Umuhimu na nafasi ya Ibada ya Hija katika Uislamu-2
Imesimuliwa kuwa Sahaba mmoja alieleza kuwa mke wake ameenda kuhiji, na yeye mwenyewe alijiandikisha kwa vita fulani vya Jihadi. Mtume (s.a.w) alimuamuru asiende kwenye vita na badala yake aende kuhiji. (Bukhari).
Mwanamke ambaye Hija imemuwajibikia na ambaye anaongozana na maharimu wake, hana budi kumtaka ruhusa mumewe. Kama mumewe atamnyima ruhusa, itabidi aende tu kwani mume hana haki ya kumkataza mkewe kutekeleza maamrisho ya Allah (s.w) bali anaweza kumkatalia kufanya kitendo cha Nawafil (Sunnah).
Amesimulia abdullah bin Umar kuwa wakati mmoja mwanamke tajiri alikataliwa kwenda safari ya Hija ya nyongeza. Shauri hili lilipofikishwa kwa Mtume (s.a.w) Mtume (s.a.w) alikubaliana na uamuzi wa yule mumewe. (Dar Qutni).
Kwa ujumla matendo yote ya Nawafil (Sunnah) wanawake watafanya kwa kutaka ruhusa kwa waume zao. Muislamu atakapokamilika kwa sifa zote hizi, (a)-(f) hana budi kuharakisha kukamilisha ibada hii ya Hija, ili baada ya muda asije akapungukiwa na baadhi ya sifa hizi na kushindwa kutekeleza ibada hii. Tukumbuke kuwa tukijichelewesha kufanya Hija kwa uzembe tu baada ya kuwa na uwezo tutakuwa mas-uul (wenye kuulizwa) mbele ya Allah (s.w), endapo tutaondokewa na uwezo wa kuhiji baada ya muda kupita. Daima mwanadamu hajui yanayokuja mbele yake. Mtu anaweza kufirisika au kupatwa na ugonjwa wa kudumu au kufa wakati wowote. Hivyo, daima Muislamu anatakiwa aharakie kutekeleza maamrisho ya Allah (s.w). Ni katika msingi huu Mtume (s.a.w) anatuusia:
"Yeyote anayekusudia kuhiji na aharakishe". (Abu Daud, Darimi).
Muda wa Hijja
Ibada ya Hija hufanywa katika muda maalum wa mwaka kama inavyosisitizwa katika Qur-an:
"Hija ni miezi maalum..." (2:197).
Miezi iliyowekwa kwa ajili ya Muislamu kunuia kuizuru Makka na Ka’ba kwa ajili ya Hija ni mwezi wa Shawwal, mwezi wa Dhul-Qaadah (mfungo pili) na siku kumi za mwanzo za mwezi wa Dhul-Hijah. Wakati wowote katika miezi hii mtu anaweza kwenda Makka kwa ajili ya Hija, lakini hataweza kufanya matendo ya Hija mpaka uianzie mwezi wa Dhul-Hija. Siku ya Hija ni kuanzia tarehe 8 Dhul-Hija mpaka tarehe 13 Dhul-Hija.
Mwenendo wa mwenye kunuia Hija au ‘Umra
Mwenye kunuia kuhiji katika miezi hiyo iliyotajwa, analazimka ajipambe na tabia nzuri. Ajizuilie na maneno na matendo machafu na maovu. Ajitahidi kuishi na watu kwa wema, awatake radhi kwa yale yote mabaya aliyowatendea na azidishe kuwatendea wema. Allah (s.w) anatuagiza:
"... Na anayekusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika hiyo Hija. na kheri yoyote mnayoifanya Mwenyezi Mungu huijua ...." (2:197).
Mwenye Kuhiji au kufanya ‘Umra anatakiwa ajipambe na tabia hiyo njema kwa kipindi chote atakapokuwa safarini. Yafuatayo ni mambo muhimu anayotakiwa ayazingatia mtu anapokuwa katika safari ya Hija au Umra.
(i) Ajiepushe na maneno maovu na machafu pia ajiepushe na vitendo viovu na vichafu.
(ii) Azidishe kusoma Qur’an na Kuswali swala za faradhi kwa jamaa, kuswali swala za sunnah, kuomba msamaha na kutubu kikweli kwelikwa Mola wake.
(iii) Ajitahidi kuwa mwema na mpole kwa wasafiri wenzake, kuongea nao vizuri, kuwapa msaada wanaohitajia, kuwasamehe kwa kosa lolote watakalomfanyia, kujizuia na hasira na kuvumilia maudhi mengi yanayotokana na wasafiri wenzake au wenyeji wa sehemu za Hijja.
(iv) Ajitahidi kuchanganyika na wasafiri wenzake kutoka sehemu mbalimbali, ajitahidi kujihusisha kwenye mikutano na mazungumzo ya kheri na kujaribu kubadilishana mawazo na wenzake kutoka sehemu mbali mbali ambao wanaelewana lugha, juu ya kuusimamaisha Uislamu ulimwenguni.
(v) Ajitahidi kuinamisha macho yake katika makundi yenye mchanganyiko wa wanawake na wanaume na kila itakapowezekana ajiepushe kuwa katika mchanganyiko wa wanaume na wanawake.
Vituo vya kunuia Hija
Miongoni mwa mambo muhimu kwa wenye kuhiji au kufanya ‘Umra ni kufahamu vituo ambapo watanuia kuanza kuhiji rasmi na kuvalia vazi la Ihram. Vituo hivi huitwa Miiqaat. Miiqaat ni vituo maalum vilivyowekwa katika njia za sehemu mbali mbali za kuingilia sehemu takatifu (Haram) ya Makka ambapo mahujaji wakifika humo huvua nguo zao za kawaida na kuvalia vazi rasmi la Ihram na kunuia rasmi kuanza ibada ya Hija au ‘Umrah. Vituo vya kunuia Hijja alivyoviweka Mtume (s.a.w) kwa watu wa kutoka kila upande ni hivi vifuatavyo:
(i) Zul-Hulaifa: - ni kituo cha watu wanaotoka sehemu za Madina. Kituo hiki kiko umbali wa kilometa 450 kutoka Makka. Hivi sasa kituo hiki kinajulikana kwa jina la Bir-‘Ali.
(ii) Juhfah: Kituo hiki kiko umbali wa Kilometa 187 Kaskazini-Magharibi ya Makka. Ni kituo cha watu wanaotoka sehemu za Misr, Sham (Syria), n.k. Hivi sasa kituo hiki kinajulikana kwa jina la Rabigh.
(iii) Qurnul Manazil: - Kituo hiki kiko umbali wa Kilometa 94 mashariki ya Makka na ni kituo cha watu kutoka mji wa Najd. Kituo hiki hivi sasa kinajulikana kwa jina la Sail.
(iv) Yalamlam: Kituo hiki kiko umbali wa kilometa 54 kusini magharibi ya Makka: Ni kituo cha watu kutoka Yemen na sehemu nyingine za kusini kama vile Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kusini, n.k.
(v) Makka: Wakazi wa Makka watavalia Ihram na kunuia Hija au ‘Umra humo humo majumbani mwao. Vile vile wakati wa vituo vingine, vilivyotajwa hapo juu, watanuia Hija au ‘Umra na kuvalia Ihram humo humo majumbani mwao. Vituo hivi vitano vimebainishwa katika hadith ifuatayo:
Amesimulia Ibn abbas (r.a) kuwa Mtume wa Allah ameweka Dhul-Hulaifa kama Miiqaat ya watu wa Madina; Al-Juhfa kwa watu wa Sham (Syria); Qarn ul-Manaazil kwa watu wa Najd; na Yalamlam kwa watu wa Yemen. Kwa hiyo hivi ni vituo (Mawaaqiit) kwa wale wote wanaoishi katika vituo hivi na wale wanaopitia katika vituo hivi kwa nia ya Kuhiji au kufanya ‘Umra na yoyote anayeishi katika sehemu hizi atavalia Ihram nyumbani kwake, hali kadhalika wakazi wa Makka wanaweza kuvalia Ihram humo humo Makka. (Bukhari).
(vi) Dhaaru-Irq: Kituo hiki kipo umbali wa kilomita 94 kaskazini-mashariki ya Makka. Ni kituo cha watu wa Iraq, Iran, n.k. Kituo hiki hakikuwekwa na Mtume (s.a.w) bali kiliwekwa na ‘Umar bin Khattaab (r.a) alipokuwa Khalifa kama tunavyofahamishwa katika Hadith ifuatayo:
Amesimulia Ibn Umar (r.a): Wakati miji hii miwili (Basra na Kuufa) ilipotekwa, watu walikwenda kwa ‘Umar (r.a) na kusema: Ee Amir wa Waumini, Mtume (s.a.w) ameweka Qarn kama Miiqaat ya watu wa Najd, lakini iko kinyume kabisa na njia yetu na ni vigumu sana kwetu kupitia hapo. Akasema, (Umar), fanyeni kituo (miiqaat) chenu katika sehemu iliyo kinyume na Qarn ambayo iko katika njia yenu ya kawaida. kwa hiyo aliiweka Dhaaru-irq kama Miiqaat. (Bukhari)
(vii) Jiddah: Miiqaat ya Wasafiri wa ndege. Kama ilivyosisitizwa katika hadith watu kutoka sehemu mbali mbali wanalazimika kuvalia Ihram na kunuia Hija au ‘Umra katika vituo vilivyowekwa endapo watapitia humo. Ilivyo ni kwamba vituo vyote hivi vilivyotajwa katika hadith hizi vinapitiwa na wasafiri wa gari au wanyama. Wasafiri wengi wanaotoka nchi za mbali husafiri kwa ndege mpaka Jiddah na hapo ndipo wanapovalia Ihram na kunuia Hija au ‘Umra. Jiddah iko kilomita 72 kutoka Makka.
Ihram
Mwenye kunuia Hija au ‘Umra katika Miiqaat anakuwa katika hali ya kuchunga masharti kadhaa mpaka akamilishe matendo kadhaa ya Hija au ‘Umra. Hali hii ya kuchunga masharti hujulikana kwa jina la "Ihram".
Wanaume wanapokuwa katika Ihram hulazimika kuvaa vazi rasmi la Ihram. Vazi la Ihram kwa wanaume ni kuvaa shuka mbili nyeupe zisizo shonwa. Shuka moja hufungwa kiunoni na mkanda huweza kutumika ili kuhakikisha isivuke. Shuka la pili huvaliwa lubega kwa kufunika bega la kulia na kuacha wazi bega la kushoto. Katika hali ya Ihram, ni haram kwa mwanamume kuvaa nguo nyingine yoyote, ni haramu kufunika kichwa, ni haram kuvaa socks au kuvaa viatu vinavyofunika miguu.
Wanawake hawana vazi rasmi la Ihram. Akiwa katika Ihram Al-hajat analazimika kama kawaida kujifunika mwili wake wote isipokuwa uso na viganja vya mikono na atavalia ushungi. Hijab yaweza kuwa ya rangi yoyote isiyovutia kama kawaida ya vazi la mwanamke wa Kiislamu lakini vazi jeupe ni bora. Mwanamke akiwa katika Ihram ni haramu kufunika uso au kuvaa gloves. Pia wanawake katika Ihram hawaruhusiwi kuvaa socks wala kuvaa viatu vinavyofunika miguu.
Yaliyoharamishwa kwa Mwenye kuwa katika Ihram
Mwenye kuwa katika Ihram (Muharrim) ameharamishiwa yafuatayo:
(i) Kujamii (kufanya tendo la ndoa) au kubusu au kukumbatiana au kufanya vitendo vingine vya kimapenzi kati ya mume na mke ambavyo vitawaletea fikra za kufanya tendo la ndoa.
(ii) Kusema maneno maovu na machafu kama vile kusengenya, kugombana, kugombanisha, kusema uwongo, kubishana, n.k.
(iii) Kutenda maovu na machafu.
Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an:
Na anayekusudia kufanya Hija katika (miezi) Hiyo basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika hiyo Hija ... (2:197).
(iv) Kunyoa au kung’oa nywele, kukata kucha au kukata au kupunguza sehemu yoyote ya mwili ila kwa matibabu kama vile kuumika, kutolewa damu kwa ajili yamatibabu, n.k.
(vi) Kuoa au kufanya mipango ya ndoa au hata kupeleka posa.
(vii) Kujipaka manukato
(viii) Kuvaa nguo ya rangi yenye kuvutia
(ix) Kwa wanaume kuvaa nguo iliyoshonwa, na kufunika kichwa.
(x) Kwa wanawake kufunika uso na kufunika viganja vya mikono kwa kuvaa glovu (gloves).
(xi) Kuvaa viatu vinavyofunika miguu na kuvaa socks.
(xii) Kuwinda au kusaidia kuwinda angalau kwa kuonyesha mnyama anayewindwa.
(xiii) Kula nyama iliyowindwa au iliyopatikana kwa msaada wa mtu aliyekuwa katika Ihram.
(xiv) Kula mayai ya ndege waliopatikana kwa kuwindwa.
Kafara kwa mwenye kuvunja masharti ya Ihram
Allah (s.w) kwa Urehemevu wake, ametoa nafuu kwa wale watakaovunja masharti ya Ihram kwa kutoa fidia isipokuwa kwa kosa la jimai. Tunafahamishwa katika Qur-an:
"... Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au ana vya kumuudhi kichwani mwake (akafanya yaliyokatazwa, kama vile kunyoa), basi atoe fidia kwa kufunga au (kwa kutoa) sadaqa au kuchinja mnyama ..." (2:196)
Katika Hadith tunafahamishwa:
Ka‘ab bin Ajra (r.a) ameeleza: "Nilipokuwa katika (hali ya) Ihram kwa ajili ya ‘Umra nilisumbuliwa sana na chawa kichwani mwangu. Mtume wa Allah (s.a.w) akaniambia ninyoe kisha nifunge siku tatu au nichinje mbuzi wa sadaqa au niwalishe maskini sita. (Bukhari, Muslim, Abu Daud).
Kwa hiyo kwa Muharim atakayevunja sharti lolote la Ihram atalazimika kutoa kafara kwa ama (i) kufunga siku 3 au (ii) kumchinja mbuzi na kuitoa nyama yake sadaqa au (iii) kulisha maskini sita.
Kufanya tendo la ndoa ni kosa lisilosameheka kwa kutoa kafara bali hubatilisha Hija au ‘Umra moja kwa moja. Ama kwa mume aliyefanya mapenzi na mkewe kwa kubusiana na kumkumbatia bila ya kufanya kitendo cha ndoa, atatoa kafara ya ngamia (au thamani yake) kama atatokwa na manii na kama hatatokwa na manii, atatoa kafara ya mbuzi.
Kafara kwa mwenye kuwinda au kuonyesha windo akiwa katika Ihram ni mbuzi iwapo mnyama huyo ana ukubwa wa mbuzi, au mdogo zaidi kuliko hivyo; vinginevyo atatoa kafara ya mnyama aliye sawa na huyo aliyemuwinda au atatoa thamani yake anunue vibaba vya chakula kinacholiwa sana katika sehemu hiyo, na kumlisha kila maskini kwa vibaba vitakavyopatikana. Hivi ndivyo tunavyoagizwa katika Qur-an:
Enyi mlioamini! Msiue mawindo na hali ya kuwa mmo katika Hija au ‘Umra. Na miongoni mwenu atakayemuua makusudi basi malipo yake yatakuwa kwa (kuchinja) kilicho sawa na alichokiua katika wanyama wanaofugwa kama watavyohukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe ilipo Ka‘aba (akachinjwe na kutolewa sadaqa huko) au badala ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake (hili). Mwenyezi Mungu ameyafuta yaliyopita; lakini atakayefanya tena Mwenyezi Mungu atamuadhibu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye Nguvu na Mwenye kuadhibu. (5:95).
Aina za Hija
Kuna aina tatu za Hija ambazo kila mwenye kuhiji ana uhuru wa kuchagua mojawapo kulingana na uwezo wake wa kukidhi masharti ya kila aina. Aina hizi ni (i) Ifraad, (ii) Qiran na (iii) Tamattu kama zianvyoelezwa katika hadith ifuatayo:
Amesimulia Aysha (r.a): "Tulitoka na Mtume wa Allah (s.a.w) (kwenda Makka) katika Hija ya Mtume ya kuaga. Miongoni mwetu tulivaa Ihram kwa nia ya kufanya `Umra tu (al-tamattu) wengine kwa Hija na `Umra pamoja (al-Qiran) na kwa wengine kwa Hija tu (al-Ifraad). mtume wa Allah (s.a.w) alivaa Ihram kwa nia ya Hija tu. kwa hiyo kwa yule aliye vaa Ihram kwa hija tu au kwa Hija na `Umra pamoja, hakutoka katika Ihram mpaka siku ya kuchinja (kutoa muhanga yaani siku ya mwezi 10 Dhul-Hija). (Bukhari).
(i) Ifraad: Ni aina ya Hija ambapo, "Hajj" anavaa Ihram kwa nia ya kufanya Hija tu bila ya "Umra na katika ( ) Talbiya ataanza kutikia mwito wa Allah (s.a.w ) kwa:( ) yaani "Nimeitika kwa Hija." Hajj hatavua Ihram yake mpaka amalize matendo yote ya Hija yanayomlazimu kuwa katika Ihram. Hija huruhusiwa kuvua Ihram na kutoka kwenye masharti yake baada ya kutupa mawe kwenye mnara na kunyoa au kupunguza nywele siku ya mwezi 10 Dhul-Hija. Kwa yule aliyechagua aina hii ya Hija halazimiki kuchinja siku ya mwezi 10 Dhul-Hija.
(ii) Qiran: Ni aina ya Hija ambapo Haji huvaa Ihram kwa nia ya kufanya Hija na ‘Umra pamoja na katika talbiya ataanza kutikia mwito wa Allah kwa: ( ) - yaani "Nimeitika kwa Hija na ‘Umra’. Hajj katika aina hii ya Hija hatavua Ihram mpaka baada ya kuchinja na kufanya Tawaful-Ifadha (tawafu ya nguzo) siku ya mwezi 10 Dhul-Hija.
Aina hii ya Hija inafanywa na wale wanaokuja Makka na wanyama. Katika Hija yake ya kuaga, baada ya kumaliza ibada ya ‘Umra, Mtume (s.a.w) aliwaamrisha watu wote wavue Ihram ila kwa wale waliokuja na wanyama.
(iii) Tamattu: Katika aina hii ya Hija, Haji anapofika katika Miiqaat yake huvaa Ihram kwa nia ya kufanya ‘Umra tu na ataitikia mwito wa ( ) - yaani "Naitikia kwa ‘Umra’. Baada ya kumaliza ‘Umra atanyoa au kupunguza nyewele na kuvua Ihram au kuwa huru na miiko yote ya Ihram. Atavaa tena Ihram kwa nia ya Hija mnamo mwezi 8 Dhul-Hija, na atabaia na Ihram mpaka amalize Hija ya mwezi 10 Dhul-Hija kama ilivyo katika aina nyingine za Hija.
Katika aina hizi tatu za Hija, At-Tamattu ndio aina bora zaidi na yenye nafuu kubwa kwa wale wanaotoka mbali wasioweza kuja na wanyama, ama kwa wakazi wa Makka au majirani wa Makka ambao wana uwezo wa kwenda na wanyama, Hija iliyo bora kwao ni hii ya Al-Qiran. Lakini wenye kuhiji Hija ya Tamattu wanalazimika kununua mnyama na kumchinja siku ya mwezi 10 Dhul-Hija kama tunavyofahamishwa katika Qur’an:
"... Na mtakapokuwa kwenye salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya `Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliyesahilika (mbuzi au kondoo). Na asiyepata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba atakaporudi (kwake; hizi ni kumi kamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawako karibu na msikiti Mtakatifu wa Makka. na mcheni Mwenyezi Mungu na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa Kuadhibu." (2:196).
Matendo ya Hija na ‘’Umra
Matendo yote yanayokamilisha Ibada ya ‘Umra na aina zote za Hija ni haya yafuatayo:
1. Ihram na nia ya Hija na ‘Umra
2. Talbiya
3. Tawaf
4. Sa’i
5. Matendo ya siku ya Tarwiya (8 Dhul-Hija)
6. Siku ya Arafa (9 Dhul-Hija)
7. Kulala Muzdalifah (usiku wa kuamkia 10 Dhul-Hija)
8. Matendo ya siku ya kuchinja (siku ya Idd - 10 Dhul-Hija)
9. Matendo ya siku za Tashriq (11, 12, 13 Dhul-Hija)
10. Tawaful-Widaa (Tawaf ya kuaga)
1. Ihram na Nia ya Hija au ‘Umra
Matendo ya Hija au ‘Umra huanza rasmi kwa kuvalia vazi la Ihram. Kama tulivyoona Ihram huvaliwa nyumbani au katika vituo maalum - Mawaaqiit - vilivyowekwa na Mtume (s.a.w) kabla ya kuingia kwenye uwanja Mtakatifu wa Makka. Wakazi wa Makka huvalia Ihram nyumbani kwao.
Utaratibu unaofuatwa ni kwamba Hajj, kabla ya kuvaa Ihram, ni sunna kunyoa nywele za makwapani na sehemu nyingine za mwili, kupunguza nywele za kichwani, kunyoa ndevu na kukata kucha. Kisha ni sunnah kukoga, kutawadha na kupaka manukato ndipo uvalie Ihram. Ni vyema kuvaa Ihram wakati wa swala mojawapo ya faradhi. Mtume (s.a.w) katika Hija ya kuaga alivaa Ihram wakati wa swala ya Adhuhuri.
Kabla ya kutia nia ya aina ya Hija au ‘Umra, Haji ataswali rakaa mbili za sunnah, kisha mara tu baada ya kutoa salaam atanuia aina ya Hija anayokusudia kuifanya, na ataitikia wito wa Allah (s.w) kulingana na nia yake.
Kama nia yake ni ya kufanya I‘Umra (At-Tamattu) ataitika:
Ee Allah nakutikia kwa ‘Umra.
Kama nia yake ni ya kufanya Hija na ‘Umra (Al-Qiran) ataitika:
Ee Mola. Naitika kwa Hija na ‘Umra.
Kama nia yake ni ya kufanya Hija tu (Al-Ifraad) ataitikia:
Ee Mola, Naitika kwa Hija
2. Talbiya
Talbiya ni maneno ya kutikia wito wa Allah (s.w) pale alipomuamrisha Nabii Ibrahim (a.s) kuwaita watu kwa Hija:
"Na (tukamwambia Ibrahim): Utangaze kwa watu habari za Hija, watakujia (wengine) kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyokonda (kwa uchovu wa safari ndefu). Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja jina la Mwenyezi Mungu katika siku zinazojulikana ..." (22:27-28).
Maneno ya kuitikia wito huu wa Allah, yaani maneno ya Talbiya, kama yalivyo katika hadith iliyosimuliwa na Abdullah bin Umar (r.a) ni haya yafuatayo:
"Labbayka Allaahumma labbayka. Labbayka laashariika laka labbayaka. Innal-hamda wanni-i-mata laka wal-mulka; laashariika laka".
Tafsiri:
"Naitika wito wako Ee Allah, Naitika. Naitika, Ewe Usiye na Mshirika, Naitika. Hakika sifa zote njema na neema zote ni zako na Ufalme ni Wako, Ewe Usiye na Mshirika" (Bukhari na Muslim).
Wanaume wataitika kwa sauti ya juu na wanawake wataitika kwa sauti ndogo. Kwa wale walionuia kwa Hija tu au Hija na ‘Umra, talbiya huanza mara baada ya kuvaa Ihram na kunuia, mpaka watakapotupa jiwe la kwanza katika mnara mkubwa -"Jamratul’Aqaba" siku ya mwezi 10 Dhul-Hija.
Talbiya ya ‘Umra huanzia kwenye Miiqaat baada ya kuvaa Ihram na kutia nia ya ‘Umra mpaka kwenye Nyumba Takatifu ya Ka‘aba. Kwa wale walionuia Hija ya "Tamattu", wataanza Talbiya tena baada ya kuvalia Ihram kwa nia ya Hija siku ya mwezi 8 Dhul-Hija, na wataendelea mpaka wakati watakapoanza kutupa jiwe la kwanza kulenga mnara mkubwa siku ya mwezi 10 Dhul-Hija.
Wakati wa kwenda Makka talbiya itarudiwa tena na tena. Isomwe kila baada ya swala ya faradh, kila Hajj anapopanda na kuteremka katika kipando au chombo anachosafiria, na kila akipanda na akiteremka mlima, kila anapokutana na msafara mwingine. Mtume (s.a.w) alifanya hivyo pamoja na maswahaba wake alioongozana nao katika Hija ya kuaga. Kila alipotaka Waislamu wasome talbiya aliwaamrisha kwa kusema "Takbiir". Kisha Masahaba wake na yeye mwenyewe walianza kusoma Talbiya kwa nguvu.
3. Tawaf
Kutufu ni kitendo cha kuizunguka Ka’aba mara saba kuanzia kwenye Jiwe Jeusi (Hajaral aswad). Wakati wa kuzunguka Ka’aba inakuwa upande wa kushoto, yaani mzunguko ni kinyume na ule wa saa (anti-clockwise). Kutufu ndio Ibadah ya kwanza anayoifanya mwenye kuhiji au kufanya ‘Umra mara tu baada ya kuizuru Ka’aba na kubusu Jiwe Jeusi.
Masharti ya Tawaf
Mwenye kutufu hana budi kuwa twahara. Yaani awe ameepukana na najisi na aina zote za hadath - asiwe na janaba, hedhi wala nifasi na awe na udhu.
Kwa wanawake wenye hedhi wanaruhusiwa kuingia katika Ihram na kufanya vitendo vyote vya Hija isipokuwa kutufu kama tunavyofahamishwa katika hadith ifuatavyo:
Amesimulia Aisha (r.a): Nilikuwa katika hedhi nilipoingia Makka, kwa hiyo sikuweza kutufu wala kusali. Kisha nilimfahamisha Mtume wa Allah, akaniambia, ‘fanya vitendo vyote vya Hija kama wengine lakini usitufu mpaka uwe twahara.: (Bukhari).
Namna ya Kutufu
Kama kawaida ya kila ibadah, mwenye kutufu atatia nia ya kutufu na ataanza tawafu kwa kulibusu Jiwe Jeusi kisha atasema: "Bismillaah Allaahu Akbar". Kama, kutokana na msongamano wa watu haitawezekana kulibusu "Jiwe Jeusi", basi inatosha kwa kuligusa kwa mkono au kwa fimbo kisha kuubusu mkono au fimbo na kusema: "Bismillaah Allahu Akbar". Kama vile vile itashindikana kuligusa jiwe jeusi kwa mkono au kwa fimbo, basi itatosha kuashiria kwa mbali kwa mkono au fimbo bila kubusu mkono au fimbo hiyo, kisha utasema: "Bismillaah Allaahu Akbar". Hivi sasa kuna alama ya mastari mweupe uliochorwa ili kuwawezesha wale wanaozunguka mbali na "Jiwe Jeusi" kujua kuwa wamefika usawa na Jiwe Jeusi ili waashirie (Angalia picha).
|
|