Tahariri
 
Tupo tayari kuuza roho kwa ajili ya Pepo
NCHI yetu ni ya utawala wa kisheria ambapo huelezwa kwamba mahakama ni huru na kuwa ni chombo kinachotarajiwa kusimamia sheria na kutoa haki.

Aidha, nchi yetu ni huru yenye serikali inayowekwa na watu ambapo haki za raia ikiwa ni pamoja na uhai wao na mali zao hulindwa na katiba na sheria za nchi.

Ili kuhakikisha haki hizo na nyingine hazihujumiwi; serikali imekuwa ikikemea na kupiga vita rushwa.

Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, mahakama na vyombo vya dola kama polisi, rushwa imeelezwa kusitawi sehemu hizo kinyume na matarajio ya wananchi.

Wananchi wengi wamekuwa wakivilalamikia vyombo hivyo kwa mwenendo usioridhisha unaopelekea wananchi wengi kukosa haki zao mbele ya vyombo vya sheria.

Sasa swali ni je, kama mtu amekosa au ameporwa haki yake na vyombo vya sheria na ana yakini kabisa ile ni mali yake; akimbilie wapi?

Mafundisho ya Uislamu yanatufahamisha kwamba mwanaadamu kwa udhalimu wake; "Lau watu wangeaminiwa kwa madai yao tu; baadhi ya watu wangedai damu na mali ya watu wengine; lakini mshitaki anawajibika kutoa uthibitisho wa madai yake".

Katika suala la nyumba za Wakf mtaa wa Somali na Mchikichi; Bw. Daniel anadai ni zake kwa hoja kwamba alipewa usimamizi wa mirathi ya Hajat Aziza Omar. Na kwa kibali hicho cha kusimamia mirathi Bw. Daniel anadaiwa kuuza nyumba hizo kwa Bw. Pius Kipengele.

Kwa sheria za nchi hii mtu akipewa usimamizi wa miradhi huwa kibali cha kuchukua mirathi (mali) hiyo?

Waislamu wanavyo na wamewasilisha vielelezo vyote katika vyombo vya sheria kuthibitisha kwamba nyumba hizo zilikuwa mali ya Hajat Aziza Omar na kwamba alizitoa Wakf kwa shughuli za dini.

Wosia wenyewe hakuutoa kienyeji, lakini kwa kufuata taratibu zote za kisheria. Lakini leo vyombo hivyo vya sheria na vile vya dola vinasema nyumba hizo ni mali ya Pius/Daniel na ulinzi umetolewa kumhami Daniel.

Wakati huo huo Waislamu wanakamatwa kuwekwa rumande na kufunguliwa kesi. Anayelindwa leo na vyombo vya dola na kuambiwa "ishi" tu kwenye nyumba za Wakf ni zako; ni huyo huyo ambaye rikodi ziko katika vyombo hivyo hivyo vya dola kwamba ni mhalifu wa kosa la jinai alipoghushi hati za nyumba za Hajat Aziza kabla hajafariki.

Katika mazingira haya tuseme nini? Ni ule ule udhalimu dhidi ya Waislamu kama Mh. Rais alivyolalamikiwa siku ya Idd el Fitr! Ni rushwa; au ipo sheria mpya ambayo sisi hatuijui isiyotambua Wakfu au inayohalalisha mali ya marehemu kuporwa maadhali ni Hajat au Alhaj!

Vyovyote iwavyo, tungependa kusema hivi: Mtume wetu (s.a.w.) katika siku ya Arafa kama ya leo miaka 1410 iliyopita alituambia; "Enyi watu, hakika damu yenu (yaani uhai wenu), mali yenu na heshima yenu ni vitu vitukufu, katu visiharibiwe hadi mtakaposimama mbele ya Mola wenu, kwani utukufu wa vitu hivyo ni kama ulivyo utukufu wa siku hii, na mwezi huu na wa mji huu (wa Makka). Kwa hakika mtakutana na Mola wenu na atakuulizeni juu ya vitendo vyenu."

Hata wale ambao hawakubahatika kwenda Hija mwaka huu, lakini wapo katika mazingatio ya mafundisho yatokanayo na kupiga jamarati na kumwaga damu ya mnyama. Mali za Wakf ni vitu vitakatifu katu havitageuzwa baa wala Kanisa.

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook