Maelfu yashangilia askari wa Nigeria
Mwafrika, No. 1,121 Ijumaa Aprili 10, 1964
UMATI wa maelfu ya watu leo walijipanga katika barabara kadhaa za mji wa Dar es Salaam kuwashangilia askari jeshi wa Nigeria wakati wakipita kutoka kwenye gwaride lililokuwa kwenye jumba la Rais.
Baada ya askari hao kuondoka kwenye jumba la Rais, waliongozwa na gari la polisi kupitia katika barabara za Azania Front, Acacia Avenue, Independance na Uhuru Street.
Kisha waliongozana katika barabara ya Lumumba wakapita kwenye makao makuu ya TANU.
Kutoka katika barabara ya Lumumba waliongozana katika barabara ya Morogoro Road na kuendelea mpaka Karimjee Hall ambako walichukuliwa na magari yao kurudi Colito Barracks.
Mapema kwenye Jumba la Rais, askari hao walikaguliwa na Rais wa Jamhuri Bwana Nyerere, katika sherehe maalum.
Katika hotuba ya kuwakaribisha askari hao, mwalimu alisema kwamba kule kuwepo kwa askari wa Nigeria hapa ni ushahidi wa wazi kuonyesha uwezo wa Umoja wa Afrika.
Mwalimu Nyerere alisema kuwa kuwapo kwa jeshi la askari wa nchi ndugu ya Afrika nchini Tanganyika ni matokeo ya matukio mabaya ya mwezi wa Januari’.
Hata hivyo alitamka, ‘tukisahau tukio hilo, nataka Watanganyika na Wanigeria waone kuwa kukakaa kwa kikosi hicho hapa ni jambo la furaha na kusisimua.
Akiwakaribisha askari hao
Mwalimu alisema kwamba sio tu kama anatoa shukurani zake kwa Rais na serikali
ya Nigeria, lakini anawasemea Makamu wa Rais, serikali na watu wa Tanganyika.
UHURU, No. 941, Jumatano, Agosti 23, 1967
JIMBO la Nigeria ya Mashariki lililojitenga na kujiita Jamhuri ya Biafra liko tayari kufanya mazungumzo ya usuluhishi wa kutafuta amani na serikali ya Shirikisho iwapo Serikali hiyo inayoongozwa na Major General Yakubu Gowon, itaitambua Biafra kama ni Taifa na wala sio kama Jimbo ambalo ni sehemu ya Nigeria kama ilivyokuwa zamani.
Habari hizi zilitangazwa kwa njia ya Radio na Gavana wa Biafra, Lt. Col. Odumegu Ojukwu jana usiku na usikiliza hapa Cotonou, Dahomey.
Radio hiyo baadaye ilieleza kwamba Ojukwu ameyasema hayo akiwa anarudia wito wake wa kumtaka Gowon akubali amani baina ya Shirikisho na Biafra.
Habari kutoka Lagos, mji mkuu wa Shirikisho la Nigeria, zimeeleza kwamba majeshi ya Biafra sasa yameteka na kuzitawala barabara zote kuu zinazokwenda Lagos na Ibadan, mji mkuu wa Jimbo la Nigeria ya Magharibi ambako majeshi hayo yamekwisha teka baadhi ya miji.
Jana majeshi hayo yaliuteka mji maarufu sana wa jimbo hilo uitwao Ore na majeshi ya Shirikisho yaliyokuwa huko yamekimbilia.
Habari hizo za kuaminika zilizotangazwa na msemaji mmoja wa serikali ya Shirikisho zinazidi kueleza kwamba ndege za majeshi ya Shirikisho yanatazamiwa kufanya mashambulio kwa kuyapiga mabomu majeshi ya Biafra ili kuyazuia yasiingie zaidi katika jimbo la Magharibi. Lakini majeshi hayo ya Biafra yamenuia kabisa kwenda ndani zaidi ya jimbo hilo na kuteka miji zaidi kwa kadiri watakavyoweza.
Majeshi ya Shirikisho yanategemea kuzitumia ndege mpya zilizowasili Lagos juzi kutoka Urusi na Czechoslovakia.
Mji wa Ore ambao sasa uko mikononi mwa majeshi ya Biafra ni njia panda ya barabara zote kuu zinazokwenda Lagos, Ondo na Ibadan.
Majeshi ya Shirikisho nayo
yametangaza kuwa yameiteka barabara moja maarufu katika Biafra pamoja na
Reli ilioko umbali wa maili 20 tu kutoka mji wa Nsukka, Biafra. Yametangaza
pia kuwa kikosi kimojawapo cha Shirikisho kimekaribia sana kuingia katika
mji wa Enugu, mji mkuu wa Biafra.
Mwafrika, No. 169 Jumamosi Juni 13, 1964
VIONGOZI wa chama cha African National Congress wa Afrika ya Kusini ambao walikuwa wakishitakiwa kwa makosa ya kutaka kuiangusha serikali ya huko walihukumiwa jana mjini Pretoria kifungo cha maisha, habari hii ilitangazwa mjini Dar es Salaam na Bw. Oliver Tambo Makamu wa Rais wa chama hicho.
Viongozi hao ambao kesi yao imekuwa ikisikilizwa kwa muda wa karibu ya miezi sita ni Nelson Mandela, Walter Sisulu Govan Mbeki, Ahmed Kathrada, Raymond Mhlaba, Andrew Mlangeni, Denis Goldberk na Elias Matsoaledi.
Kwa muda huo wote ambao kesi
ilikuwa ikiendelea kusikilizwa nchi nyingi katika dunia ambazo hazikubaliani
na siasa ya ubaguzi inayoendeshwa na Afrika ya Kusini zimejaribu bila ya
mafanikio kuiomba serikali ya Afrika ya Kusini kuachilia mbali mashtaka
ya watu hao.
Ngurumo Jumatano Mei 3, 1961
MATEMBEZI ya Mh. Bw. Nyerere kuzuru sehemu mbalimbali za Tanganyika baada ya kuwa Prime Minister yalitangaza jana alasiri. Waziri Mkuu wa kwanza ataanza kuitembelea wilaya ya Dodoma ambapo atapata nafasi ya kuonana na wakuu wa wilaya hiyo na kuzungumza nao kwa ukamilifu jinsi gani shida ya njaa inavyoweza kupunguzwa kwa haraka. Ataondoka kwa ndege ya serikali tarehe nne, kesho.
Baada ya kupumzika, jioni hiyo hiyo ataonana na wajumbe wa baraza la mji huo, na hatimaye atakagua majengo mapya ya baraza hilo.
Ataona vipofu
Asubuhi yake Waziri Mkuu atazuru makao makuu ya idara ya utafutaji wa mawe, pia ataitembelea hospitali ya Dodoma na hospitali inayowatunza vipofu wa kiume huko Buigiri.
Jumamosi ataondoka Dodoma na gari mpaka Manyoni ambako anatazamia kuonana na kikundi cha wajumbe wa baraza la mji huo, na hatimaye atakwenda kuonana na wajumbe wa baraza la Turu na Maofisa kutoka Kiomboi. Atarejea Dodoma kwa gari Jumapili.
Magharibi
Baada ya kuzuru jimbo hilo la kati Waziri Mkuu atakwenda mpaka jimbo la Magharibi Jumatatu kwa ndege mpaka Tabora. Vile vile atazuru wilaya ya Nzega ambako ataonana na wajumbe wa baraza la mji huo na baadhi ya wajumbe wa baraza la jimbo la Magharibi. Atalala hapo.
Ofisi
Asubuhi Jumanne atarejea Tabora na kushiriki katika mkutano wa baraza la mji na jimbo pia. Jumatano atafungua ofisi za TANU kabla ya kuruka kwa ndege kuelekea Kigoma.
Mkutano
Alhamisi, Waziri Mkuu baada
ya kuonana na wajumbe wa baraza la mji, atahutubia mkutano wa halaiki huko
Ujiji jioni hiyo ataruka hadi Sumbawanga. Ijumaa tarehe kumi na mbili,
baada ya kuonana na wajumbe wa baraza la Sumbawanga anatazamiwa kurudi
kwa ndege mpaka hapa Mzizima, kwa kupitia tena Tabora.
|
|