambue kuwa balaa lolote wakati mwingine haliondoki isipokuwa kwa balaa ... na sisi tunamwambia Mkuu huyo wa Wilaya kwa sasa tuko tayari kwa lolote", alisema Ustadh Magezi na kuongeza kuwa "kinachowakera watu hawa ni kule kusilimu makundi ya Wakristo".
Wakati huo huo, kituo cha Khidmat Da’awah kinaendelea na muhadhara wake katika Msikiti wa Hijra uliopo maeneo ya Mbagala Zakhem, Jijini Dar es Salaam.
Muhadhara huo unatarajiwa
kumalizika hapo Machi 24, mwaka huu. Taarifa za awali zimethibitisha kuwa
mama mmoja aliyekuwa muumini wa dhehebu la Katoliki alikuwa amerejea katika
Uislamu kupitia muhadhara huo.
|
|