FIKRA ZANGU
 
Tuimarishe Misikiti
 

Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC, USA

KITU cha kwanza alichokifanya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) alipofika Madina, ilikuwa ni kujenga Msikiti. Haikuwa kujijengea nyumba yake ya kulala au kuishi. Na alipoijenga nyumba yake, ilikuwa ndani ya eneo la Msikiti huo. Hapa pana fundisho kwetu la umuhimu wa kuushughulikia Msikiti na kuishi karibu na maeneo ya Msikiti au kuwa na Msikiti katika maeneo yetu ya kuishi au kufanyia shughuli zetu za maisha.

Ilikuwa muhimu kwa Mtume wetu kuupata Msikiti kwa ajili ya Waislamu, kwa sababu ndani ya Msikiti kulifanyika mambo mazito manne:

Da'awa: Waislamu walijipatia elimu ya dini yao humo, ili wapate kuutekeleza Uislamu wao kwa ufasaha. Na vile vile waitumie elimu hiyo na hekima zao kuueneza Uislamu kwa wengine.

Ibada: Swala zote tano za fardhi na zile za sunnah, Waislamu walizifanyia Msikitini. Na hapa ndio Mtume (s.a.w.) anatufundisha umuhimu wa kuswali Misikitini kwa pamoja (jamaa). Faida zake ni ajra nikubwa zaidi, kuliko zikifanyiwa mahali pengine au majumbani mwetu ila kwa akinamama.

Dhikr: Ndani ya Msikiti Waislamu walitulia kufanya dhikr zao za kumhimidi Mola wao Subhanahu Wataala kwa unyenyekevu na utulivu kwa kiwango cha hali ya juu kabisa.

Mikutano: Msikitini ndipo mahali ambapo Waislamu walipokutania kila siku kutwa mara tano au zaidi, iwe nje yake au ndani yake. Hapo ndipo Mtume (s.a.w.) na masahaba zake pamoja na wafuasi wao walipokuwa wakipangia mikakati yao dhidi ya makafir. Msikitini ndipo palipokuwa panapangwa mbinu za maendeleo ya Uislamu na Waislamu wenyewe. Kazi hii ya nne, iliyokuwa ikifanyika Msikitini, kwa kifupi ilikuwa ni kuunusuru Uislamu na Waislamu.

Hivi ni baadhi ya vielelezo vya vitendo vya mpendwa Mtume wetu (s.a.w.) na ndiyo sunnah zenyewe hizo. Ni muhimu kwetu kufuata vitendo hivyo. Msikitini ndipo mahali pa kufanyiwa hayo na mengineyo yaliyo mema na mazuri ya kumpendeza Allah (s.w.)

Hali hii inatuonyesha utakatifu wa Msikiti na umuhimu wake. Msikiti si mahali pa kuchezewa. Mikutano ya Msikiti haihitaji kibali wala kiwango cha wahudhuriaji hakiwekwi. Wala hakuna ubaguzi wa wahudhuriaji. Waislamu wote ni ndugu.

Hii leo, Alhamdulillah Rabbil Alamina, Waislamu wa Tanzania wanaijaza Misikiti, siyo tu siku za Ijumaa, bali hata na siku zingine na karibu katika nyakati zote za swala. Lakini kutokana na maelezo ya hapo juu, ingefaa kama kila mmoja angejiuliza mwenyewe, kuwa zaidi ya kuhudhuria Msikitini kwa ibada ya swala, kuna jingine lolote la ziada linaloweza kumfikisha Msikitini?

Kwa mfano, kama vile kuufagia Msikiti, kuupamba Msikiti kwa kuufyekea majani, kuupaka rangi, kuzungumzia na kujadili kuwaendeleza Waislamu na watoto wao katika maeneo jirani na Msikiti huo. Na mengine mengi kama hayo.

Je, Msikiti una kamati mbalimbali za kushughulikia Msikiti huo? Kama hauna kwa nini? Mimi binafsi naweza kufanya nini ili kamati hizi ziwepo? Na kama zipo, mimi nitajihusisha vipi ili niweze kuchangia katika masuala ya ufanisi wa Waislamu na Uislamu?

Ni bora kwetu iwe tumechelewa kuanza kuyafanya hayo, kuliko kuyaacha kabisa. Ikiwa bado hatujafanya hivyo, basi bora kuyaanza hivi sasa. Na ikiwa tunayafanya hayo, basi nashauri ni vizuri hivi sasa tuyavalie njuga na kujizatiti katika shughuli za Misikitini. Shughuli ambazo malipo yake anayajua Yeye Mwenyewe Subhanahu Wataala.

Katika kuyafanya haya Waislamu tunahitaji viongozi. Viongozi wenye taqwa, walioushiba Uislamu, wenye uzoefu na ujuzi waliobobea katika taaluma za kiutawala wa haki, uongozaji uliozingatia lengo na utekelezaji wa dhati unao mukhofu Allah (s.w.).

Hivi sasa tumepata bahati, tuna Waislamu wengi miongoni mwetu, wenye elimu ya kutosha katika masuala ya elimu tunayoiita ya kidini na ile ambayo tunayoiita si ya dini na pia tunao wale ambao wamejaaliwa kupata moja tu kati ya hizo mbili.

Wote hawa wanahitajika katika uongozi wa uendeshaji na uendelezaji wa Misikiti, hali kadhalika na uongozaji na uendelezaji wa Waislamu na Uislamu kwa jumla. Kila mmoja wao ana sehemu yake na nafsi yake katika kufanikisha lengo la kuunusuru Uislamu na Waislamu wenyewe.

Ili tuweze kujiendeleza na kuuendeleza Uislamu, tunahitaji viongozi wenye kumtanguliza Allah (s.w.) mbele yao, bila ya kumwogopa mtu mwingine au kitu kingine. Wawe wenye kushirikiana, ushirikiano utakaowafanya Waislamu wanaowaongoza nao kushirikiana kati yao wenyewe kwa wenyewe, na vile vile pamoja na viongozi wao.

Viongozi wa aina hii ya pili wanaohitajika ni wale Waislamu waliomo na watakaokuwemo katika ufalme wa kisiasa, katika taasisi mbalimbali za Kiislamu, katika vyama mbalimbali vya kisiasa na katika serikali zote tangu ile ya kata, kijiji, mji, wilaya, mkoa mpaka ile ya ngazi ya kitaifa. Hawa ndio tegemeo letu katika kuunusuru Uislamu na Waislamu hapa duniani katika maisha yetu ya kila siku. Hatuhitaji hapa waropokaji, waoga wa binadamu wenzao na wateteaji matumbo yao na vyeo vyao.

Ni dhahiri kuwa iko haja ya kuwa na viongozi wa Kiislamu katika jamaa ya Kiislamu nchini mwetu Tanzania.

Ingawa idadi ya Waislamu walilochaguliwa kushika vyombo mbalimbali vya dola, ilikuwa bado ndogo sana, na kuwa haikulingana na uwiano wa wingi wetu kwa jumla, lakini tuliona kuwa huo ulikuwa ni mwanzo mzuri katika kutuletea na kutulindia maendeleo na maslahi yetu kidini na kidunia.

Tulijionea raha mioyoni mwetu kuwaona viongozi wetu wa Kiislamu wakiingia kwa wingi Misikitini, huku wamevalia kanzu zao, vibaraghashia vichwani mwao, wakiswali pamoja nasi, kwa utulivu, unyenyekevu na kujisalimisha mbele ya Mola wao na wetu (s.w.). Huo ni mfano mzuri kwetu tunaoongozwa nao.

La kusikitisha ni kuwa wengi wa viongozi wetu hawa hunyamazia kimya wakati Waislamu wanapopata misiba kama ule wa Mwembechai na mingineyo. Wale wachache wanaothubutu kusema, ukiyasikia wasemayo hutadhani kuwa wao ni Waislamu. Viongozi wa aina hii kwa hakika hatuna haja nao. Hatuna budi kuwashughulikia wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Lazima tutambue kuwa ni bahati kubwa sana mtu kuwa Muislamu. Ni mjaala kutoka Kwake Mwenyewe Rahmani. Uislamu ni mfumo mzima wa maisha ya BinAdam. Uislamu huishii katika kuswali peke yake, wala haukamiliki kwa swala pekee. Ingawa swala imepewa uzito mkubwa sana kuliko ibada zote, ibada katika Uislamu, huendelea wakati wote katika kila BinAdam anachofikiri, kila anachosema na kila anachotenda. Yote hayo yatimizwe kwa dhamira ya kumpendeza na kumweka Allah (s.w.) mbele na juu ya yote na vyote.

Waislamu nchini kote Tanzania tumekuwa na malalamiko chungu mzima dhidi ya serikali yetu. Malalamiko hayo yametokana na dhahma za makusudi tunazofanyiwa kwa kunyimwa haki sawa na raia wenzetu ambao hawajapata bakhti ya kuwa Waislamu. Tunanyanyaswa, tunadharauliwa na kupuuzwa mno, kiasi cha kulalamika.

Katika hali kama hii, tunahitaji sana kusimama kidete ili kuunusuru Uislamu na hali kadhalika Waislamu wenyewe. Ni jambo la kufurahisha na kujivunia, kumuona kiongozi jasiri wa Kiislamu, Mheshimiwa Kitwana Kondo, akijitokeza katika zoezi hili. Anachokifanya KK ndicho kiitwacho Jihad. Na malipo yake anayajua Allah (s.w.). Tunakushukuru na kukupongeza KK kwa ujasiri wako. Siku zote tutakuwa pamoja nawe na tutakupa ushirikiriano wetu ulio thabiti na Insha-Allah ufanisi utakuwa wetu na kwetu.

Inatusikitisha kuona kuwa viongozi wengine wa Kiislamu wamekuwa kimya. Hawamuungi mkono katika usemaji wala utendaji. Wanaogopa kupoteza kula yao. Wamesahau kuwa umoja ni nguvu. Viongozi wa Kiislamu wanatakiwa kuwa pamoja na kuwa na sauti moja ili tuweze kupata tahfifu tuitafutayo,

Je, viongozi wa Uislamu na wale wa Kiislamu mpo? Au tutafute viongozi wengine? Kazi kwenu!
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook