Na Kipondo wa Changarawe
SI kawaida ya yeyote yule aisikiaye kwa sikio lake sauti ya Qur'an na maneno ya Mtume (s.a.w.) akaumwa na nyoka katika shimo moja mara mbili au zaidi. Si mwenendo wa mtu aliyefundishika na mafunzo ya Qur'an kupitia nyayo za Muhammad (s.a.w.) akajipiga kifua kuchora mstari baina yake na mwenendo wake katika kuyaendea maisha yake ya kila siku.
Kutakuwa na faida gani mtu akijitaabisha kwa kujikurupusha kila siku asubuhi na kuacha shughuli zake ili awahi safu ya mbele, akaacha chakula chake kwa mwezi, akafunga safari mguu mosi mguu pili mpaka Makkah, akavaa rubega na kupiga talbiya, kisha akakimbia baina ya Saffa na Marwa, akatufu na kusimama Arafa na kuchinja mnyama. Akafanya yote hayo kwa kuzingatia masharti na nguzo zake bila ya kinyongo.
Kisha baada ya hayo akawa yeye ndiye mtekelezaji hodari wa sera za kuwadhulumu viumbe vya Allah na kueneza fisadi kwenye ardhi, ufitini, majungu, uongo, ukachero, ukware, usengenyi na ubalakala ukawa ndio mtindo wa maisha yake. Majoho yote haya akayavaa kuwa furaha na ufakhari. Kuna faida gani. Kuna faida ikiwa dhulma inapitia mikoni mwake na kufanyika mbele ya macho yake.
Huu ni mchezo wa habari kweli kweli wa kumtupia kejeli Muumba ambaye anazimiliki pumzi za kila mtu, aliyeumba kila kitu na kukifanya kuwepo kutoka kwenye hakuna. Aliyemwumba mwanaadamu kutoka kwenye hali dhaifu, akamleta duniani akiwa kichanga kisichojimudu wala kumiliki chochote, akakipa nguvu na uwezo wa kuirithi dunia kwa muda maalum.
Pamoja na nguvu, elimu, mamlaka, zana, jeuri na machachari aliyonayo mwanaadamu; ukweli unabakia pale pale kuwa yeye ni mwenye kutoweka na kufutika kwenye uso wa dunia. Hakuna hata mmoja mwenye akili timamu atakayejinadi kuwa ataishi duniani milele. Kumbe kuna nguvu inayommiliki mwanaadamu iliyo kinyume na hiari na nguvu alizonazo.
Huu ni ukweli usiopingika. Wamepita mabingwa walioota pembe katika siasa za dhulma na ukandamizaji wakiwa na wapambe na washabiki. Waliwatii katika kila walilowaamuru. Hivi sasa yamebakia majina tu kwenye mabuku ya kihistoria.
Kuna jambo moja kubwa ambalo hutia nguvu, matumaini na faraja kwa kila anayepigania haki linalopatikana kutokana kufutika madhalimu waliotangulia pamoja na sera na siasa kwenye uso wa dunia. Ni kwamba walijitokeza wema waliosema kwa kauli na vitendo vyao kuwa dhulma ikome. Ijapokuwa wapenda haki hawa walionekana kuwa dhaifu na wachache bado walikuwa ndio chachu ya kuporomoka na kusambaratika kwa mifumo ya dhulma, waasisi na vinara wake.
Kanuni inayotawala katika mapambano yanayopelekea kwenye ushindi wa watu walio kwenye haki dhidi ya madhalimu ni moja tu. Ni pale wale wanaodhulumiwa watakapoamua kwa hiari yao kujikwamua kutoka kwenye mikono ya waonezi waliopora uhuru wao kwa mabavu au kwa kutumia vitanzi vya kivuli cha serikali, chama, bunge, mahakama n.k. Katika mapambano baina ya haki na batili kujitupa kwa Allah (s.w.) ndiyo siri ya ushindi na mafanikio dhidi ya udhalimu na madhalimu.
Katika maudhui zilizotangulia, dodoso lilijikita katika kuelezea ghilba za waonezi wenye kuendeleza na kudumisha dhulma kwenye jamii. Tukaona kuwa sababu ya kutoa mizizi na kushamiri uonezi na dhulma duniani ni kutowajibika kwa wale waliokabidhiwa jukumu la kuisimamisha haki, wamejifungia kwenye Misikiti na kulitelekeza jukumu hilo mikononi mwa watu wanaotumikia matashi ya nafsi na kimwili. Tukaona kuwa endapo tutatumia vyema falsafa ya "utamaduni wa kuku" tutaweza kungamua kwa wepesi janja janja ya madhalimu.
Leo dodoso linakusudia kuziendea aya zinazotuelekeza namna ya kujinasua kutoka kwenye mtego walioutega wakandamizaji ili kutunyonya. Neno mtego linamaanisha mifumo, miongozo na taratibu zote za maisha zilizobuniwa kutokana na udhaifu, uzoefu na ujuzi unaosukumwa na utashi wa binaadamu.
Kutokana na misingi iliyotumika katika kuziunda taratibu za maisha za wanaadamu daimahuwa ni za kinyonyaji kwa kuwa huwanufaisha na kuwastarehesha wachache kwa gharama za nguvu na kuvuja jasho kwa walio wengi. Ni wale tu waliojichimbia kwenye viti vya ufalme, usultani, urais, uwaziri, ubunge... na wale walio karibu katika kuwalinda ndio wenye kutumbua rasilimali iliyochumwa kupitia mikono ya wakulima, wafanyakazi, vibarua na wafanya biashara.
Kinyume chake utawaona walio wengi wanaangukia kwenye shimo la watu wa tabaka la chini, wanaohaha na kusaga lami kutwa kucha wakiishia kuambulia makoko pamoja na maumivu, machungu ya mwili uliochoshwa kwa kazi ngumu, kutokana na walivyokaliwa shingoni, wengi katika watu wa tabaka la chini na vizazi vyao ndio wanaoonekana kuyajaza magereza na sero katika nchi zote zisizofuata mwongozo wa Qur'an katika uchumi, siasa na mambo ya kijamii. Hii ndio hali halisi ya mifumo iliyobuniwa na wanaadamu, haki huwa ni za wale tu walio na nyadhifa katika serikali.
Wakati wale waliokalia viti wamejiwekea madaktari maalum wa kuwakagua afya zao kila siku wakiruka ng'ambo kwenda kupata matibabu, walipa kodi wakiumwa huwa hata kupata viasprini ni kwa mbinde. Wengi katika walipa kodi wa kipatwa na maradhi huwa kwao ni mtihani mara mbili, lakini kutokana na mazingira wanamoishi, ubovu wa huduma za jamii pamoja na lishe duni wao wanajikuta kuwa ndiyo gunia la mazoezi ya magonjwa mbalimbali.
Hakuna namna yoyote iliyobora ya kujinasua kutoka kwenye mtego wa madhalimu usipokuwa ni "kuhajiri". Kuhajiri ni istilahi inayowakilisha hatua muhimu za kuzifuata ili kujikomboa kutoka kwenye mirija na makucha ya wanyonyaji. Ni hatua kutoka kwenye mifumo ya maisha iliyobuniwa na wanaadamu kuelekea kwenye mfumo wa maisha wa haki na uadilifu uliotoka kwa Muumba wa ulimwengu na vilivyomo, Allah (s.w.) ambaye si mwenye kuhitaji chochote kutoka kwa viumbe bali viumbe vinamuhitajia Yeye.
Mwanaadamu ni kiumbe wa kimwili na kiroho aliyejaaliwa vipawa mbalimbali na Mola wake. Ana uwezo wa kufikiri na kutafakari, uwezo wa kujielimisha na kujitambua kwa hali ya juu pamoja na udadisi. Kutokana na vipawa hivi inakuwa ni vigumu sana kwa madhalimu kumtawala mwanaadamu bila ya kwanza kuiteka nyara akili yake kwa kuifanya izame katika mambo ya kipuuzi na kuitumikisha itii mashati ya kimwili.
Kwa kulitambua hili, viongozi madhalimu hujaza na kuhamasisha ulevi wa kila aina uwepo kwenye nchi zao. Pombe za aina mbalimbali, madawa ya kulevya, Makasino, minenguo yangoma na muziki chini ya kinyago cha sanaa na utamaduni, kuimarisha ushabiki katika michezo, filamu za X, mashindano ya urembo, magazeti ya penografia na mabaa.
Lengo ni kuwashughulisha watu wazame huko pamoja na akili zao. Mazezeta wanakuwa wengi sana kwenye jamii. Si Profesa, mwenye digrii wala wa darasa la saba wote mahututi kiasi ambacho kwa mtu anayeona, inakuwa ni vigumu sasa kuwatofautisha. Mtu hafikirii ila pombe, ngono huria, ndombolo, mpira na ushabiki. Katika mazingira haya, watu watadhulumiwa na kunyonywa bila ya upinzani.
Leo katika jamii yetu yametapakaa mabango ya kutangaza ulevi barabarani na kwenye kuta za nyumba, "salam" mapicha ya wenda wazi. Ukitembea unapishana na mabaa kama upishanavyo na daladala, mandombolo yamechachamaa mpaka kwenye majumba ya hoteli za Maustaadh. Dhana iliyojengeka vichwani mwao ni kwamba kila mteja ni mwanachama na mpenzi wa ndombolo na vichaa wa Marekani.
Tazama namna Allah (s.w.) anavyomjua vyema mwanaadamu! Jambo la awali lililowekwa na Qur'an ili watu waweze kujinasua kwenye mtego wa kudhulumiwa ilimu sahihi inayomwezesha mtu kujing'oa kutoka katika mambo yanayoharibika, kudumazana, kupumbaza akili. Akili iliyoviza ni muhali kujikomboa. Kisha Qur'an inawataka watu wachore mstari wa kuonyesha mpaka baina yao na pumbao za aina zote.
Hii ni hatua muhimu sana katika kupambana na dhuluma. Huiweka huru akili na kuipa wasaa wa kutafakari namna ya kuusimamisha mfumo wa maisha ya haki na uadilifu katika jamii na kuwakomboa watu kutoka kwenye himaya za madhalimu.
Inapaswa kuzingatiwa kuwa 'vidini' vyote vinavyojishughulisha na mambo yanayoitwa ya kiroho tu na kuacha sehemu ya maisha ya kijamii, siasa na uchumi ni pumbao (opiums), kwa sababu zinawatoa wazuri kwenye kuongoza jamii na kuwafungia mahekaluni, Makanisani, kwenye Masinagogi. Inabidi zihamwe kwa sababu zinaitekeleza jamii mikononi mwa madhalimu.
Kuna faida gani bai kuisumbua akili, kuchoma muda kwa kumwaga wito eti unajenga hoja kuwa Mungu anatakiwa kuabudiwa siku fulani, wakati hata ukikesha kuanzia Alhamisi ukaunganisha na Ijumaa ukiwa Msikitini au Kanisani unajisalia tu au kumwimbia Bwana hali ya kuwa umewaachia wale watumwa wa matashi ya kimwili kuwaongoza watu kwenye giza na kueneza sera za kuchafua maadili.
Dawa ni kushikamana na mwenendo mwema na kuonyesha madhara yanayoikumba jamii kutokana na kufuata mifumo ya maisha iliyobuniwa na wanaadamu jinsi inavyomomonyoa maadili, inavyowalinda madhalimu na inavyovuruga amani na kueneza fisadi. Sambamba na hilo ni kuionyesha jamii kwa vitendo namna mwongozo wa Qur'an unavyowakomboa wanaadamu chini ya viongozi waadilifu (Muttaq) wanaoandaliwa kupitia chuo cha sala, zakkat, swaumu na hijja. Hii ni hatua ya pili muhimu katika kupambana na udhalimu.
La mwisho katika kujinasua ni kukusanya nguvu, rasmi kwa ajili ya kuichambua mizizi ya ukandamizaji. Hatua hii uhusisha hata kuyahama makazi pamoja na mahali mtu alipozaliwa, kukata ushirikiano na wale wote wanaopiga vita harakati za kuing'oa dhulma. Kwa kifupi ni kujenga ukuta unaokata mahusiano yote isipokuwa yale ya kimapambano baina ya haki na batili mpaka kimoja kitoweke.
Hizi ndizo hatua walizopitia Mitume wote (s.a.) ambao ndiyo viongozi waliopigania kuusimamisha utaratibu wa maisha ulio wa haki na uadilifu na unaotoa haki kwa kila kiumbe. Ndizo nyayo waliozifuata waja wema wa zama zote waliopambana na kuuing'oa mifumo ya dhulma na kuusimamisha Uislamu badala yake. Hijira ndiyo njia muafaka ya kujinasua kutoka kwenye kitanzi cha waonezi.
Wakati tunaelekea lifunga dodoso ni vyema tukajikumbusha kuwa tayari wameshajitokeza wajiitao nambari wani; wakatuvamia kinyume cha sheria katika Misikiti huku wakitupa mkong'oto bila ya hatia, wakawasaka Masheikh usiku na mchana katika majumba yao na kuwarundika rumande, wakawavamia akinamama wa Kiislamu na kuwadhalilisha, na baya zaidi ni kule kutuua kwao hadharani kisha wakapongezana.
Kinachosikitisha ni ule ukimya uliopigwa na dereva wa chama nambari wani. Pamoja na mauaji, vitisho na kamata kamata vinaendelea, yeye kimya. Kisha baada ya masiku tele kupita, na afya za Waislamu waliosukumwa rumande kuwa mbaya na wengine kufa, inatoka kauli kuwa hakuwa hadhiri na ule unyama uliotendwa na wachapakazi pale Mwembechai. Pamoja na kukiri na kuahidi kuwa atashughulikia bado Waislamu kuna umuhimu wa kujinasua. Kwa sababu imekuwa ni kawaida ya serikali ya chama nambari wani kugeuza miili ya watu na Miskiti yetu kuwa ndiyo sehemu ya kufanyia mazoezi ya kupima nguvu za dola.
Sisemi kuwa tuhajiri, lakini basi ni njia gani iliyo bora zaidi kuliko ile waliopitia Mitume (a.s.) na waja wema ambao Allah (s.w.) aliwapa ushindi. Ni mafunzo gani yanayozidi ubora kuliko Qur'an na Sunnah ya Muhammad (s.a.w.).
Ningependa tumalize maudhui ya dodoso kwa kuzitafakari aya zifuatazo:
"Ewe uliyejifunika maguo, simama uonye, Mola wako umtukuze; na Mabaya uyahame (yapuuze) (74:1-5)
"Nasubiri juu ya hayo wayasemao (madhalimu) na uwahame (uwaepuke) mwepuko mwema". (73:10)
Hakika nyinyi muna mfano mzuri kwa Ibrahimu na wale waliokuwa pamoja naye; walipowaambia jamaa zao (madhalimu): Kwa hakika sisi tu mbali nanyi, na mbali na hayo mnayoyaabudu kinyume cha Allah (s.w.); tunakukataeni, umekwisha dhihiri uadui na bughudha ya daima baina yetu na nyinyi mpaka mtakapomwabudu Allah (s.w.) Peke Yake. Kwa yakini umekuwa mfano mzuri kwenu katika mwendo wao, kwa amwogopaye Allah na Siku ya Mwisho. Na anayepuuza haya basi Allah ni Mkwasi mwenye kusifiwa. (60:4,6).
|
|