BARUA
 

Uvaaji wa hijabu shule za msingi

Ndugu Mhariri

SISI wanafunzi wa shule ya msingi Makurumla tunaomba kutoa machache yahusiyo uvaaji wa Hijabu katika shule za msingi.

Tunampongeza Mwalimu Mkuu wetu Juma Abdallah kwa kututangazia wanafunzi wote wa Kiislamu (wasichana) kuwa tumepewa ruksa kuvaa hijabu shuleni ambazo alieleza ziwe nyeupe na sketi ya bluu iwe ndefu, pongezi sana.

Kutokana na tangazo hilo, walimu wa shule hii wamelipokea kila mmoja kwa mtazamo wake. Wengine wamefurahia na wengine wamechukia.

Kati ya walimu waliochukia ni pamoja na Mwalimu E. Msimbe ambaye anafundisha darasa la tatu, yeye huwavulisha wanafunzi wa mkondo wake hijabu mara tu anapoingia darasani na kuwaambia wamevaa matambara ya kufutia meza, mara wananuka n.k.

Kwa kweli sisi wasichana ambao wadogo zetu wanafanywa hivyo tunajisikia vibaya na tunashindwa kumuuliza kwa kuogopa kupigwa.

Hivyo tumeona heri tulete malalamiko yetu katika gazeti letu. Wapo na wengine wa darasa la IV na la VI hawapendelei Hijabu nao hutoa lugha za matusi (kashfa).

Pamoja na hayo bado ndugu zetu wengine wanaosoma shule jirani wanatuuliza "mbona nyie mnavaa hijabu? Tukiwaambia tumetangaziwa hushangaa kwani shule kama Karume, Turiani na Magomeni hawajaruhusiwa kuvaa hijabu, nasi tungependa kujua ni kwanini wao wasiruhusiwe? Mbona shule ya Mianzini na Makurumla wameruhusiwa?

Ni sisi Wanafunzi Makurumla,
S.L.P. 7070,
Dar es Salaam.



Walimu hawa wanatushangaza

Ndugu Mhariri

NASEMA wanatushangaza tena wanatushangaza kweli walimu wanaogomea wanafunzi wa Kiislamu kuvaa mavazi ya stara (hijabu) mashuleni.

Baadhi yao katika hoja wanazozitoa kupinga wanafunzi Waislamu kuvaa hijabu ni kutopata waraka unaowapa maelezo hayo.

Lakini hii inashangaza kwa sababu mbona wakati wa kuahirishwa kwa mitihani ya kidato cha nne mwishoni mwa mwaka jana serikali ilitumia vyombo hivyo hivyo vya habari, na mitihani hiyo ilisitishwa kufanywa?

Mbona hatujasikia walimu wakuu nchini wakiwaamuru wanafunzi waendelee kufanya mitihani hiyo kwa kuwa hawakupata waraka unaowapa maelekezo hayo?

Kwanini walimu hao wasijiulize kwa sababu gani wao hawakupata waraka huo hadi hivi leo? Kwanini wasifuatilie Wizara ya Elimu kuulizia waraka huo? Mbona mishahara yao ya mwezi mmoja tu ikichelewa huifuatiila kwa nguvu zote?

Hii inatuonyesha wazi kabisa kwamba sababu si maagizo wala waraka, bali kinachowasumbua walimu hao ni ugonjwa wa kuogopa Uislamu na chochote kinachohusiana au kunasibishwa na Uislamu basi kinampa msisimko usiopendeza na anaingiwa na hofu kubwa. Kama wanavyofanya hivi sasa baadhi ya wakuu wa shule juu ya uvaaji wa mavazi ya stara (hijab) mashuleni.

Dk. K.K. Rashid,
Mikocheni,
Dar es Salaam.



Viongozi wako kwenye kampeni?

Ndugu Mhariri

KWA muda wa mwezi mmoja sasa viongozi wetu wa juu wako kwenye ziara sehemu mbalimbali nchini.

Wakati Rais akiwa Singida, Makamu wa Rais alikuwa mikoa ya ziwa, wakati huo huo Waziri Mkuu alikuwa Tabora.

Hotuba za viongozi hawa hasa ile aliyoitoa Rais kule Pemba zinavunja moyo. Inavyoonyesha viongozi wetu hawana habari na matatizo yanayowataza waliowachagua.

Nasema hivi kwa sababu mikoa ya Tabora, Singida na Kisiwa cha Pemba iko nyuma sana kimaendeleo.

Wananchi wa sehemu hizi tumeachwa kama wakiwa kwa kipindi chote cha utawala wa Tanzania huru.

Nilitegemea serikali ya awamu ya tatu kwa ahadi ilizozitoa juu ya kuwaondolea kero wananchi ingeelekeza jitihada zake kwa kuipa kipaumbele mikoa hii lakini wapi.

Cha ajabu zaidi ni kwamba badala ya japo kuzungumzia kutatua matatizo ya wananchi wanapita wakiwakoga wapinzani.

Je, viongozi wetu mmeanza kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa mwakani?

Kama hivyo ndivyo kutaka kwenu kuendelea kuongoza kuna maana gani wakati hamjali matatizo yetu wala hampo tayari kutusikiliza.

Hatuoni sababu ya kuwachageni tena ili mrejee madarakani. Wapisheni wenzenu wenye kujali shida za watu.

Khalfani Idd,
Singida.



Mambo yajirudia Mlimani

Ndugu Mhariri

FEBRUARI 19, mwaka huu Rais wa awamu ya tatu alitembelea Chuo Kikuu Mlimani kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe. Huko Mlimani kaambiwa amstaafishe Bw. Abdallah Ngororo.

Hii inanikumbusha tukio la miaka ya nyuma wakati wa utawala wa awamu ya pili wakati wanafunzi wa Chuo hiki kusema hawamtaki Katibu Mkuu wa Wizara mama Dk. Mohamed Bilal na Waziri wa Fedha Shujaa Profesa Kighoma Malima.

Chakushangaza kwa haya majina mawili wote walikuwa Waislamu na kwa wakati huo shujaa Profesa Malima alikuwa Waziri wa Fedha, wanafunzi hawakutaka Waziri wa Elimu ya Juu kwa wakati ule (sasa ndiye Rais) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha wastaafishwe?

Hawa wanafunzi wametawaliwa na chuki za kidini. Kwa wakati ule Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ya Juu alikuwa Muislamu, Waziri wake Mkristo na Wizara ya Fedha Waziri alikuwa Muislamu na Katibu wake ni Mkristo.

Hii inaonyesha kuwa mlimani hatakiwi Muislamu kabisa. Matatizo ya Mlimani makubwa yanasababishwa na uchumi duni wa nchi, sehemu ndogo sana inasababishwa na uongozi. Sasa kama serikali haitoi fedha za kutosha na kwa wakati muafaka, Bw. Ngororo afanye nini maskini?

Tukio la Mlimani la Februari 16, mwaka huu linaonyesha udini tu si zaidi ya hapo.

I.D. Mjema,
Box 2654,
Arusha.



Walimu wakuu mnapanda mbegu gani ?

Ndugu Mhariri

SIJAELEWA hasa kinachowafanya walimu wakuu wasimame kidete kuzuia vazi la stara kwa baadhi ya wanafunzi wao.

Hivi nini hasa kinachowakera hadi waamue kuwa wagumu kuruhusu vazi hilo. Nini hasa matarajio katika kampeni ya hii. Hoja zinatolewa kuzuia vazi hili zinawadhalilisha wakiwa kama walezi waliokabidhiwa dhamana ya ulezi wa akili, maadili na Man power ya kizazi kijacho.

Kwa nini hawagopi historia kurekodi msimamo huu usio na busara. Wanadhani kuwa kwa kufanya hivi watawakomoa wale wanaotaka kujistiri kwa mujibu wa imani zao.

Mbona wamekuwa wepesi kuruhusu kutumika vyumba vya madarasa ya shule zao kwa ajili ya mikutano ya kiroho ya madhehebu fulani kila jioni.

Hivi kwa kufanya hivi hawaoni kuwa wanapandikiza chuki za kidini miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzao wa madhehebu mengine. Wanafanya hivi kwa manufaa ya nani?

Zuberi Mwafongo,
Dar es Salaam.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook