Hija ni nguzo ya tano ya Uislamu iliyofaradhishwa kwa waumini kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:
"... Na Mwenyezi Mungu amewawajibishia watu wafanye Hija katika Nyumba hiyo (Al-Ka’aba), yule awezaye kufunga safari kwenda huko. Na atakayekanusha (asiende na hali ya kuwa ana uwezo) basi Mwenyezi Mungu si muhitaji anayewahitajia walimwengu"(3:97).
Pia katika hadith iliyosimuliwa na Abu Hurairah, Mtume (s.a.w) alitoa khutuba akasema:
"Enyi watu! Hija imeamrishwa kwenu, basi Hijini". Mtu mmoja akauliza: "Ee Mtume wa Allah! ni kila mwaka? Mtume (s.a.w) alinyamaza mpaka yule mtu akarudia kuuliza swali hilo mara tatu. Kisha Mtume akasema: "kama ningalisema Ndio, ingalikuwa faradhi kuhiji kila mwaka na pangalikuwa hakuna hiari ..." (Muslim).
Hija imefaradhishwa kwa Waislamu wenye uwezo wa kusafiri na kugharimia safari na masurufu, mara moja katika maisha yao. Mwenye uwezo wa kuhiji, akaacha makusudi kuhiji si Muislamu japo ataendelea kujiita Muislamu na watu wataendelea kumuita hivyo, kwani Allah (s.w) anasema:
".. Na atakayekanusha (asiende na hali ana uwezo) basi Mwenyezi Mungu si muhitaji, kuwahitajia walimwengu" (3:97).
Maneno haya ya Allah (s.w) ni makemeo makubwa sana kwa wanaopuuzia Ibada hii. Allah (s.w) hana haja na Uislamu wao, na matendo yao mema waliyofanya yataruka patupu kwani Allah (s.w) hana haja nayo. Katika kuonyesha ubaya wa kukanusha amri hii ya Hija, Mtume (s.a.w) anasema katika hadith iliyosimuliwa na Ali (r.a) kuwa:
Yeyote atakayekuwa na uwezo wa kuhiji katika Nyumba ya Allah, lakini asifanye hivyo akifa atakuwa hana tofauti na Myahudi au Mkristo na hiyo ni kwa sababu Allah (s.w) amesema:
"... Na Mwenyezi Mungu amewaamrisha watu wafanye Hija katika Nyumba hiyo, yule awezaye kufunga safari kwenda huko ..." (3:97) (Tirmidh).
Ni katika msingi huu Mtume (s.a.w) amemuru katika hadith aliyosimulia Ibn Abbas:
"Yeyote anayehusika kuhiji, na aharakishe". (Abu Daud, Darimi).
Hivyo basi mtu akifikia baleghe na akawa na afya njema na uwezo wa kugharimia safari ya Hija, Ibada hiyo itakuwa faradhi kwake na kama hataitekeleza wakati huo na ikawa uwezo huo umemuishia baada ya Hija hiyo, basi afahamu vyema kuwa atahesabiwa kuwa kavunja faradhi ya Hija. Kwa hivyo kila Muislamu anapopata uwezo wa kuhiji, hana budi kuhiji wakati huo huo.
Hija na Umra ni Ibada za hali ya juu zenye kuahidiwa malipo makubwa mbele ya Allah (s.w) kama tunavyojifunza katika hadith zifuatazo:
Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: "Atakayefunga safari ya Hija kwa ajili ya Allah bila kuongea maneno maovu na kufanya vitendo viovu, atarudi (akiwa huru na dhambi) kama siku ile aliyozaliwa na mama yake." (Bukhari na Muslim).
Abu hurairah (r.a) amesimulia
tena kuwa Mtume wa Allah kasema: "Umra moja ni kifutio cha dhambi zilizofanywa
katika kipindi kati ya Umra hii na Umra inayofuatia na Haji iliyokamilika
(Haj-mab-bruur) haina malipo mengine isipokuwa Pepo." (Bukhari na Muslim)
Wanaowajibika kuhiji
"Na Mwenyezi Mungu anawaamrisha watu kufanya Hija katika nyumba hiyo (Al-Ka’aba) yule awezaye kufunga safari kwenda huko ..." (3:97).
Wanao faradhikiwa na Hija ni Waislamu wenye sifa zifuatazo:
(a) Waliobaleghe
Watoto wa kiume na wa kike ambao hawajabaleghe au hawajafikia umri wa kubaleghe (miaka 15), hawawajibiki kwa Hija hata kama wana uwezo wa kwenda huko. Hata hivyo watoto wanaruhusiwa kuhiji kama tunavyofahamishwa katika Hadith zifuatazo:
Ibn Abbas ameeleza kuwa katika safari ya Hija ya kuaga, mwanamke mmoja alimleta mtoto wake mbele ya Mtume na akauliza kama naye anaruhusiwa kuhiji. Mtume (s.a.w) alijibu: "Ndio na pia utapata malipo yake." (Bukhari).
Jabir (r.a) amehadithia:" tuliongozana na Mtume (s.a.w) katika msafara wa Hija na tulikuwa pamona na wanawake na watoto. Tuliitikia - "Labbayka" kwa niaba ya watoto na tulitupa mawe (kwenye minara( kwa niaba yao)". (Ahmad, Ibn Majah).
Kutokana na hadith hizi watoto pia wanaruhusiwa kuhiji, na vile vitendo wasivyoweza kuvitekeleza vifanywe kwa niaba yao na wazazi au walezi wao. Kama mzazi au mlezi itabidi ambebe mtoto kwa ajili ya kutekeleza ibada ya tawafu na sai, ni lazima anuie kuwa anamfanyia mtoto na haitachanganywa na tawafu na sai yake. Hivyo itabidi atufu na kusai tena kwa niaba yake mwenyewe. Ieleweke kuwa Hija ya mtoto haimvui mtu kwenye wajibu wa kuhiji atakapofikia baleghe. Hivyo mtu atakapofikia baleghe atalazimika kuhiji tena iwapo atakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
(b) Wenye Akili Timamu:
Mtu aliyepungukiwa au aliyevurugukiwa na akili k.m. kichaa, punguani, n.k. hawajibiki kwa amrisho lolote lile la Uislamu na hesabu yake ni kama ile ya mtoto ambaye hajafikia baleghe, kwani Mtume (s.a.w) amesema: "Kalamu (ya kuandika amali njema au mbaya ya mja) inasimamishwa kwa watu watatu - mtu aliye lala mpaka aamke, mtoto mpaka afikie baleghe, na kichaa (mgonjwa wa akili) mpaka apone."
(c) Waungwana
Wafungwa au watumwa hawawajibiki kwa Hajj mpaka watakapokuwa huru.
(d) Wenye Uwezo
Wanaowajibika kuhiji ni wale wenye uwezo wa afya, na nauli ya kuwawezesha kufunga safari ya Makka ya kwenda na kurudi, pamoja na matumizi (masurufu) ya safari nzima na matumizi ya kuwaachia ahli zake nyumbani. Si vyema mtu kuzunguka huku na huku kuomba omba kwa ajili ya Hija. halikadhalika si vyema mtu kufunga safari ya Hija na huku hana masurufu ya kumtosha kufunga itambidi katikati ya safari aanze kuombaomba ili aweze kumaliza safari, na huku nyumbani ahali zake kwa kukosa mahitaji muhimu ya maisha yao, itawabidi wazunguke huku na huko kuombaomba. Kwa ujumla kuombaomba katika Uislamu ni haramu. Kwa nini kujikalifisha nafsi na hali faradhi ya Hija ni kwa wale tu wenye uwezo?
Katika aya ifuatayo, Mwenyezi Mungu anasema:
".. Na Mwenyezi Mungu amewajibisha Hajj katika Nyumba hiyo (al-Ka’aba) kwa yule awezaye kufunga safari kwenda huko. (3:97).
Aidha Allah (s.w) anatuhimiza kuchukua masurufu ya kutosha katika aya ifuatayo:
"...Na chukueni masurufu (ya kutumia njiani, msiombe) Na hakika msurufu bora ni yale yanayomfanya mtu asiombe. Na nicheni Mimi enye wenyi akili" (2:197).
Ni dhahiri kuwa endapo mtu hana masurufu ya kumtosha yeye mwenyewe kutumia njiani,na ya kumtosha kuwabakishia kitu cha kuwatosha ahali zake, hawajibiki kwa Hija hata kama ana nauli ya kwenda na kurudi. Kama mtu ana uwezo wa mali lakini hana uwezo wa afya kwa sababu ya ugonjwa au uzee, hatawajibika kwa Hija. Mgonjwa atawajibika tena atakapopona endapo atakuwa bado ana uwezo wa kimali. Wazee na wenye magonjwa ya kudumu, kama wana mali ya kutosha kuhiji watawapa ndugu zao Waislamu wakahiji kwa niaba yao, kama tunavyojifunza katika Hadith ifuatayo:
Imesimuliwa na Fazal bin Abbas kuwa mwanamke mmoja kutoka katika kabila la Banu Khasham alimuuliza Mtume (s.a.w): "Allah (s.w) amefaradhisha Hija kwa watu wote, lakini baba yangu ni mzee sana kwa kiasi kwamba hawezi kufunga safari hii ya Hija Je, ninaweza kuhiji kwa niaba yake?" Mtume (s.w) alimpa ruhusa ya kufanya hivyo. Hii ilitokea katika Hija ya kuaga. (Bukhari na Muslim).
Ni muhimu kwa wenye kuhiji kwa niaba ya wengine, wawe wenyewe wameshahiji kwa mnasaba wa hadith ifuatayo:
Abdullah bin Abbas ameeleza kuwa katika Hija ya kuaga, Mtume (s.a.w) alimsikia mtu mmoja akiitikia "Labbayka" kwa niaba ya Shubruma. Alimuuliza yule mtu kuwa yeye mwenyewe keshahiji. Alipopata jibu kuwa haja hiji, Mtume (s.a.w) alimuamuru kufanya Hija yake kwanza na ndio baadaye afanye Hija kwa niaba ya Shubruma. (Abu Daud).
Mwenye kuhiji kwa niaba ya mwingine atapata malipo ya Hija sawa na yule aliyefanya Hija kwa niaba yake ambaye ndiye aliyetoa gharama zote za Hija. Pia inajuzu kufanya Hija kwa niaba ya ndugu Muislamu aliyefariki huku akiwa na uwezo na nia ya kuhiji kama tunavyojifunza katika hadith ifuatayo:
Amehadithia Abdullah bin Abbas kuwa mwanamke mmoja aliuliza: "Mama yangu alinuia kuhiji lakini alifariki kabla ya Kuhiji. Je, naweza kuhiji kwa niaba yake? Alijibu Mtume (s.a.w)" unaweza, hasa. Jaalia kuwa mama yako alikuwa na deni, je isingelikuwa umeshamlipia deni hilo? Hali kadhalika hili ni deni la Allah (s.w) juu yako na Allah (s.w) ana haki zaidi na deni lake kuliko mwingine yeyote"(Bukhari).
Kutokana na hadith hii Muislamu yeyote aliyekufa na deni la Hija, yaani aliyekuwa na mali na uwezo wa kumuwezesha kuhiji lakini akafa bila ya kuhiji, itabidi warithi wake, kabla ya kugawanya urithi watenge fungu la kutosha kuhiji kwani hili ni deni kwa Allah (s.w). Kisha warithi watamteau miongoni mwao au Muislamu yeyote kwenda kufanya Hija kwa niaba ya marehemu kwa kutumia fungu hilo.
(e) Wasiowekewa kizuizi njiani
Iwapo njia wanayosafiria kwenda Hija itakuwa imewekewa kizuizi au imefungwa kwa karantini (Quarantine), kwa usalama au kwa sababu nyingine yoyote, basi Waislamu wa sehemu hiyo hawatalazamika kwa Hija mwaka huo.
(f) Wanawake waongozane na Maharim:
Hija imeamrishwa kwa Waislamu wanaume na wanawake wenye sifa zote hizo zilizotajwa hapo juu (a)-(e), lakini pia mwanamke hatawajibika kwa Hija mpaka apate wa kuongozana naye, awe mume wake au maharimu wake kama tunavyojifunza katika hadith zifuatazo:
Abu Sayyid Khudri amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: "Ni haramu kwa mwanamke mwenye kumuamini Allah na siku ya Mwisho kuchukua safari ya siku moja au zaidi bila ya kuandamana na baba yake au kaka yake au mume wake au mtoto wake wa kiume au maharimu wake wengine" (Bukhari).
Inaendelea toleo lijalo
|
|