KWA mujibu wa elimu ya lishe, matunda ni chakula cha ajabu. Hata hivyo, mtu hawezi kuishi kwa matunda pekee. Hii ni kwa sababu matunda mengi yana kiwango kidogo sana na protini na mafuta (fat).
Kwa ujumla thamani kubwa ya matunda ni vitamini mbalimbali na nyuzi nyuzi za kilishe (dietary fibres) zinazopatikana.
Ukiacha maziwa ya mama, matunda na mboga mboga ndiyo vyanzo vikuu vya vitamini C. Vitamini hii ni muhimu sana kwa kuuwezesha mwili kuwa na kinga imara dhidi ya maradhi. Inaimarisha fizi, mishipa ya damu na mifupa (cartilage).
Matunda yenye vitamini C kwa wingi ni kama vile mapapai, machungwa, maembe, epo, matikiti, strawberries, n.k..
Vitamini A pia ni kirutubisho kinachopatikana kwenye matunda aina nyingi. Matunda yenye vitamini A kwa wingi ni yale yenye rangi ya njano. Mfano wa matunda yenye vitamini A kwa wingi ni maembe, mapera, mapapai, machungwa, pasheni n.k.
Matunda vile vile yanatupa kirutubisho kinachoitwa Carotenoid. Kirutubisho hiki kinasaidia kupunguza uwezekano wa mtu kupat maradhi ya Saratani (kansa).
Zaidi ya hayo, matunda ni chanzo kizuri cha nyuzi nyuzi za kilishe. Mtu akila vyakula vyenye nyuzi nyuzi za kilishe ana nafasi nzuri ya kupata choo kikubwa mara kwa mara. Yaani hatapata tatizo la kukosa choo (Constipation).
Nyuzi nyuzi za kwenye matunda yana kitu kinachoitwa Pectin. Pectin inasaidia kupunguza kiwango cha mafuta ya hatari (Cholesterol) kwenye damu.
Matunda yenye kiwango kikubwa cha nyuzi nyuzi ni kama vile epo, pasheni, tende, mapeyasi, machungwa, mapapai, maembe n.k. Kati ya vyanzo hivyo, matunda ya epo yanatoa nyuzi nyuzi nzuri zaidi kwa kuimarisha afya.
Matunda pia ni chanzo kizuri cha virutubisho vya sukari na baadhi ya madini.
Kabla ya kumaliza makala yetu ni vyema tukatazama swali moja ambalo watu wengi hujiuliza. Nile tunda au ninywe juisi ya matunda.
Ukinywa juisi unapata vitamini na sukari. Lakini unakosa nyuzi nyuzi za kilishe, ambazo umuhimu wake tumejifunza hapo awali. Kwa hiyo ni bora zaidi kula tunda kuliko kunywa juisi. Kama tunda halipo, ni afadhali unywe juisi kuliko kuacha kabisa.
Kama mtu anatengeneza juisi yake nyumbani ni vizuri juisi aichanganye na nyuzi nyuzi (alizozikamua).
Ni vyema pia watu wakakumbuka
kuwa vipande viwili mpaka vinne vya matunda vinatosha kwa siku kwa mtu
mmoja. Vile vile jitahidi kula tunda kila asubuhi na nyakati nyingine ambazo
siyo za mlo wa mchana au usiku. Yaani kula matunda wakati wake peke yake.
|
|