MAKALA
 
Silika ya kumjua Muumba - 2
 

TUMEONA kuwa mwanaadamu huzaliwa na fitra na kwamba umbile lake limetofautiana na viumbe vingine. Halikadhalika tumeona kuwa fitra ni mwanga unaohitaji mwongozaji. Katika sehemu hii tutaangalia kwa kifupi hoja kuhusiana na Mungu Muumba. Kwa kifupi hoja zitolewazo juu ya Mungu Muumba ziko nyingi na staili tofauti, hata hivyo zaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu.

Kundi la kwanza ni zile hoja zenye kuegemea kuyatafiti maumbile na mazingira kwa ujumla. Hoja au dalili hizi humwezesha mtafiti kugundua kwamba kuwepo kwa dizaini tofauti za maumbile, busara za kiumbaji, lengo na mpango ulio na mfungamano (coherence) wenye kutegemeana na umakini wa ajabu, kwahitaji kuwepo Muumbaji na mpangaji hodari wa maumbile. Kuhusiana na hoja hizi za maumbile mmoja wa wanachuoni maarufu wa taaluma ya sayansi ameeleza kirefu katika moja ya maandiko yake kwamba:

"Hebu na tuangalie mfano wa macho ya viumbe vyote yalivyo. Macho yanatabia ya kupitisha mwangaza ndani yake (yaani jicho lote zima lina uwezo wa kupitisha mwanga ndani yake) na ni sehemu hii tu katika mwili ipitishayo mwanga. Sehemu ya nje kuna ngozi ngumu inayoruhusu mwangaza kupita na baadae pana ute (umaji maji mzito) ambapo baina yao pana kioo chembamba na kiini - yote haya yamekusanywa pamoja na kutoa umbo la jicho kama tuliaonavyo, ambalo hufanyakazi ya kuona katika namna ambayo msanii yeyote hawezi kulirekebisha au kuliunda. Je, hivi n kweli kuwa muundo huu wa jicho ni matokeo ya bahati tu? Yaani tuseme ilisadifu tu kuwa jicho liliumbwa vile bila ya kujua awali kuwa kuna mwangaza na kujua tabia ya mwangaza na hivyo ikanasibisha macho katika hali ya kuweza kuutumia mwangaza huo katika kuona?"

Hoja za namna hii mara nyingi husaidia kuamsha mwanga asilia (fitra) alionao mwanaadamu juu ya Muumba.

Kundi la pili ni hoja pinzani dhidi ya kuwepo Muumba. Hoja hizi ni zile zitolewazo kuonyesha kutohitajika Muumba, yaani kwakuwa ulimwengu umekuwa na silka ya kujiendesha wenyewe na kwa kuwa mwanaadamu amejikuta kuwa na akili ya kujitambua mwenyewe na mazingira yake sambamba na uwezo wa kuyatumia kwa manufaa yake, basi suala la kuwepo Muumba halina umuhimu wowote kwake!

Katika kuboresha hoja hii kumebuniwa nadharia maalum. Nadharia ya Evolution kwa mfano inadai:

• Mwanaadamu amefikia umbile hili baada ya kupita mabadiliko ya maelfu ya miaka kutoka hali ya ufu (kutokuwa hai).

Mwanadamu ni mnyama; mahitaji yake pamoja na lengo lake yanathibitisha kuwa yeye ni mnyama. Nishati aliyonayo imetokana na silika hiyo ya unyama aliyorithi toka kwa wahenga wake wa zama za uhayawani (Homosapiens).

• Hapana fitra (guiding light), wala dhamiri, kanuni za kimaadili, ukweli, uadilifu, hisani, wema wala kumcha Mungu, hana hisia zozote alizopandikizwa katika umbile lake. Hakuna Mungu, roho, maisha ya baada ya kifo wala ufunuo. Mitume ni wakereketwa, wahuishaji wa jamii. Hawakufunuliwa chochote hivyo dini zote ni uwongo mtupu.

Mmoja wa 'magwiji' wa nadharia hii amethubutu kudai kwamba "Mungu (Muumba) hana nafasi katika 'Evolusheni'. Ardhi na wakazi wake wote hawakuumbwa, bali wameibuka".

• Kwa kuwa mwanaadamu ametokana na mabadiliko hayo ya muda mrefu asiyewajibika kwa yeyote wala hapana uwezekano wa kuweza kuishi baada ya kufa, yuko huru kutenda atakavyo. Anapaswa kuyaendea mambo jinsi yalivyo, hana vikwazo vya kijamii, hana mfumo wa maadili wala muongozo wa dini unaopaswa kukwaza matashi na uhuru wake wa kutenda atakavyo.

Kama ilivyoelezwa katika makala yaliyopita nadharia hii imekuwa kichocheo kikubwa cha harakati za kinyama zinazofanywa na wanaadamu ulimwengu wa hivi leo unaoitwa wa "sayansi na teknolojia".

Kundi la tatu ni zile hoja za wanafalsafa wanaojaribu kuyaangalia mambo kwa urazini.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook