MASHAIRI

Mashairi ya zamani:

Azaliwapo kiumbe

Uhuru, Jumatatu, Aprili 3, 1967

Nimekuja mfanisi, mjuaji wa sheria,
Ninakuomba nafasi, Edita kunipatia,
Nipe nafasi upesi, niseme yenye murua,
Azaliwapo kiumbe, viumbe hushangilia.

Viumbe hushangilia, furaha zinawajia,
Ashura kajifungua, mtoto kajipatia,
Mola atamkuzia, kisha awe wa mafaa,
Azaliwapo kiumbe, viumbe hushangilia.

Mtoto kajikulia, kimo amejipatia,
Hapo utawasikia, mtoto hakukawia,
Mwanzo wanaanzia, mtoto hatosikia,
Azaliwapo kiumbe, viumbe hushangilia.

Mwaka umepinduka, kimo kimeshazidia,
Anajua ya dunia, mtu akimchukia,
Huanza yao balaa, Ashura kajisumbua,
Azaliwapo kiumbe, viumbe hushangilia.

Mtoto gani kichaa, hapo utawasikia,
Wanaanza kumwambia, usicheze na dunia,
Utakuja angamia, usipo iangalia,
Azaliwapo kiumbe, viumbe hushangilia.

Sifa mbaya zamjia, kiumbe kugeukia,
Heri kukosa kuzaa, mwana asiyesikia,
Lipi utakalomwambia, kama atakusikia,
Azaliwapo kiumbe, viumbe hushangilia.

Husuda inaanzia, mwache tutamkomoa,
Ataijua dunia, katu hatanichezea,
Bwana yule kazowea, yule si mtu balaa,
Azaliwapo kiumbe, viumbe hushangilia.

Beti tisa nachia, dunia jama maua,
Haswa ukiichungua, huishi kunyenyekea,
Mwanzo walimfia, kisha wakamchukia,
Azaliwapo kiumbe, viumbe hushangilia.

Juma Ali M. Madunga,
Mikongolo, Bagamoyo.



Si pana wala si ndefu

Si pana wala si ndefu, dunia mnaiona,
Na tenapo haikifu, toka kaumba Rabana,
Wala haina uchafu,  usiku hata mchana,
Dunia mnaiona, si pana wala si ndefu.

Si pana wala si ndefu, dunia mnaiona,
Wala haina kukifu, kila unapoiona,
Hali imekaa kefu, haichakai hapana,
Dunia mnaiona, si pana wala si ndefu.

Twaishi bila kukifu, wazee hata vijana,
Daima itakatifu, uzee kwake haina,
Nadhani mtaswadifu, haya ninayo yanena,
Dunia mnaiona, si pana wala si ndefu.

Akizaliwa Yusufu, aula bibi Amina,
Haioni hitilafu, kama imeumbwa jana,
Vile ilivyo nadhifu, kwa umbo lenye kunona,
Dunia mnaiona, si pana wala si ndefu.

Imeumbwa takatifu, aridhi imelingana,
Siyo pana siyo ndefu, po pote ukiiona,
Mbinguni ni marudufu, mapambo yamejazana,
Dunia mnaiona, si pana wala si ndefu.

Twapenda kukaa kefu, japo tuzeeke sana,
Hupendi ukatawafu, dunia kufarakana,
Twakufa kwa ikirafu, lazima yake Rabana,
Dunia mnaiona, si pana wala si ndefu.

Dunia yetu kunjufu, viumbe tumejazana,
Dunia ninaisifu, haina mwisho kuona,
Safari miaka alufu, kikomo hutakiona,
Dunia mnaiona, si pana wala si ndefu.

Beti sitii shufufu, naiogopa hiyana,
Mhariri mnyimifu, asije akalibana,
Akalifanya uchafu, mkakosa kuliona,
Dunia mnaiona, si pana wala si ndefu.

Ramadhani Masangama,
Tabora.



Vipi hali ya mkwezi

Juma bin Bwanakheri, habari za siku nyingi,
Leo natunga shairi, ninakujuwa kigingi,
Kwanza ulete habari, umepita muda mwingi,
Vipi hali ya mkwezi, aliokwama mtini.

Aliokwama mtini, vipi hali ya mkwezi,
Watu tulikaa chini, na kumuomba Mwenyezi,
Ipatikane amani, kwako na huyo mkwezi,
Vipi hali ya mkwezi, aliokwama mtini.

Tulichangia maoni, nawe hujaweka wazi,
Umepata afuweni, au bado ipo kazi,
Tujuwe tufanye nini, furaha au machozi,
Vipi hali ya mkwezi, aliokwama mtini.

Wenzangu nawatajeni, tuwe na mema makazi,
Kuluthum wa Pangani, ulisema waziwazi,
Ulijibu bila soni, amehemewa mkwezi,
Vipi hali ya mkwezi, aliokwama mtini.

Nae mzee wa dini, wa Moa mtu azizi,
Alijibu kwa uneni, hakufanya pingamizi,
Piga kelele mtini, watakuja wa saizi,
Vipi hali ya mkwezi, aliokwama mtini.

Hiyo ajali kazini, alijibu kama chizi,
Mikidadi Buruhani, alitowa uamuzi,
Kweli hakuna imani, jibu silo la mzazi,
Vipi hali ya mkwezi, aliokwama mtini.

Jibule lilinihini, nikafanya uchunguzi,
Imani nikabaini, imekuwa ni tatizi,
Nilimjibu kwa peni, ninafanya upembuzi,
Vipi hali ya mkwezi, aliokwama mtini.

Tamati natumaini, utajibu kwa uwazi,
Tujuwe hali shambani, pamoja na ya mkwezi,
Tutulie burudani, tumshukuru Mwenyezi,
Vipi hali ya mkwezi, aliokwama mtini.

Zuberi Mohammed Mwinyi (Amir),
P.O. Box 61428,
Dar es Salaam.



Vazi sitoliacha (hijab)

Huu ni wangu ujumbe, tena ujumbe mwanana,
Siwezi tii kiumbe, kumuasi Sub-hana,
Hata unune uvimbe, hizo ni zako laana,
Vazi langu siliachi, ukitaka nawe vaa.

Ni vazi rasmi kwangu, naeleza kwa hakika,
Ni amri yake Mungu, siwezi kuikiuka,
Nahifadhi mwili wangu, afurahie Rabuka,
Vazi langu siliachi, ukitaka nawe vaa.

Ni vazi la hakika, linanipendeza sana,
Mwilini nikiliweka, si usiku si mchana,
Heshima nitajitwika, na nema za Maulana,
Vazi langu siliachi, ukitaka nawe vaa.

Nitalivaa popote, shuleni hata nyumbani,
Sitomwogopa yeyote, aletae ushindani,
Hata afanye chochote, siogopi asilani,
Vazi langu siliachi, ukitaka nawe vaa.

Vazi ni mimi navaa, lakutia chuki gani?
Masomo nahudhuria, kama ni hapo shuleni,
Ninakaa natulia, kama hapo dawatini,
Vazi langu siliachi, ukitaka nawe vaa.

Ni vazi rasmi hili, ukweli niwaambie,
Msonalo kama hili, naomba muigizie,
Mlivae vazi hili, neema mjipatie,
Vazi langu siliachi, ukitaka nawe vaa.

Hapa ndio nakomea, ukweli nimeutoa,
Sitopenda kusikia, hijab kuichukia,
Atayependa kuvaa, ni rukhsa namwambia,
Vazi langu siliachi, ukitaka nawe vaa.

Hidaya Juma wa Tambaza,
MSAUD (MTP) Form V,
Kinondoni, Dar es Salaam.



Ajabu ya mtawala

Kuongopa hadharani, huwa ni kubwa khatia,
Tena ni kukosa soni, pia ila kujitia,
Hasa mshika sukani, mbele alotangulia,
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli.

Ni dhamana kuikhini,na kukejeli sheria,
Kuwafanya punguwani, watu walokuchagua,
Mwenzetu wajiamini, hujali kitofatia,
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli.

Yalosomwa ukumbini, risala ukasikia,
Kisha kusema mageni, eti ndiyo wayajua,
Wachekesha Bin-yamini, mche mwenye kuumbua,
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli.

Kwamba ile tafrani, wewe hukuisikia,
Amri ya Parokoni, msiba ilotutia,
Kumbe mtawala gani, huyajui ya raia,
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli.

Hatuna matumaini, kuwa utafatilia,
Ni mbinu kutuzaini, ili tupate tulia,
Asokujueni nani, ghiliba na zenu ria,
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli.

Tulikwisha wabaini, matendo na zenu nia,
Mliyaanza zamani, wewe unayarukia,
Nyerere na wakoloni, walipita hiyo njia,
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli.

Tumeshakula yamini, nyuma mwiko kurudia,
Wala haya hatuoni, yetu kuyapigania,
Mnayokula sahani, sote tutaichangia,
Ajabu ya mtawala, kinywa kukosa ukweli.

Jihad R. Saballa,
Box 347,
Shinyanga.



Kombe la harusi (jibu)

Bismillahi naanza, shairi kuliandika,
Jinale natanguliza, Mola hana mshirika,
Apendalo hutumiza, kila analolitaka,
Nina mshukuru Rabi, Mola alotakasika.

Nia yangu na dhumuni, majibu kuyaandika,
Mshairi wa Pangani, kujibu nawajibika,
Nikutoe matatani, kama ulivyonitaka,
Hilo kombe la harusi, ni sherehe mojawapo.

Ni sherehe mojawapo, kombe huko harusini,
Si vibaya likiwepo, silitie haramuni,
Lakini kome mlapo, mchanganyiko acheni,
Hilo kombe la harusi, ni sherehe mojawapo.

Litakuwa ni halali, liliwapo kwa heshima,
Wale tu marijali, wasiwepo kina mama,
Wanawake wawe mbali, kupatikane salama,
Kombe hilo la harusi, ni haramu vitendo vyake.

Msiyafanye machafu, kombe muliandaapo,
Kuifanya israfu, wala nyimbo zisiwepo,
Vyakula kupangwa safu, ni haramu ndipo hapo,
Kombe hilo la harusi, ni sherehe mojawapo.

Wanawake kwenda cheza, hayo yote yawe sumu,
Na watu kwenda kutunza, ni vitendo vya haramu,
Dini yetu hukataza, Mashekhe hutulaumu,
Hilo kombe la harusi, vitendo ndio haramu.

Halali huwa haramu, mambo kupita mipaka,
Mambo ya Kiislamu, maadili kukiukwa,
Malipo Jahanamu, Ibilisi kutushika,
Kombe la harusi, ni sherehe ya harusi.

Hawakufanya Rasuli, kombe si katika dini,
Wala sitoi dalili, ushahidi vitabuni,
Ukweli wa kombe hili, ni mambo ya duniani,
Kila kombe la harusi, ni sherehe mojawapo.

Kombe hilo hivi sasa, kheri sasa iwe basi,
Lina kila mbaya visa, ndani yake Iblisi,
Sitoandaa kabisa, ndani yake uasi,
Kombe la hivi sasa, mambo yake ni haramu.

Mtume wetu Rasuli, hakusema kwa mafumbo,
Amesema neno hili, utakapofanya jambo,
Tumia yako akili, lifikirie kitambo,
Zingatia matokeo yake.

Ikiwa jambo la kheri, basi jambo lifanyize,
Na likiwa ni la shari, basi bora liachize,
Na hizi ndizo habari, mabaya tujikataze,
Hilo kombe hivi sasa, chakula hicho haramu.

B.A. Mohammed,
S.L.P. 4,
Pangani,
Tanga.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook