MAKALA
 
Umoja wa walimwengu wote

Na Tahir Kajia

Tuwaulize Wairani, tuwaulize Wasaudia; kulikoni? Jambo hili mwalijua? Au nasi tumekuwa kama Rais wa Misri (3:11) Enzi ya Nabii Musa ambaye alijivuna (28:39) kwa maana alifanya munkar (16:22) (alikataa Uungu pekee mmoja) na akajipachika yeye, hivyo akanadi: "Enyi Wakuu! Simjui kwa ajili yenu mungu asiyekuwa Mimi..." (28:38).

MHADHIRI Masoud wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisikika akilalama akisema: "Mungu wa Wazungu anaakili zaidi kuliko Mungu wa Waafrika". Wanafunzi wake walitaka kutokwa na akili. Vipi Mhadhiri? Ni kwamba hajui kuwa Mungu ni mmoja? Iweje awepo Mungu wa Wazungu na Mungu wa Waafrika?

Ili nasi tupate mafao na mjadala huu haiyumkini tuwe waangalifu sana. Kwa sababu maneno haya yamesemwa na mtu msomi. Msomi ambaye Allah amewasifu akisema: "Kwa hakika wanaomuogopa Allah miongoni mwa waja wake ni wale watalaamu". (35:28)

Tuelekee kwenye kamusi ya Kiswahili sanifu, neno Mungu maana yake ni - Chochote kile ambacho binadamu atakiabudu akitarajia kwamba kitamsaidia kutatua matatizo yake.

Kwa tafsiri hii, mjue Masoud ndugu yetu kuwa kasema wanaoabudiwa na Wazungu wana akili zaidi kuliko wale wanaoabudiwa na Waafrika.

Tuelekee tena kwenye kamusi ya Kiswahili sanifu, neno abudu (kd) maana yake ni - kuogopa, kuomba, kuenda kupita kiasi, kuheshimu, kutumikia n.k.

Kwa tafsiri hii, tumuelewe ndugu yetu Masoud kuwa yeye kasema: Wale wanaoogopwa na kuheshimiwa na kuombwa na kupendwa kupita kiasi na kutumikiwa na Wazungu, wana akili kuliko wanaoombwa na kuogopwa na kuheshimiwa na kupendwa kupita kiasi na Waafrika, wote hao wakitarajiwa na watu wao kuwa watawasaidia kutatua matatizo yao. Basi hao wanoogopwa n.k. kamusi inatufahamisha kuwa ni miungu.

Mhadhiri kasema kweli. Na ni ukweli huu tunataka tuudadisi. Ni nani hao miungu ya Wazungu na nani hao ni miungu ya Waafrika.

Waungu

Bum! Bum! Bum! Magoma ya watu weusi yanalia. Na kweli ni mlio huu ndio iliyokuwa adhana ya mababu zetu pale Qibla chao kilipokuwa ni mapango na au misitu.

Bum! Bum! Bum Bara la watu weusi linatikisika. Sisi wajukuu wa mababu waliotolewa katika kibla chetu na kuelekezwa katika maofisi ya vyama na serikali; jambo gani limetufika, mbona tuko hoi? Sisi nchi zetu zimejaa mali nyingi. Lakini tunaitwa nchi masikitini. Na kweli njaa iko mlangoni saa zote. Usiombe kupita mijini, wanawake wako uchi wa kinyama (20:118). Tii kiu yako ndiyo lugha ya mabango. Hata maji sasa ni biashara. Majasho, ni kwa sababu ya joto lisilo la kawaida (20:119).

Bum! Bum! Bum! Wana wa Afrika wanalia; kulikoni? Viongozi kibao. Ukigeuka kwenye majumba yao kuanzia balozi wa nyumba kumi, Mwenyekiti wa Kijiji, Katibu wa Kijiji, Katibu Kata, Katibu Tarafa, Diwani, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, Mawaziri na mpaka Rais mwenyewe. Bila kuwasahau Wabunge, Wakuu wa Majeshi, Wakuu wa Mashirika, Mahakimu na Majaji wewe taja tu. Na ukija kwenye nyumba za Mungu huwakosi Mamufti, Masheikh, Maaskofu, Wainjilisti, wewe taja tu. Mradi viongozi kibao. Na wote hawa Mwenyezi Mungu majina haya hakuyatolea dalili. Ni majina tulioyapanga sisi na baba zetu (12:40).

Gundua kwamba mababu zetu hawakuwa na viongozi wenye majina haya. Wao kiongozi wao waliyemuogopa ni Mwenyezi Mungu peke yake. Aliyefuatia kwake alikuwa ni mzazi kama ambavyo maneno yake yanavyotuwekea wazi: "Mola wako amehukumu kuwa msimuabudu (tazama kamusi maana ya neno abudu) yeyote ila Yeye tu na kuwafanyia wema wazazi." (17:23)

Sisi leo je! Adhana yetu sio ving’ora na vimulimuli! Mara utatuona tumepanga safu pembeni ya barabara tukimdhukuru kwa kutaja jina la huyo anayepita na gari lenye bendera. Na hiyo kumbe ndio sala yetu - makofi na vifijo (8:35).

Mola wetu anatujaza nini juu ya hawa tunaowaenzi? Si jingine tunalofanya, bali anasema: "Wao wameshika waungu wengine badala yake...!" (42:9). Ni kwamba hatujui ni nani Mola (Mfalme au Kiongozi au Rais au Mwenyekiti) wa mbingu na ardhi? Hivyo (tunafanya 15:96) viongozi wengine badala Yake ambao hawamiliki kwa ajili ya nafsi zao nafuu wala dhara (13:16).

Akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake, sisi huchukia (utaambiwa ondoa udini hapa). Na wanapotajwa (viongozi wao waliowapigia kura) walio kinyume Naye, si makofi hayo na vigelegele. Na gari kusukumwa, furaha tele - meno nje nje (39:45).

Wasomi wetu waliohitimu katika vyuo vikuu na watawa kumbe ndio tuliowafanya washirika wa Allah (9:31). Kwa maana viongozi wetu wa ngazi za juu, Marais, Mawaziri, Wabunge, Majaji, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi Wakuu, Masheikh, Mapadri, wote hao ndio tuliowafanya waungu badala ya Allah. Na ni kweli kwa sababu wanaloamrisha ndilo tunalolifanya. Allah anatuitia katika njia iliyonyooka (10:25) nao ndio Uislamu (6:126). Lakini hao viongozi wetu hutuitia njia ya demokrasia, ukafiri (3:100).

Hivyo wametuwekea dini asiyoitolea ruhusa Allah (42:21). Na hawa viongozi wetu ni wahitimu katika vyuo vikuu. Tujiulize, Je! hivi vyuo vikuu ni nani muasisi wake na ni vya nani? Tukijibu swali hili tutamuelewa Profesa Masoud vyema. Kwani alipoulizwa ni kwa nini unasema waungu wa Wazungu wana akili zaidi ya waungu wa Waafrika? Alisema: "Wao Wazungu, waungu wao wamewalundikia milima ya minofu ya nyama hata wasipofanya kazi watakula na kusaza. Lakini waungu wetu unga wa manjano ni mpaka tukawaombe wazungu".

Bila digrii huwezi kuwa kiongozi. Na digrii hii utaipata kwa Wazungu tu. Kumbe waungu wetu (viongozi wetu), waalimu wao ni Wazungu! Je! Mwalimu si ana akili kuliko mwanafunzi wake? Masoud kasema kweli. Ni kwa mafunzo yao hayo mali inatoka kwetu kwenda kwa Wazungu kwa kasi kubwa ajabu, pia kwa gharama zetu. Nchi zao ambazo ni masikini, hawana madini, wala mafuta, wala mbao, wala wanyama, wala maeneo ya kilimo, wamebanana, vijinchi vidogo, lakini wamejijengea viwanda na sisi kupitia kwa wanafunzi wao (viongozi wetu) tumefanywa masoko.

Hivyo wao hujiita nchi tajiri na viongozi wetu kasumba hiyo wameikubali. Lakini mambo sio marahisi hivyo. Ili sisi kuweza kupata mazao yanayotoka viwandani mwao ambayo huliwa na kutu, viongozi (miungu) wetu wamefundishwa kikamilifu jinsi ya kuendesha mradi wa Wazungu (serikali) wakiusimamia vilivyo.

Kwa hiyo, sisi wenyewe kwa gharama zetu hukusanya madini yetu, ng’ombe wetu, mbao zetu, mazao ya mashambani n.k., vitu visivyoliwa na kutu tukivisafirisha kwa gharama zetu mpaka Ulaya. Kwa kubadilishana na vitu vya anasa na mapambo, basi! Kumbe hivyo gharama yote ya maisha ya Wazungu na faida yao na pia starehe zao, tunabeba sisi. Kwao shida sio kuwa mtu atakula nini, bali ni uroda gani hajauonja auendee. Ndio maana mtu anatoka kwao kwa mamilioni ya fedha kuja Afrika akaangalie mijusi. Eti ikaitwa utalii. Wanafaidi bure hawa. Na idara ya serikali (mradi wa Wazungu) ikaundwa - Wizara ya Utalii inaitwa.

Mradi wa Wazungu

Berlin Conference awamu ya kwanza ilikuwa kuigawa Afrika na kuifanya makoloni yake. Humo kupitia Makanisa wakatayarisha ndugu zao katika dini na kuwachomeka katika mradi wao (serikali). Wakati huo kama jina lako halikuwa John, darasa la tano hukuruhusiwa kuingia. Kwa hiyo mwaka 1957 ili ugombee Ubunge iliwekwa sharti uwe umefika darasa la sita na una dola 50 benki. Vitu ambavyo wale waliokuwa Waislamu walikuwa hawana.

Berlin Conference awamu ya pili waliwasimika wahitimu wao kutoka katika vyuo vikuu (miungu 9:31) kuendesha serikali kama walivyokuwa wameiasisi. Mambo yakawa hivi:

Kwa dhulma yao hao Mayahudi walituharamishia vitu vizuri tulivyohalalishiwa, wakazuilia watu wengi na njia ya Allah. Tukawa sasa tunalishwa riba na kula mali sasa kwa njia za batili. (4:160-161)

Tunaposema mradi wa Wazungu elewa kinachosemwa hapo ni serikali (sera na siri na kali). Mradi huu sera zake ni:

Udhalimu. Na ni nini kitakujulisha hata ukajua ni nini huo udhalimu? Udhalimu ni kuukurubia ule mti (2:35). Na neno hili mti Allah ametupigia mfano tu. (14:25). Mti maana yake ni "Neno" (14:26) Kwa hiyo udhalimu ni kukurubia neno (kauli).

Sasa ni kauli gani hiyo ambayo ukiikurubia unakuwa dhalimu? Dhalimu unayeonywa usimkaribie ambaye Mwenyezi Mungu anatupigia mfano kwa kumuita "mti" ni yule atakayesema miongoni mwetu: "Mimi ni mungu (kiongozi au mfalme au Rais) badala Yake, (kwani) huyo ni dhalimu (21:29). Kwa tafsiri hii adhimu, tumeachwa hoi. Kwani wao Wazungu wamepotosha tafsiri wakisema kuukurubia uwongo wao ule ni kuzini Adamu na Hawa. Naye Allah kawafichua uwongo wao (2:35) kwani wao Adamu waliingia bustanini kama mume na mke.

Hivyo madhalimu ni watu wanaomtii binadamu mwenzao mungu waliomteua kuwa kiongozi wao. Na hapa nini tujue?

Itaendelea toleo lijalo
 
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook