WAUMINI Mkoani Kilimanjaro wameazimia kupambana na Bw. Rashid Malya wanayemtuhumu kuhujumu mali za Waislamu.
Katika hatua ya hivi karibuni, Waislamu hao kupitia kwa Mawakili wao wamemtaka Bw. Malya arejeshe fedha alizopokea kutoka Manispaa na kwa upande mwingine Manispaa wasiendelee kulipa fedha nyingine.
Waumini hao wanamtuhumu Bw. Malya aliye Katibu wa Bakwata (M) kwamba ameuza ukumbi wa mkutano wa Bakwata bila kufuata taratibu zozote zinazokubalika kisheria kufuatana na katiba na taratibu za Bakwata.
Kutokana na tuhuma hiyo, Bw. Malya ametakiwa kusitisha zoezi hilo mara moja vinginevyo anafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, Bw. Malya ametuhumiwa kwa udanganyifu au kughushi kumbukumbu za vikao.
Katika barua yake No.BMK/WMM/15/142 ya Machi 9, Bw. Malya alieleza kwamba kwa maelekezo ya Halmashauri Kuu ya Bakwata (M) Kamati ya Ulamaa ilimfuta kazi Katibu wa Wilaya Bw. Shaban Ali Mnyone.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu wameeleza kwamba; Halmashauri hiyo iliyokutana Machi 2, 1999 haikuwa na agenda yoyote ya kumjadili Bw. Shaabani.
Aidha ni katika kikao hicho ambapo Bw. Malya alikiri kupokea shilingi milioni 2 toka Halmashauri bila ya idhini ya kikao chochote cha Bakwata; na kwa ajili hiyo akatakiwa atatue mgogoro wake na Manispaa kama mtu binafsi kwani Bakwata hawajatoa idhini ya kuuza jengo.
Katika hatua nyingine Bw. Shabani Mnyone aliyeandikiwa barua ya kusimamishwa Ukatibu amedai kwamba; yeye bado ni Katibu kwani hakuna kikao chochote stahiki kilichopitisha uamuzi huo.
Katika mlolongo wa kadhia hii; Katibu wa Bakwata Bw. Malya ametoa onyo kwa uongozi wa Msikiti wa Riadha kwamba endapo hautafuata taratibu na matakwa ya Bakwata utang'olewa uwekwe uongozi mwingine.
Uongozi huo katika kujibu onyo hilo umesema kwamba utaendelea kupigania haki za Waislamu hata kama utang'olewa.
|
|