Aliyedai kutekwa nyara:
 
Adaiwa kuwa ni kachero wa CCM
Na Mwandishi Wetu, Mwanza

ALIYEWAHI kuwa Mwakilishi wa CUF Jimbo la Mkunazini Salim Msabaha amewachanganya Waislamu Mwanza hali iliyowafanya wamtuhumu kuwa anatumiwa na CCM kuwaparaganya.

Aidha nasaha zimetolewa kwa Waislamu kote nchini kuchukua hadhari zao wanapotembelewa na watu wanaoibuka ghafla na kujijengea umaarufu hewa.

Tuhuma na nasaha hizo zimekuja kufuatia ziara ya Bw. Salim Msabaha Mkoani Mwanza ambapo alikutana na kuongea na Waislamu katika Misikiti kadhaa.

Akiongea katika Misikiti ya Tawfiq, Rufiji, Rawdha, Arafa na Msikiti Mkuu wa Ijumaa Bw. Msabaha aliwakilisha mada zilizokuwa muafaka kabisa na wakati huu sasa.

Mada hizo zilihusu umoja, mshikamano kati ya makundi, madhehebu na watu wa aqida tofauti kushirikiana katika mambo ya msingi wanayokubaliana wote.

Alitoa mfano wa kuwa na sehemu za huduma ya jamii, kuwa na uchumi imara, kuwa na viongozi waadilifu na kukubali kutofautiana na wakati huo huo kuvumiliana bila ya kutukanana na kupeana majina mabaya mabaya. Alisema mambo hayo ndiyo yanayopandikizwa na maadui zao ili kuwagawa na kuwaacha wakizidi kushutumiana bila ya kupanga mambo ya maendeleo.

Tofauti ilikuja alipogusa mambo ambayo yanawagusa Waislamu kama jamii kwa ujumla. Mambo hayo hasa ni siasa za Tanzania, haki za Waislamu na madai yao, kutochanganya dini na siasa, namna ya kuwakilisha madai yao serikalini na mjadala wa Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

Mada zote hizi hazikwisha au kujibiwa na mhusika. Mara nyingi alitoa madai kuwa katika hadhara kama hiyo hawezi kuzungumza mambo ya siasa, alisisitiza kuwa Waislamu wajishirikishe kwa wingi katika mambo ya siasa, lakini alipoulizwa yeye alikuwa na nafasi muhimu na ameipoteza bila ya maelezo ya kukinaisha toka kwake na ana mipango gani, hakujibu ila alisema asiingizwe kwenye mtego.

Alizusha maswali mengi alipodai kuwa hakuna haja ya kuendelea kulalamika na kuishia kufanya fujo, akitoa mfano akasema kadhia ya Mwembechai imeleta hasara ya mali na roho za watu kupotea na kudai kuwa watu wasiingilie mambo kwa jazba.

Maneno hayo ya Bw. Msabaha yameibua dhana miongoni mwa Waislamu kwamba huenda ametumiwa na vyombo vya CCM au Dola kuwavuruga Waislamu.

Alipoomba maoni ya wasikilizaji, aliulizwa nini Fat-wa ya waliouawa Mwembechai ambapo alijibu kuwa Mungu ndiye atakayeamua.

Katika kuzunguka kwake mjini Mwanza Bw. Msabaha alikuwa akichukuwa maoni ya Waislamu kuhusu masuala mbalimbali, jambo ambalo limewafanya waumini wajiulize anamuwakilisha nani? Je' ni Ansaar Sunna au Kamati ya Alhaj Madabida!

Kilichowachanganya zaidi Waislamu ni kule kupinga kwake hatua ya Waislamu kuzidi kuishinikiza serikali iyatizame na kuyafanyia kazi madai yao kwa kuleta hoja ya kuacha kulalamika na kutumia jazba.

Waislamu wengi mjini Mwanza waliongea na Mwandishi wa habari hizi wametoa nasaha kwa Waislamu wote nchini kuwa waangalifu katika kupokea mahubiri ya wanasiasa, kwani mara nyingi ni ya ulaghai.

Bw. Salim Msabaha akiwa Mwakilishi wa CUF jimbo la Mkunazini alidai kutaka kutekwa nyara (na vyombo vya dola - CCM) ambapo alikimbilia katika moja ya Balozi za nje nchini kutafuta hifadhi.

Hata hivyo, baadaye alikanusha tena "kutekwa nyara huko". Katika masiku ya hivi karibuni Bw. Msabaha amekuwa pamoja kisiasa na Mh. Naila Jidawi anayetuhumiwa kwenda kinyume na chama chake cha CUF.

Mara tu baada ya Waislamu kuuliwa Mwembechai, Bw. Msabaha ni miongoni mwa watu waliopata fursa kuongea katika Msikiti huo na ni wakati huo huo Waziri Ali Ameir akaibuka na hoja kwamba Mwembechai hakuna dini ila siasa.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook