MAKALA
 
Kumbukumbu zangu juu ya Bosnia, Chechnya na hivi karibuni Kossovo
 

VYOMBO vya habari vya ndani na vya nje vilikuwa vinatutangazia na kutuonyesha vita vya Bosnia jana. Vita hivyo vilihusisha Waislamu, Wakorati na Wasebia. Wakorati ni wafuasi wa dhehebu la Kanisa Katoliki na mwanzo mwa vita hivyo walisaidiwa sana na serikali ya Crotia chini ya uongozi wa Rais Franjo Tojman kuwashambulia Waislamu.

Wasebia pia walipewa misaada ya hali na mali na serikali ya Serbia chini ya uongozi wa Rais Slobodan Milosovic dhidi ya Waislamu. Kutokana na hali hiyo Waislamu walijikuta hawana pa kukimbilia wala pa kutokea, bali kupambana kimbinu dhidi ya maadui hao wawili ambao wote kwa upande mmoja ni Wakristo wa Kanisa la Roma, na upande mwingine Wakristo wa dhehebu la Orthodox.

Baadaye Waislamu wakaungana na Wakorati. Katika vita hivyo vya Bosnia, Waserbia waliwauwa kikatili Waislamu na Wakoroti au katika kambi maalum za mateso. Hivi ni nani aliyewasha 'moto' huo wa mauaji hayo?

Rais wa Serbia, Slobodan Milosovic, yeye ndiye aliyewasha 'moto' huo akimsaidia katili mkubwa wa ubinadamu na binadamu wa Bosnia, Ratko Mladic na wafuasi wake. Lengo kuu la Maderbia hawa ilikuwa ni kupanua mipaka na kuunda dola kubwa ya Serbia. Waserbia hawakuwa peke yao katika lengo lao kuu.

Nchi kama Ugiriki, Urusi, Bulgaria, Australia na Slovinia ziliwasaidia. Hali hii iliwawesha Waserbia kumiliki au kuteka karibu asilimia sabini ya ardhi ya Bosnia na wakawafanya Waislamu na Wakorati wengi kuwa wakimbizi katika nchi za Ulaya.

Umoja wa Mataifa kama kawaida yake ni umjoa wa maneno matupu. Katika vikao vyake mbali alijitahidi sana kulaani vitendo vilivyotokea Bosnia, na huku Waserbia wakiendelea kufanya ukatili wao dhidi ya Waislamu na Wakorati mithili ya ukatili ule uliyofanywa na majeshi ya Hitler dhidi ya Wayahudi. Umoja wa Mataifa ndiyo iliyozuia Waislamu wa Bosnia wasipate silaha kwa madai kuwa wakipata silaha vita vya Bosnia vitakuwa vikali mno.

Serikali ya Amerika na baadhi ya nchi za Ulaya walikuwa wanafuatilia kwa makini maendeleo ya vita hivyo, na huku wakiweka kando uadilifu na haki za binadamu. Pia NATO iliendelea kutoa vitisho dhidi ya Waserbia kwa kuanzisha mashambulizi makali. Amerika na nchi za Ulaya hawakuwa na sera nzuri ya mambo ya nchi za nje kuhusiana na Bosnia ndiyo maana Waserbia wakawa vichwa vikubwa na vigumu.

Pamoja na upungufu huo uliojitokeza, Amerika na washirika wake wa nchi za Ulaya walifanikiwa kuwakutanisha kwa mara ya mwisho, viongozi wa Waserb kwa upande mmoja, na viongozi wa Waislamu na Wakorati, katika mji wa Deyton, Serikali, ili waweze kujadili matatizo yao kinaga ubaga.

Mazungumzo ya Deyton yalimaliza vita vya Bosnia na mkataba wa Deyton ukapitishwa. Mkataba huo umewapatia Waislamu na Wakorati asili mia arobaini ya ardhi na baki ya asili mia sitini umebaki kwa Waserbia. Pamoja na mkataba huo wa kisiasa, bado yapo matatizo mengi ya kisiasa na kijamii. Na majeshi ya NATO ndiyo yanayosimamia utekelezaji wa mkataba wa Deyton nchini Bosnia.

Historia inatuonyesha dhahiri kuwa Bosnia imepita katika kipindi kigumu, hususan kipindi cha vita vikuu vya kwanza vya dunia vilivyoanza mwaka wa Kirumi 1914 mpaka 1918. Na kwa ujumla katika utawala wa kiimla wa Hayati Rais Tito.

Watu wenye fikra huru na wenye kufuatilia historia, walikuwa wanajiuliza baada ya Bosnia kitafuata nini?

Vita katika Jamhuri ya Chechnya huko Urusi, ilizuka baada ya ile ya Bosnia. Wakazi wengi wa Chechnya ni Waislamu na utajiri wao ni mafuta. Waislamu waliamua kuanzisha vita hivyo dhidi ya serikali ya Russia, baada ya kuchoshwa na udhalimu mkubwa wa Warusi.

Warusi walitumia silaha kali katika vita hivyo ambazo zilileta uharibifu wa mali na maisha ya watu katika miji, vijiji mbalimbali vya Waislamu. Hawakujali hata kidogo haki za binadamu katika mapigano. Waislamu wa Chechnya hawakuwa na nguvu kubwa kuliko majeshi yaliyotumwa vitani na serikali ya Urusi.

Pamoja na nguvu zao, Waislamu wa Chechnya waliwashinda Warusi. Ushindi huu uliwashangaza walimwengu walio wengi, ambao wamejisahau na kuwepo na Mwenyezi Mungu. Ni kwamba Mwenyezi Mungu huwasaidia sana watu wanaopigana kuondoa dhulma na kusimamisha haki na uadilifu katika ardhi.

Pia Warusi hawakuwa peke yao katika vita hivyo. Walikuwa wanabadilishana habari za siri na za kivita na serikali ya Amerika, haswa katika kumsaka kiongozi wa Chechnya, Dudayev.

Kiongozi huyo aliuawa kutokana na mbinu fulani ya serikali ya Amerika iliyoitumia. Hili halikuwakatisha tamaa Waislamu wa Chechnya, bali waliimarika na wakajipanga sawasawa dhidi ya adui wao. Ingawaje hali ya kisiasa nchini Chechnya ni shwari, lakini Urusi sasa anapika mambo ili siku moja Jamhuri hiyo ianguke tena mikononi mwake. Vivyo hivyo Amerika na baadhi ya nchk za Ulaya. Baadae watu wenye kutafakari dunia inakwenda wapi na inatoka wapi, wakawa na swali linalosumbua mbongo zao, nalo ni baada ya Chechnya kitafuata nini?

Sasa kuna vita Kossovo, jimbo ndani ya Serbia. Kwanza, wakazi wengi wa Kossovo ni Waislamu. Lakini bahati mbaya vyombo vya habari vya dunia haviwatangazi hivyo, bali hutangaza kuwa ni Waalbania. Huu ni upotoshaji wa habari na kuficha ukweli.

Rais Milosovic ndiye anayetuma majeshi yenye silaha kali na kisasa kuwapiga Waislamu kwa kisingizio kuwa anawapiga wanajeshi 'waasi' wa jeshi la ukombozi wa Kossovo. Miji ya Waislamu au vijiji vyao vimewashwa moto na kuangamizwa. Waislamu walio wengi wamekimbia miji au vijiji vyao na sasa wanaishi kama wakimbizi katika nchi za nje.

Kwa nini atafute visingizio? Alilonalo ni chuki tu dhidi ya Waislamu na anataka kuhakikisha tu kwamba watu wote wanawekwa, watake, wasitake chini ya himaya ya Waserbia na Ukristo wa Orhtodox. Ni nani anayewapa nguvu Waserbia? Warusi wanawasaidia kwa sababu Waserbia ni ndugu zao katika imani ya Kikristo ya Kiorthodox; na ni ndugu zao wa damu.

Ni kweli isiyoweza kupingika kuwa Kossovo ilikuwa na utawala wake wa ndani. Lakini Rais Milosovic aliufuta utawala huo wa ndani katika mwaka 1984 kufuatia kufa kwa sera za Kikomonisti nchini Yugoslavia. Hatua hii ilifuatiwa na ugandamizaji wa Waislamu. Alama kuu ya kupinga ugandamizaji huo ni Waislamu kuunda jeshi la ukombozi wa Kossovo.

Vita vya Kossovo vimekwishagharimu maisha ya watu zaidi ya elfu mbili, Misikiti na mali nyingine nyingi kuteketezwa. Amerika na nchi za Ulaya haziridhiki na hali ya matokeo yanayotokea nchini Kossovo. Wameandaa "mkataba" wa amani unaowahusisha makundi mawili yanayopingana huko. Kwa mara ya kwanza, walifanikiwa kuwakutanisha huko Ufaransa katika mji wa Rambullel kwa muda wa wiki mbili.

Wakati mazungumzo hayo yalipokuwa yanaendelea, Amerika na nchi za Ulaya zinazounda shirika la kijeshi la NATO walimshinikiza Rais Milosovi kukubali makubaliano, vinginevyo atapigwa. Vitisho hivyo havikuzaa matunda na bado Rais huyo akaendelea kukaidi kupelekwa kwa NATO Kossovo. Pamoja na yote, mazungumzo ya Rambullel kwa meza ya kwanza ya mazungumzo, hayakufanikiwa hata kidogo. Baadae nchi za Amerika na Ulaya zikatamka kuwa sasa NATO haitamshambulia, kwa sababu mazungumzo ya Rambullel yameweka misingi ya mafaniniko ya baadae ya kuleta amani. Amani gani? Bado majeshi ya Serbia yanaendelea kuua na kuchoma moto miji na vijiji vya Waislamu. Amani gani, wakati wanawake wenye mimba wa Kiislamu wanalazimika kujifungua au kuharibu mimba majiani katika harakati zao za kutafuta usalama wa maisha yao.

Hivi sasa mkutano wa pili, uliyoanza Machi 13, 1999 nchini Ufaransa wa kutafuta amani sina uhakika kwamba utaleta amani ya kweli. Hii ni kwa sababu nchi za Ulaya na Amerika zinatumia vitisho na shinikizo kutafuta makubaliano kati ya makundi mawili. Labda ingalikuwa busara kutafuta njia muafaka itakayopunguza mvutano na uhasama kati yao. Vinginevyo ni kujenga misingi ya udanganyifu kwa suala zima la Kossovo.

Pia nchi za Magharibi na Kaskazini ya Ulaya zielewe kuwa haki na batili ni vitu visivyochanyika na vyote vikazamishwa, kimoja ambacho ni haki kuibuka na kushinda. Ifahamike kuwa hawataacha tabia yao ya kuchanganya haki na batili katika masuala mbalimbali, haswa yanayohusu watu. Kwa nini iwe hivyo? Kwa sababu wanatumia vitabu visivyokuwa na nuru. Mambo yote yanayohusu maisha ya watu, ni ya Mwenyezi Mungu, hivyo hayawezi kuendeshwa kwa njia kama hizi za vitabu vinavyotokana na fikra za mwanaadamu.

Waislamu wakati umefika wa kuumba hali itakayoleta mapinduzi ya nguvu katika uongozi wa dunia. Pia tuwe tayari kwa hali na mali kuangamiza kabisa hatari za wadhalimu na watenda mabaya ili kuweza kuitakasa jamii. Pia tuwe na mpango wa makusudi utakaohakikisha kuwa uongozi uwe mikononi mwa wacha Mungu, wafanyao mema au wanaomuogopa Mwenyezi Mungu.

Ni jambo la kusikitisha kwamba Waislamu na wasiokuwa Waislamu wanapuuza umuhimu wa kazi hii, ambayo iko mbele yetu. Waislamu wanaiangalia kazi hii kama ni mpango wa kisiasa na hawaelewi thamani ya lengo la Uislamu kufuatana na mtazamo wa Qur'an na Hadith.

Wasio Waislamu, baadhi yao wana fikra zisizokuwa na uhakika. Wengine wanapuuza, hawaamini kwamba uongozi wa mabaya na waovu ndiyo mama wa mabaya yote yanayosababisha ubinadamu leo kutabika na kwamba ustawi wa watu unategemea sana kuwepo kwa viongozi wacha Mungu na wanaomwoga Mwenyezi Mungu.

Hii leo ulimwengu unatawaliwa na wanao mkana Mwenyezi Mungu, wanaopenda vitu na wadhalimu. Dawa ya wanaomkana Mwenyezi Mungu, wanaopenda vitu na wadhailmu ni kuitangaza, kuifundisha na kuitetea kwa hali na mali Qur'an na Hadith.

Kama hivyo ndivyo, tutaweza kubadilisha mambo mengi na kupata watu wema. Watu wema hawatokei kwa bahati mbaya, bali wanatayarishwa. Sina wasiwasi hili linawezekana, hivyo tujaribu.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook