Na Mwapwani Mohammed
KULINGANISHA na dini nyinginezo, Uislamu pekee undio ulio na taasisi zilizo "multi-purpose" kwa jina la Misikiti. Misikiti ni taasisi muhimu sana katika Uislamu. Wakati wa Mtume (s.a.w.) Msikiti wake ndio ulikuwa Ikulu, jengo la kusalia, Chuo cha Elimu, Ukumbi wa mikutano, mahali pa kupanga mikakati ya Jihad n.k.
Harakati zote za kuuneza Uislamu ulimwenguni kimahubiri (Da'awah) na kivita (Qitali) zilipangwa na kuratibiwa katika Msikiti wa Mtume (s.a.w.).
Hivi leo tunashuhudia ulimwengu wote umejaa Waislamu, Misikiti, Taasisi za Kiislamu, ustaarabu wa Kiislamu (n.k.) vyote vikiwa ni matunda ya Msikiti mmoja tu wa Mtume (s.a.w.), Allahu Akbar.
Tofauti kubwa ya Msikiti katika Uislamu na Makanisa au Masinagogi ni kuwa Misikiti haitawaliwi, kuongozwa au kudhibitiwa ama kuendeshwa kwa kile kinachoitwa "religious hierachy".
Misikiti huendeshwa na waumini wenyewe ambao hufanya iwepo, kimsingi Msikiti ni mali ya Allah (s.w.) na si milki ya watu wa kikundi au dhehebu fulani kama ilivyozoeleka.
Msikiti katika Uislamu huwapa waumini wa vikundi na hali zote hali ya kutoa pumzi. Leo hii sijui hali ikoje katika Misikiti yetu? Kihistoria, Mtume (s.a.w.) sio tu alijenga Msikiti bali pia alihimiza na kuratibu matumizi yake, hivyo Misikiti iliwafaidisha sana Waislamu kisiasa na kijamii, tofauti na leo Waislamu tumetosheka kwa kuyafanya majengo ya kusalia.
Madhumuni makubwa ya kuwepo Misikiti ni kwa ajili ya Waislamu wenyewe waweze kukutana pamoja, kuangalia mambo yao na kujadili matatizo yanayoikabili jamii kisiasa, kielimu, kiuchumi, kiutamaduni n.k..
Kwa bahati mbaya madhumuni haya hayaangaliwi na matokeo yanayotarajiwa hayapatikani kutoka katika mikusanyiko ya Waislamu Misikitini.
Inasikitisha sana kuona japo Misikiti imezagaa na Waislamu wanafurika humo kila siku lakini Uislamu umepoteza kabisa umuhimu, heshima na fahari yake.
Ulimwengu wote umejaa kufru dhidi ya Mwenyezi Mungu,hata zile nchi zinazojiita za Kiislamu na nyinginezo zimejiingiza katika vifungo vya ibada ya kumwabudu shetani mkubwa anayeukabili ulimwengu hivi leo (Amerika). Uislamu halisi unaangamiza tamasha za bure, ibada za kuabudu miungu ya uongo na ubinafsi.
Maasi ya kutisha (mauaji, ulevi, kuacha sala, ufuska n.k) yamekuwa ndio ibada ya watu wengi, inasikitisha zaidi kuona kuwa Waislamu na baadhi ya viongozi wao ndio wako mstari wa mbele kuyatenda au kuyatetea maasi hayo katika fikra kwamba Uislamu haujaendelea kiutamaduni, kifikra, kiuchumi n.k. Akili za Waislamu wengi zimeshawishika kwa kadri iliyowapelekea wautupilie mbali Uislamu wao.
Wanachojivunia Waislamu wa leo ni sehemu iliyobaki baada ya kukikata kichwa cha Uislamu, wamejitengenezea na kutengenezewa hali ya namna hii, wanaswali, wanafunga, wanakwenda "kutalii" Makka, basi.
Katika hali kama hii, kazi ngumu na ya hatari iliyofanywa na Mtume (s.a.w.) na maswahaba zake, Tabiina, Tabii-Tabiina na Waislamu wa huko nyuma umeporomoka na kubaki katika vitabu vya historia tu.
Sababu mojawapo kubwa ya kutokea kwa hali hii ya kufedhehesha Uislamu ni Misikiti na taasisi za Kiislamu kuongozwa na watu wasiostahiki.
Watu hao wakiwa na malengo ya kuua Uislamu kwa kutumia majina mazito ya Kiislamu, wameigeuza Misikiti na taasisi za Kiislamu kuwa miradi yao ya kujinufaisha kidunia. Baadhi yao hutumia hata njia zisizokubalika kuhodhi nafasi walizonazo, wengi wa viongozi wa aina hii wamejazana Misikitini na katika taasisi za Kiislamu.
Kibaya zaidi ni kitendo cha viongozi hao kuwazuia, kuwatisha, kuwaadhibisha (kwa kutumia vyombo vya dola) na kuwapa madhila makubwa Waislamu wanaotaka kuitumia Misikiti na taasisi zao kwa matumizi yake ya asili (kueneza Uislamu).
Viongozi hao wanataka Misikiti ibaki kuwa makambi ya kufanyia maozezi ya viungo (physical exercises) mara tano kwa siku.
Ili kufanikisha malengo yao, viongozi hao huwashakiza wenye mamlaka na serikali zilizopo watumie nguvu za dola kwa manufaa yao binafsi, na kuwazima wanaharakati.
Mara nyingi viongozi wa aina hii ni wasababishaji wakubwa na wastawishaji wa mizozo Misikitini nao huona njia inayofaa kuwa ufumbuzi wa mizozo hiyo ni kukimbilia vyombo vya dola kuomba "misaada" ya kuwazima wale wanaowaita "wakorofi wachache".
Sifa za viongozi wa Misikiti na taasisi za Kiislamu zinaelezwa wazi na Allah (s.w.) katika Qur'an 9:18-19: "Wanaoamrisha Misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na kusimamisha sala na kutoa zaka na hawamuogopi yeyote ila Mwenyezi Mungu; basi hao ndio wanaotarajiwa kuwa miongoni mwa walioongoka.
Je, mnafanya kuwanywesha maji mahujaji na kuamrisha Msikiti mtukufu ni sawa na (kazi ya) wale walioamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wakaipigania dini ya Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu". (Qur'an 9:18-19)
Hapo Allah (s.w) anafafanua wazi kuwa, sifa kubwa za viongozi wa Kiislamu ni hizi, "...na hawamugopi yeyote ila Mwenyezi Mungu", "...wakaipigania dini ya Allah".
Hivyo, ni wazi kuwa kiongozi wa taasisi ya Kiislamu au wa Msikiti (Imamu) anayeogopa kitu chochote aidha serikali au dola na anayemugopa yeyote kuliko anavyomugopa Allah (s.w.) na asiyetaka kuipigania dini ya Allah (s.w.) kwa mali zake, nafsi yake na nguvu zake hafai kabisa kuwa kiongozi katika umma wa Kisilamu na kama anafahamu hilo kwa heshima yake ni bora akajiondoa mwenyewe kwa kujiuzulu mara moja, na kama hafahamu na wala hana uungwana wala heshima ni wajibu wa waumini kumuondoa mara moja na kwa haraka ili asiuletee Uislamu na Waislamu madhara zaidi.
Misikiti au taasisi zinazowakumbatia viongozi wasio na sifa zilizotajwa na Allah (s.w.) hizo ni jumuiya za wanafiki. Na hazitofautiani na Masjid Dhirara uliojengwa na wanafiki wa Madina wakati wa Mtume (s.a.w.) (Qur'an 9:107-110). Kwa kuwa Allah (s.w.) aliamuru Msikiti huo uvunjwe, basi Misikiti au taasisi za aina hiyo nazo zivunjwe. Ikishindikana kuzivunja basi visusiwe kwani ni vyombo vya kuupiga vita na kuuangamiza Uislamu (9:107). Kinatuzuia nini kuikimbia Misikiti na taasisi za aina hiyo?
Ndio sababu inakuwa haieleweki wala kutambulika kwanini umma wa Kiislamu unaendelea kulalamika juu ya wanachosema dhuluma za serikali wakati Qur'an ambayo ni kioo cha Uislamu inaamrisha, inaelekeza na kuongoza katika kukabiliana na hali iliyopo.
Viongozi wa Kiislamu lazima wafahamu kuwa wao ndio ummat Muhammad (s.a.w.). Hivyo wao wanapolegea na kujawa na hofu, umma wote nao unalegea na kuangamia.
Aidha, wazingatie kuwa Misikiti au taasisi za Kiislamu zinakuwa halali pale tu zinapotumika katika kuupigania Uislamu. Misikiti na taasisi zenye lengo kinyume na hilo ni haramu na hazistahiki kuwepo kwa kutumia jina la Kiislamu.
Nao waumini (Waislamu) wengine wote lazima wahakikishe viongozi wao hawaitumii Misikiti na taasisi zao kinyume na lengo la Allah (s.w.) la kuueneza, kuupigania na kuuhami Uislamu. Wasiwe na uvumilivu na viongozi wa aina hiyo ambao wana unajisi Uislamu kwa manufaa yao.
Ninamuomba Allah (s.w.) kwa
utukufu wa Uislamu kuulinda kutoka katika makucha ya wadhalilishaji wa
ulimwengu. Na kwa Waislamu wote washikane na ahadi ya Allah (Qur. 3:102),
kushika ahadi hii ni kusaidiana na kushirikiana na kuepukana na kitu chochote
cha kutengana, kuleta hitilafu na kujiabudu wenyewe ambavyo ni vyanzo vya
kushindwa na kuubakisha Uislamu na nguzo zake nyuma. Haya yatosha kuwa
waadhi kwa wale waliojaliwa uongofu na Mwenyezi Mungu (s.w.).
|
|